Nafasi Ya Matangazo

March 30, 2023

Naibu waziri wa Nishati Stephen Byabato na viongozi waandamizi wa Tanesco wakifurahia baada ya uzinduzi wa mpango wa miaka minne wa masuala ya jinsia kwa shirika la umeme Tanzania TANESCO
Mkurugenzi wa TANESCO Maharage CHande (Kulia) akisalimiana na Naibu waziri Mara baada ya kuwasili kwenye ukumbi.
Sehemu ya washiriki
Naibu waziri wa Nishati Stephen Byabato akikata utepe kuashiria uzinduzi wa programu ya miaka minne ya masuala ya jinsia
Na Neema Mbuja, DODOMA
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa kushirikiana na Benki ya Dunia kupitia mradi wa kusafirisha umeme mkubwa kutoka Tanzania hadi Zambia (TAZA) imezindua mpango wa miaka minne wa masuala ya jinsia unaoanza kutekelezwa chini ya Benki ya dunia
Progamu hii imezinduliwa na Mgeni Rasmi na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Stephen Byabato ukiwa na lengo la kutatua changamoto wanazokutana nazo wafanyakazi wanawake katika maeneo yao ya kazi na kuongeza uwiano wa utendaji kazi baina ya wanawake na wanaume kati ya mwaka 2023 hadi 2026.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mpango huo, Mhe. Byabato alisema TANESCO imejizatiti kwa kiasi kikubwa kwenye usawa wa kijinsia na kuitaka menejimenti ya Shirika hilo kuhakikisha inaanzisha kitengo maalumu cha jinsia ili kuwepo na uwanja mpana wa kujadili masuala ya kijinsia.

"Naiagiza menejimenti ya TANESCO kupitia mradi wa TAZA kuhakikisha wanawake wanapewa kipaumbele sawa na wanaume na kuongeza fursa zaidi kwa wanafunzi wa vyuo ambao wanajiandaa kuajiriwa kwenye ajira rasmi".

Akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Bw. Maharage Chande alisema kuwa Shirika tayari lilishaanza kutekeleza programu ya masuala ya jinsia, ila kupitia mradi wa TAZA masuala ya kijinsia yataongezwa kwenye sera na taratibu za Shirika.

Ameyataja maeneo ya kipaumbele kuwa ni pamoja na sera ya Shirika kutoa kipaumbele kwenye masuala ya jinsia, upatikanaji wa taarifa sahihi za masuala ya jinsia kwenye taasisi na kuwepo kwa nafasi za mafunzo ya ukuzaji taaluma kwa wafanyakazi wanawake hasa wanaofanya kazi za kiufundi ili kuwajengea uwezo kupitia mpango wa mafunzo kazini.

Mradi wa TAZA unatekelezwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Nishati na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kupitia mkopo wa Jumuiya ya  Maendeleo ya Kimataifa (IDA) ya Benki ya Dunia, mkopo wa Mfuko wa Maendeleo wa Ufaransa (AfD), Umoja wa Nchi za Ulaya (EU) na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Posted by MROKI On Thursday, March 30, 2023 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo