Nafasi Ya Matangazo

March 17, 2023

Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Bw. Maharage Chande akifafanua jambo kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini walipotembelea kituo cha kupokea na kupoza umeme mkubwa wa kilovoti 400/220/132/33 cha Chalinze mkoani Pwani siku ya Ijumaa, 17 Machi 2023.
Meneja Mradi wa Kituo cha kupokea na kupoza umeme mkubwa wa kilovoti 400/220/132/33 cha Chalinze, Mha. Newton Livingstone akitoa maelezo ya mradi huo kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini walipotembelea mradi huo siku ya Ijumaa, 17 Machi 2023.
Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Stephen Byabato akiongea na waandishi wa habari (hawapo kwenye picha) wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini walipotembelea kituo cha kupokea na kupoza umeme mkubwa wa kilovoti 400/220/132/33 cha Chalinze mkoani Pwani siku ya Ijumaa, 17 Machi 2023.


**********
Na Neema Mbuja, Chalinze
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imefanya ziara katika kituo cha kupokea na kupoza umeme mkuwa wa kilovoti 400/220/132/33 cha Chalinze mkoani Pwani pamoja na njia ya kusafirisha umeme mkubwa wa kilovoti 400 kutoka katika mradi wa bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere (JNHPP).

Kamati hiyo ilitembelea kituo hiko ili kujionea maendeleo ya ujenzi wa miradi hiyo inayotekelezwa na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na kuwataka Wizara ya Nishati pamoja na TANESCO kuhakikisha wanakamilisha kwa wakati miradi hiyo miwili kabla ya kukamilika kwa mradi wa  bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere (JNHPP).

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Dustan Kitandula (Mbunge) alipokuwa akizungumza wakati wa majumuisho ya ziara ya Kamati hiyo.
Mhe. Kitandula amesema kamati imeridhishwa na utekelezaji wa mradi hiyo na kuongeza kuwa itasaidia sana katika uwekezaji mkubwa na kukuza uchumi wa nchi yetu.

"Uchumi wa nchi unakuwa kwa kasi sana sambamba na mahitaji ya upatikanaji wa umeme hivyo TANESCO hakikisheni mnaweka msukumo mkubwa kwenye miradi hii" alisema Mhe. Kitandula.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Stephen Byabato amesema kukamilika kwa mradi huu wa kituo cha kupokea na kupoza umeme cha Chalinze ambao unafadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa asilimia mia moja utanufaisha mikoa mbalimbali kwa kuongeza hali ya ubora na uhakika wa upatikanaji wa umeme wa uhakika utakaoingizwa katika Gridi ya Taifa.

Aidha, Mhe. Byabato ameishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuidhinisha fedha za kugharamia miradi hii ambapo hapo awali mradi huu wa kituo cha kupokea na kupoza umeme cha Chalinze ulikuwa ufadhiliwe na mradi wa North Grid kabla ya Serikali kuamua kuanza kuufadhili mradi huo kwa asilimia mia moja.

Naye Meneja mradi wa kituo hiki cha kupokea na kupoza umeme cha Chalinze, Mhandisi Newton Livingstone amesema kuwa mradi huu unajumuisha miradi miwili ambayo ni njia ya kusafirisha umeme mkubwa kutoka bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere (JNHPP) hadi kituo Cha chalinze kwa msingi wa kilovoto 400 yenye urefu wa kilomita 160 wenye thamani ya dola za kimarekani milioni 51.5 na shilingi bilioni 39.12 pamoja na kituo cha kupokea na kupoza umeme mkubwa wa kilovoti 400/220/132/33 cha Chalinze wenye thamani ya dola za kimarekani milioni 44.06 na shilingi bilioni 30.85 kitakachohusisha ufungaji wa mashine umba sita zenye uwezo wa Megavoti 250 kila moja.

Ujenzi huu wa mradi wa kituo cha kupokea na kupoza umeme cha Chalinze kwa sasa umefikia asilimia 59 wakati ambapo kwa upande wa njia ya kusafirisha umeme mkubwa wa kilovoti 400 kutoka JNHPP umefikia asilimia 92.
Posted by MROKI On Friday, March 17, 2023 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo