Nafasi Ya Matangazo

October 15, 2015

 Habari zilizotufikia hivi punde zinaarifu kuwa Mwanasiasa Mkongwe nchini Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha NLD, Dk Emmanuel Makaidi (74) amefariki dunia hii leo mchana.

Dk Makaidi pia alikuwa ni  Mwenyekiti Mwenza wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) unaoundwa na vyama vya NLD, Chadema, CUF, na NCCR Mageuzi.

Kifo cha Makaidi kimethibitishwa na Viongozi wenzake wa NLD ambao wanadai kupata taarifa kutoka kwa mjane wa marehemu Modesta Ponera.


Makaidi ni Mgombea Ubunge wa Tano kufariki tangu akuanza kwa Kampeni za Uchaguzi mwaka 2015.  

Wagombea hao ni Mohamed Mtoi wa CHADEMA jimbo la Lushoto,  Celine Kombani wa CCM jimbo la Ulanga Mashariki, Estomih Malla wa Chama cha ACT-Wazalendo Mgombea Ubunge jimbo la Arusha Mjini, Dk Abdallah Kigoda wa CCM Jimbo la Handeni Mjini na, Dk Emmanuel Makaidi wa NLD jimbo la Masasi.


Dk Emmanuel Makaidi ni mhandisi aliyebobea. Alizaliwa Aprili 10, 1941 huko wilayani Masasi mkoani Mtwara. Baba yake mzazi alikuwa ni katekista wa Kanisa la Anglikana.

Alianza elimu katika Shule ya Msingi Namalenga wilayani Masasi kati ya mwaka 1948 – 1952, mwaka 1953 – 1954 alisoma katika Shule ya Kati (Middle school) iitwayo Luatala hukohuko Masasi. Baadaye alijiunga na Shule ya Sekondari ya Chuo cha Mtakatifu Joseph na kusoma kidato cha kwanza hadi cha nne kati ya mwaka 1953 hadi 1956.

Makaidi alisoma darasa la 13 na 14 (kidato cha tano na sita) katika Shule ya Sekondari Luhule, Uganda kati ya mwaka 1957 – 1958. Alipelekwa Uganda si kwa sababu ya kipato cha baba yake, la hasha, alisaidiwa na Askofu wa Anglikana baada ya kuona anafaulu mitihani yake kwa alama za juu sana. SOMA ZAIDI BOFYA  HAPA
Makaidi aliendelea kufadhiliwa na askofu huyo ambaye alimuunganisha na mashirika mengine na kumtafutia chuo Afrika ya Kusini. Akapelekwa Chuo Kikuu cha Witwatersrand na kuhitimu Shahada ya Uendeshaji na Usimamizi kati ya mwaka 1958 – 1960.

Baada ya kuhitimu vizuri pale Witts, aliendelea kupata ufadhili wa masomo ya shahada ya uzamili, mara hii alielekea Marekani na kusoma masuala ya Menejimenti na Utawala kwa ngazi ya uzamili kati ya mwaka 1960 – 1962. Alisoma pia katika Chuo Kikuu cha Howard kilichoko jijini Washington, Marekani.

Baada ya kurejea nchini akiwa mhitimu wa M.A, Makaidi alianza kazi serikalini mwaka 1966 hadi mwaka 1973 akiwa mchambuzi kazi mkuu, katika kitengo cha Utumishi.

Kati ya mwaka 1974 na 1975 (miaka miwili). Alirudi tena Marekani na kusoma Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Sayansi ya Siasa katika Chuo Kikuu cha Howard akipata kuwa karibu na mmoja wa maprofesa nguli duniani, Wamba Dia Wamba. Makaidi ameniambia kuwa hata tabia ya kuandika vitabu na kutunga mambo ya ubunifu, alifundishwa na profesa huyu mahiri.

Aliporejea nchini kwa mara ya pili mwaka 1976 aliendelea na kazi yake pale Utumishi hadi mwaka 1985 alipopewa kazi nyingine kubwa zaidi, akawa Mkurugenzi wa Miundo na Mishahara kwenye kamati iliyokuwa inashughulikia mashirika ya umma nchini.

Wakati anaendelea na kazi utumishi, alipata fursa nyingine ya kusomea stashahada ya Kuchakata Taarifa za Kielektoniki katika Chuo Kikuu cha Trinity, Ireland. Alikwenda huko na kuhitimu mwaka huohuo 1977.

Kabla hajafanya kazi katika kamati maalum ya kusimamia mashirika ya umma akapandishwa cheo na kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kazi na Ustawi wa Jamii na mwaka huohuo 1985 akafukuzwa kazi.

Kisa cha Makaidi kufukuzwa kazi serikalini, tena akiwa na wadhifa huo ilikuwa ni kwa sababu ya kuandika kitabu cha Kiingereza chenye jina “mwanasiasa mwenye roho ya shetani”. Serikali ikamzonga vilivyo, ikamtuhumu kuwa kitabu kile kinamtukana Mwalimu Julius Nyerere. Mwisho wa siku “kazi ikaota mbawa”.

Bahati nzuri, mwaka huohuo 1985 akaajiriwa na Shirika la Finwork Directory kuwa Mkurugenzi Mtendaji, kazi aliyoifanya hadi mwaka 1991.

Kuanzia mwaka 1992 hadi hivi leo, Dk Makaidi hajajishughulisha tena na kazi za serikalini wala mashirika binafsi. Amejiajiri akiwa na kampuni kadhaa zilizoajiri Watanzania wa vipato vya kawaida, lakini pia ameendelea kutoa ushauri wa kitaalamu kwa kampuni za ndani na nje ya nchi huku akiongoza chama cha NLD akiwa Mwenyekiti.

Dk Makaidi ni mwandishi mzuri wa vitabu, ameshaandika zaidi ya 10. Amemuoa Modesta Ponela na wana watoto wanane.


MBIO ZA UBUNGE
Dk Makaidi alijitosa katika mbio za ubunge kwa mara ya kwanza mwaka 2010 katika Jimbo la Masasi, Mtwara akipambana na Mariam Kasembe wa CCM (aliyeibuka mshindi wa jumla kwa asilimia 63.7) na Clara Mwatuka wa CUF (aliyepata asilimia 15.2). Katika uchaguzi huo Dk Makaidi alishika nafasi ya tatu kwa kupata kura 5,384 sawa na asilimia 11.7 ya kura zote zilizopigwa.

Januari 2014, Dk Makaidi alikuwa mmoja wa Watanzania walioteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kuwa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba ambalo liliendeleza mchakato wa kikatiba, ulioanzishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

MBIO ZA URAIS
Kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005, Dk Makaidi alipitishwa na chama chake, NLD, kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ni mmoja wa wagombea waliofika katika maeneo kadhaa ya nchi kuomba kura pamoja na kuwa chama chake hakikuwa na nguvu kubwa ya kisiasa na hata uchumi. Kwenye uchaguzi ule ambao mshindi alikuwa Kikwete, Dk Makaidi alipata asilimia 0.19 ya kura zote zilizopigwa na kushika nafasi ya saba kati ya wagombea 10 waliokuwa wanashindana.
Posted by MROKI On Thursday, October 15, 2015 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo