Nafasi Ya Matangazo

February 26, 2015

Tarehe 24/02/2015 katika Mahakama ya Wilaya ya Mpwapwa Mkoa wa Dodoma, mtu mmoja anayefahamika kwa jina la YUSUPH CHATAMBALA, umri miaka 45, kabila Mchaga, Mkulima na mkazi wa Kijiji cha MAKUTUPA Kata ya Lupeta Wilayani Mpwapwa Mkoa wa Dodoma, amehukumiwa kifungo cha maisha jela kwa kosa la KUNAJISI mtoto wa miaka mine (4).


Mwendesha Mashitaka wa Polisi katika Mahakama ya Wilaya ya Mpwapwa Mkaguzi Msaidizi wa Polisi  GODWILL S. IKEMA (A/Insp) akisoma mashitaka Mahakamani alisema, Mtuhumiwa alitenda kosa la KUBAKA lililo kinyume cha sheria za nchi chini ya Kifungu namba 130 (1) 2 (a) na 131 (1) cha Kanuni ya Adhabu kama kilivyofanyiwa mapitio mwaka 2002. 

YUSUPH CHATAMBALA alitenda kosa hilo siku ya tarehe 20/02/2015 saa 12:00 jioni, huko kijiji cha Makutupa Wilaya ya Mpwapwa Mkoa wa Dodoma, ambapo alimbaka mtoto mdogo wa kike mwenye miaka 04 (jina limehifadhiwa). Alitenda kosa hilo baada ya kumkamata alipokuwa akicheza na watoto wenzake jirani na nyumbani kwao kisha kumpeleka kwenye shamba la mahindi kisha KUMNAJISI mtoto huyo na kusababishia majeraha na maumivu makali.


Mtuhumiwa alifikishwa mahakamani siku ya tarehe 23/02/2015 na kusomewa shitaka lake, ambapo alikiri kutenda kosa hilo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya ya Wilaya ya Mpwapwa Mh. PASCHAL F. MAYUMBA. Siku ya tarehe 24/02/2015 alifikishwa tena Mahakamani hapo na kusomewa tena shitaka lake na kukiri tena kutenda kosa hilo.


Hakimu Mkazi  Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Mpwapwa Mh. PASCHAL  F. MAYUMBA alimtia hatiani mtuhumiwa huyo baada ya kukiri kutenda kosa hilo. Akisoma hukumu hiyo; Mh. Hakimu Mkazi Mfawidhi,  alisema Mahakama inamhukumu kwenda Jela Kifungo cha Maisha kwa kosa la Kumnajisi mtoto ili kuwa fundisho kwake na kwa wengine wanaotenda makosa kama hayo.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi D. A. MISIME – SACP alithibitisha kuwepo kwa tukio hilo na hukumu iliyotolewa dhidi ya mtuhumiwa huyo. Kamanda Misime alisema Makosa ya Unyanyasaji wa Kijinsia yamekuwa yakichukuliwa hatua kali kutokana na uelewa wa wananchi juu ya ubaya wa vitendo vinavyofanywa na kutolea taarifa bila woga katika Madawati yanayoshughulikia kesi hizo katika vituo vya Polisi. Alisisitiza kuwa wananchi waendelee kushirikiana na Jeshi la Polisi kuwafichue wahalifu wa makosa yote na kuyafanya makazi yao kuwa sehemu salama ya kuishi na kujiletea maendeleo bila hofu dhidi ya wahalifu.



Imetolewa na Idara ya Habari na Matukio Polisi Mkoa wa Dodoma.
KNY: Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma 
Picha iliyotumika ni ya Gereza Kuu la Kigali Nchini Rwanda
Posted by MROKI On Thursday, February 26, 2015 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo