Nafasi Ya Matangazo

January 23, 2013

KAMATI YA RUFANI YA UCHAGUZI TFF YAAHIDI HAKI
Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imeahidi wadau wa mchezo huo kuwa itafanya kazi zake kwa misingi ya haki.

Akizungumza baada ya uzinduzi wa Kamati hiyo uliofanywa Dar es Salaam leo mchana (Januari 23 mwaka huu) na Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah kwa niaba ya Rais wa TFF, Leodegar Tenga, Mwenyekiti wa Kamati hiyo yenye wajumbe watano Idd Mtiginjola amesema wapo kwa ajili ya kutenda haki.

Mtiginjola amesema Kamati yao inaundwa na watu waadilifu, hivyo watafanya kazi kwa kuzingatia kanuni zilizopo na sheria nyingine za mpira wa miguu ikiwemo Katiba husika.

“Niwakikishie kuwa hatutafanya uamuzi kutokana na mawazo yetu, tufanya uamuzi kwa kuzingatia kanuni na sheria. Kamati hii ni chombo cha haki, hivyo itafanya kazi zake kwa kuzingatia sheria. Sheria na haki ni vitu viwili tofauti. Sheria zipo kwa ajili ya kuitafuta haki,” amesema Mtiginjola ambaye kitaaluma ni Mwanasheria akiwa ni Wakili wa Kujitegemea.

Baada ya uzinduzi, Osiah aliwakabidhi wajumbe wa kamati hiyo vitendea kazi (instruments) mbalimbali zikiwemo kanuni za uchaguzi za TFF na wanachama wake, Katiba ya TFF na Katiba ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).

Mbali ya Mtiginjola, wajumbe wengine wanaounda kamati hiyo ni Makamu Mwenyekiti, Francis Kabwe ambaye ni Naibu Msajili wa Mahakama Rufani ya Tanzania, Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Tanzania, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Mohamed Mpinga ambaye pia kitaaluma ni Mwanasheria.

Mshambuliaji wa zamani wa timu ya Reli Morogoro, Profesa Madundo Mtambo ambaye kwa sasa ni Mkufunzi katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) kilichopo mjini Morogoro, na mdau wa soka Murtaza Mangungu ambaye pia ni Mbunge wa Kilwa Kaskazini.
Posted by MROKI On Wednesday, January 23, 2013 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo