Nafasi Ya Matangazo

November 08, 2026



WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Serikali imechukua hatua za kufanya bei ya saruji kuwa himilivu kwa kuondoa kodi kwenye saruji inayoagizwa kutoka nje na malighafi zinazotumika kuizalisha.


Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, akihutubia wananchi katika viwanja vya Stendi ya Mwanhuzi, wilayani Meatu, mkoani Simiyu, Novemba 7, 2026. Katika mkutano huo, alisema zaidi ya shilingi bilioni 330 zimeingia kwenye Mfuko wa Barabara ndani ya mwezi mmoja.                                                                                                           
 



Amesema hayo leo (Jumapili, Novemba 8, 2026), wakati akizungumza na wananchi katika Viwanja vya Shule ya Msingi Nyamikoma, Kata ya Kabita, Wilaya ya Busega, akihitimisha ziara yake ya kikazi mkoani Simiyu.

Dkt. Mwigulu amesema Serikali inatambua kupanda kwa bei za vifaa vya ujenzi, ikiwemo saruji, na imechukua hatua kupunguza gharama zinazochangia bei hizo.

“Tumefuta kodi kwenye saruji inayoagizwa na tumefuta kodi kwenye malighafi zinazotengeneza saruji,” amesema.

Ameeleza kuwa saruji itakayozalishwa kwa malighafi yenye gharama nafuu, pamoja na itakayoagizwa baada ya kuondolewa kwa kodi, inatarajiwa kusaidia kufanya bei kuwa himilivu katika siku zijazo.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka watumishi wa umma kuacha kuwanyima wananchi huduma kwa kisingizio cha kutokuwa na miadi, wakati watumishi hao wapo ofisini na wanaweza kuwahudumia.

Amesema baadhi ya wananchi hutumia fedha nyingi kufuata huduma, hivyo kuwataka warudi siku nyingine bila sababu za msingi kunawaongezea gharama na usumbufu.

“Lazima tujue kuzifikia ofisi za umma, baadhi yetu wanakuwa wameingia gharama. Wengine wanatumia zaidi ya laki moja na nusu, wengine laki mbili,” amesema.

Kwa upande wa afya, Dkt. Mwigulu ameelekeza wagonjwa wa dharura, wakiwemo wajawazito waliozidiwa na uchungu na majeruhi, wapatiwe matibabu mara moja bila kucheleweshwa na taratibu za usajili.

“Majeruhi amefika anahitaji huduma ya kwanza ya haraka, mkimbizeni akatibiwe, mtamwandikishia pale pale. Siyo kusubirisha mtu ambaye anahitaji matibabu ya dharura, mnamsubirisha mapokezi,” amesema.

Vilevile, amesisitiza kuwa wagonjwa wanaohitaji kupelekwa hospitali za rufaa hawapaswi kuchangishwa fedha za mafuta ya ambulansi za Serikali.

Amesema Serikali imenunua magari hayo na kuajiri madereva ili yaokoe maisha ya wananchi, hivyo wasimamizi wahakikishe yanakuwa tayari kutoa huduma.

Kuhusu dawa, Waziri Mkuu amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama kufuatilia kila mwezi fedha za dawa na matumizi yake, na kuwasilisha taarifa ili hatua zichukuliwe pale uvujaji utakapobainika.

Amehoji sababu za wagonjwa kuendelea kuelekezwa kununua dawa katika maduka binafsi wakati taarifa anazopewa zinaonesha utoshelevu mkubwa wa dawa katika vituo vya Serikali.

Aidha, Dkt. Mwigulu amesisitiza kutoshikilia vitendea kazi vya wananchi, vikiwemo bodaboda, bajaji na magari, kwa makosa ambayo adhabu yake ni faini.

Amesema mamlaka zinazohusika zifuatilie malipo ya faini kwa mujibu wa sheria bila kuzuia shughuli zinazowaingizia wananchi kipato.

“Haya mambo ya kutokujali mitaji ya watu yanarudisha nyuma maendeleo ya watu. Wengine ni mikopo hivyo vitendea kazi vyao,” amesema.
Posted by MROKI On Sunday, November 08, 2026 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo