Makatibu Wakuu wanaosimamia sekta za Uchukuzi, Mawasiliano na Hali ya Hewa kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wamekutana jijini Arusha kukamilisha maandalizi ya Mkutano wa 20 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Uchukuzi, Mawasiliano na Hali ya Hewa (Transport, Communications and Meteorology Sectoral Council – TCM), unaotarajiwa kufanyika Julai 10, 2026.
Mkutano huo wa ngazi ya Makatibu Wakuu umejadili na kupokea taarifa ya wataalamu waliokutana kuanzia Julai 6 hadi 8, 2026, kuhusu utekelezaji wa maamuzi ya mkutano uliopita wa TCM pamoja na maendeleo ya miradi na programu za kikanda zinazolenga kuimarisha miundombinu, kurahisisha shughuli za usafiri na biashara na kuongeza ushirikiano kati ya nchi wanachama.
Miongoni mwa masuala muhimu yaliyojadiliwa ni maendeleo ya ujenzi wa miundombinu ya barabara, reli, usafiri wa anga na majini, uboreshaji wa Vituo vya Huduma kwa Pamoja Mipakani (One Stop Border Posts – OSBPs), pamoja na kuimarisha mifumo ya ubadilishanaji wa taarifa za hali ya hewa.
Akifungua mkutano huo, Naibu Katibu Mkuu wa Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki anayesimamia Sekta za Miundombinu, Uzalishaji, Jamii na Siasa, Bw. Andrea Aguer Ariik, alibainisha kuwa EAC inaendelea kupiga hatua kubwa katika kuendeleza miundombinu ya uchukuzi na mawasiliano, hatua ambazo zinachangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa uchumi na maendeleo ya kijamii katika ukanda.
“Hadi sasa tumepiga hatua tunazostahili kujivunia. Kwa mfano, takribani kilomita 15,000 za mtandao wa reli zinatumika na kuendelea kujengwa katika nchi wanachama, hususan Tanzania na Kenya, hatua hii itachochea muunganiko wa kikanda na kurahisisha mwingiliano wa watu na bidhaa,” alisema Bw. Ariik.
Mkutano wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Uchukuzi, Mawasiliano na Hali ya Hewa ni jukwaa muhimu la kufanya maamuzi ya kisera yanayolenga kuimarisha mtangamano wa kikanda kupitia maendeleo ya miundombinu ya kisasa, usafiri salama na wenye ufanisi, pamoja na huduma bora za mawasiliano na hali ya hewa kwa manufaa ya wananchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo umeongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Dkt. Charles Msonde, akiwa ameambatana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi – Zanzibar, Mhandisi Ali Said Bakari, Mkurugenzi Mtendaji TCAA, Dkt. Jabiri Kuwe Bakari, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASHICO), Bw. Eric B. Hamissi, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dkt. Ladislaus Benedict Chang’a, pamoja na maafisa wengine waandamizi kutoka wizara na taasisi mbalimbali za Serikali.





.jpg)






0 comments:
Post a Comment