Mwanza — Katika hatua inayoonesha dhamira ya dhati ya wanawake viongozi kushiriki katika maendeleo ya jamii, taasisi ya Ladies of New Millennium ikiongozwa na Mama Tunu Pinda imefanya ziara mkoani Mwanza kutembelea miradi ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) inayotekelezwa chini ya Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (PSSN).
Wanawake hao, waliotoka katika nyanja mbalimbali za uongozi na uanaharakati wa kijamii, walifanya ziara ya siku kadhaa katika Wilaya ya Ilemela, ambako walishuhudia mafanikio ya mpango huo katika maeneo ya elimu, ujasiriamali na nishati safi ya kupikia.
Wakiwa katika Shule ya Sekondari ya Igogwe, waliona maboresho ya miundombinu ya elimu yaliyofanikishwa na TASAF, hatua inayowezesha wanafunzi kutoka kaya masikini kupata mazingira bora ya kujifunzia. Pia walikutana na vikundi vya wanawake wajasiriamali walioinuliwa kupitia mpango huo kwa mafunzo na mikopo midogo, hatua iliyowaimarisha kiuchumi.
Ili kuendeleza harakati za kuhamasisha nishati salama na rafiki kwa mazingira, taasisi hiyo iligawa mitungi ya gesi kwa walengwa, wakisisitiza kuwa afya ya familia na mazingira bora ni nguzo muhimu ya maendeleo endelevu.
Katika ziara hiyo, wajumbe hao walikutana na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Bw. Balandya Mayuganya, ambaye aliwapa taarifa za utekelezaji wa mpango huo katika mkoa huo na mafanikio yaliyopatikana.
Kwa upande wa TASAF, Bw. Japhet Boaz, Mkurugenzi wa Mifumo, Tathmini na Mawasiliano, alieleza kuwa zaidi ya kaya milioni moja zimenufaika na mpango huo katika nyanja mbalimbali ikiwemo elimu, afya na ajira za muda, na kuongeza kuwa TASAF inaendelea kujenga uwezo wa walengwa kushiriki kikamilifu katika maendeleo yao.
Wanawake hao walitoa saluti kwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendeleza jitihada za kupambana na umaskini na kuhakikisha wananchi wote wanashiriki katika uchumi wa taifa.
Wajumbe waliotembelea miradi hiyo ni Mama Tunu Rehani Pinda, Asina Kawawa, Blandina Mususa, Suzana Charles Majua na Frida Rugemalira – wote wakionesha namna wanawake wanaweza kuwa sehemu ya suluhisho kwa changamoto za kijamii kupitia ushawishi na matendo yao.
Ziara hiyo imeweka wazi kuwa wanawake wana nafasi muhimu siyo tu kama walengwa wa maendeleo, bali kama waratibu, wachochezi na wadau muhimu wa mabadiliko chanya katika jamii.
0 comments:
Post a Comment