Balozi wa Tanzania amekutana na Rais wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Kisiwa cha Anjouan na ujumbe wake na kuwahimiza kuzidisha uagizaji wa bidhaa toka Tanzania kwa kuzingatia ukaribu wa kijiografia na uhusiano wa kihistoria uliopo.
Balozi Yakubu ambaye yuko ziarani kisiwa cha Anjouan aliwaeleza wafanyabiashara hao kuwa hivi sasa kutokana na maboresho na mageuzi ya sekta ya biashara chini ya uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kuna urahisi mkubwa wa mauzo kwa wageni wanaohitaji bidhaa na hivyo ni wakati muafaka wa kuagiza kutoka Tanzania.
Balozi Yakubu pia alitumia fursa hiyo kusikiliza changamoto wanazozipata katika biashara wawapo Tanzania na kuwaahidi kuwapatia ufumbuzi kwa mawasiliano na taasisi husika za Tanzania na kuwaeleza pia kuwa kuanzia Oktoba Mosi kutakuwa na usafiri wa ndege baina ya Tanzania na Comoro kwa siku zote saba za wiki na nne kati ya hizo ndege itafika kisiwa cha Anjouan.
Kwa upande wake,Rais wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Anjouan,Alilfata Ibrahim alimshukuru Balozi Yakubu kwa ujio wake katika ofisi zao na kumuahidi ushirikiano na kumuomba suala la tofauti ya bei baina ya raia wa kigeni na wananchi wa Tanzania hususan katika vyombo vya usafiri liangaliwe upya ili kuongeza wingi wa abiria toka Comoro.
Ziara hiyo ni ya kwanza ya Balozi Yakubu katika kisiwa cha Anjouan tangu alipowasili katika Umoja wa Visiwa vya Comoro mwezi Mei mwaka huu.
0 comments:
Post a Comment