Nafasi Ya Matangazo

August 23, 2024

Mgeni rasmi ambaye ni Mkuu wa Wilaya Siha, Dkt. Christopher Timbuka aliipongeza CYCT kwa juhudi zake za kuwaleta pamoja vijana na jamii katika jitihada za kuokoa misitu ya Mlima Kilimanjaro.
Na Mwandishi Wetu.

Shirika la Connecting Youth Connecting Tanzania (CYCT) limefanya uzinduzi wa Mradi wa Urejeshaji na Ulinzi wa Misitu ya Kilimanjaro Magharibi na Kaskazini uliofanyika katika uwanja wa West Kilimanjaro Forest (Simba Gate).
Tukio hilo lililohudhuriwa na wadau mbalimbali pamoja na wananchi wa maeneo ya Kilimanjaro.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Mhifadhi Mkuu PCO Robert Faida alipongeza jitihada na kuahidi kutoa ushirikiano ili kupata matokeo chanya, pia kutoa eneo la kutekeleza mradi.
PCO Faida amesema kuwa mradi huu unaofadhiliwa na GEF/UNDP kupitia Mpango wa Ruzuku Ndogo (Small Grant Programme - SGP), unalenga kurejesha uoto wa asili wa maeneo yaliyoathirika kutokana na mabadiliko ya tabianchi na shughuli za kibinadamu, kusaidia jamii zinazozunguka hifadhi kupitia ufugaji nyuki na kuazisha vitalu mashuleni vya miche ya matunda na mingine.

Ameongeza kuwa zaidi ya ekari 15 za misitu zitarejeshwa kwa kupandwa miti ya asili, huku jamii ikielimishwa na kuhamasishwa kuhusu umuhimu wa kuhifadhi mazingira.
Kwa upande wake mgeni rasmi ambaye ni Mkuu wa Wilaya Siha, Dkt. Christopher Timbuka aliipongeza CYCT kwa juhudi zake za kuwaleta pamoja vijana na jamii katika jitihada za kuokoa misitu ya Mlima Kilimanjaro.

"Mradi huu ni mfano bora wa jinsi vijana wanavyoweza kuongoza juhudi za kuhifadhi mazingira na kuchangia maendeleo endelevu ya taifa letu," alisema Dkt. Timbuka.
Shirika la CYCT, kupitia mwakilishi wake Bw. Peter Kayombo, lilieleza kuwa mradi huu ni sehemu ya mkakati wa muda mrefu wa shirika hilo katika kuhakikisha kuwa vijana wanakuwa mstari wa mbele katika kulinda mazingira.

"Tunaamini kwamba ushirikiano na jamii ni msingi wa mafanikio ya mradi huu. Tunafurahi kuona jinsi ambavyo wananchi wameupokea kwa mikono miwili mradi huu, na tutaendelea kushirikiana nao kuhakikisha tunafikia malengo tuliyojiwekea," alisema Bw. Peter.

Kwa ujumla, uzinduzi wa mradi huu umeashiria mwanzo mzuri wa safari ya kurejesha misitu ya Kilimanjaro Magharibi na Kaskazini, huku wananchi wakiwa na matumaini makubwa ya kunufaika na mradi huu kwa namna mbalimbali.
 
Posted by MROKI On Friday, August 23, 2024 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo