Nafasi Ya Matangazo

May 30, 2024

Mkuu wa Mkoa wa Manyara Bi. Queen Sendiga, akipokea nyenzo za kufundishia   elimu ya fedha na majarida mbalimbali ikiwemo jarida lenye elimu ya uwekezaji kutoka kwa Afisa Mkuu Usimamizi wa Fedha kutoka Wizara ya Fedha, Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Bw. Salim Kimaro, baada ya kufika Ofisini kwake kabla ya kuingia kwenye kikao cha Baraza la Biashara la Mkoa kutoa elimu ya fedha kwa wajumbe wa kikao hicho wakiwemo Wakuu wa Wilaya takribani zote za Mkoa huo kujadili masuala mbalimbali ya kiutendaji.
Wajasiriamali, wafanyabiashara na wananchi wa Kata ya Magugu Wilaya ya Babati Vijijini Mkoani Manyara wakifuatilia filamu ya mafunzo ya elimu ya fedha, yenye maudhui mbalimbali ikiwemo madhara ya kukopa bila malengo, madhara ya kukopa sehemu ambazo hazijasajiliwa, kuweka fedha kwenye vikundi ambavyo havijasajiliwa, matumizi mabaya ya fedha binafsi na mambo ya kuzingatia kabla ya kukopa fedha, mafunzo hayo yameandaliwa na Wizara ya Fedha, walipotembelewa na  baadhi ya watumishi wa Wizara ya Fedha kupewa elimu ya fedha.
Timu ya wataalamu wa kutoa mafunzo ya elimu ya fedha kutoka Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais -TAMISEMI, wakiwa katika kikao na Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Bi. Queen Sendiga (katikati) Ofisini kwake, mjini Babati, ambapo moja ya mazungumzo yao ni pamoja na kutambulishana na kumweleza lengo la kufika Mkoa wa Manyara na kutaja baadhi ya maeneo waliyotoa elimu ya fedha na maeneo wanayoelekea kutoa elimu hiyo katika Mkoa huo baada ya kumaliza kutoa elimu hiyo kwa wajumbe wa kikao cha Baraza la Biashara.
Washiriki wa kikao cha Baraza la Biashara la Mkoa, wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kikao hicho, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Bi. Queen Sendiga, pamoja na Wakuu wa Wilaya mbalimbali za Mkoa wa Manyara na viongozi wengine wa Serikali, wakipata elimu ya fedha kutoka kwa Afisa Mkuu wa Usimamizi wa Fedha kutoka Wizara ya Fedha Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Bw. Salim Kimaro (hayupo pichani) ambao licha ya agenda mbalimbali za kikao cha Baraza walipata fursa ya kupata elimu ya fedha.
***************
Na Asia Singano, WF, Manyara.
Watoa huduma za fedha mkoani Manyara wametakiwa kufuata sheria na taratibu za Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ikiwemo kujisajili, kutoza viwango sahihi vya riba na kuwapa nakala za mikataba wakopaji baada ya wao kuelewa mkataba wa makubaliano ya kukopa na kusaini ili kuepuka adhabu mbalimbali zitakazotolewa kwa wanaokiuka sheria za huduma za fedha.

Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Bi. Queen Sendiga, ofisini kwake alipokutana na baadhi ya watumishi wa Wizara ya Fedha kabla hawajaingia kwenye kikao cha Baraza la Biashara lililofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara, kutoa elimu ya fedha kwa wajumbe wa kikao hicho.

Alisema kuwa Serikali inaendelea kufanya uchunguzi kuwabaini wanaofanya biashara ya kutoa huduma za fedha bila leseni, ambapo baadhi yao wamekuwa wakikamatwa na kuadhibiwa huku akiwaonya wafanyabiashara wasiofuata kanuni, taratibu na sheria ya huduma za fedha kusajili biashara zao kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

‘’Wafanyabiashara wanaofanya biashara zao bila kujisajili, bila kufuata sheria, waache na Serikali ipo kazini tumekuwa tukiwakamata na tutaendelea kuwakamata na sheria itachukua mkondo wake’’ Alisema Bi. Sendiga.

Aliipongeza Wizara ya Fedha kwa kutoa elimu ya fedha katika mkoa wake kutokana na mkoa huo kuwa na uhitaji mkubwa wa elimu ya fedha, kwakuwa wananchi wengi wamekuwa wakijiingiza kwenye mikopo kwa wafanyabiashara wasio waaminifu na baadae kusababisha umasikini.

‘’Kwanza nichukue fursa hii kuwashukuru sana Wizara ya Fedha, kupitia Hazina kwa kuja na mpango huu mzuri wa kutoa elimu ya fedha, maeneo makubwa ambayo wanaathirika ni pamoja na watumishi wa Umma na wafanyabiashara wadogowadogo, sisi kama Mkoa tuna changamoto hiyo pia kwa baadhi ya wananchi wetu’’ Alisisitiza Bi. Sendiga.

Kwa upande wake Mwl.  Hamisi  Maginga mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, alisema kuwa kukosa elimu ya fedha kumechangia baadhi ya walimu kujiingiza kwenye mikopo mingi iliyosababisha baadhi yao kupata msongo wa mawazo kutokana na kuwa na mikopo iliyokithiri kutoka kwenye taasisi zenye riba kubwa.

“Tumekuwa na tatizo kubwa sana hasa kwenye sekta yetu ya elimu, walimu wamekuwa na tabia ya kuwa na mikopo mingi, mpaka inafikia hatua hawawezi kuhimili mahitaji ya familia zao, na wengine imefikia hatua mpaka  kadi zao za benki zinabaki huko kwa taasisi za fedha’’ Alisema Mwl. Maginga.

Naye Afisa Mkuu wa Usimamizi wa Fedha, kutoka Wizara ya Fedha, Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Bw. Salim Kimaro, alisema kuwa Wizara ya Fedha itahakikisha kuwa elimu ya fedha inawafikia wananchi wote kutokana na umuhimu wa elimu hiyo.

“Lengo la program hii ni kuhakikisha kwamba wananchi wote wanafikiwa na kupewa elimu ya fedha, na chimbuko lake ni baada ya utafiti mdogo kufanyika na kubaini kwamba wananchi hawana uelewa mkubwa na wa kutosha wa elimu ya fedha na hivyo wanaendelea kusaidiwa kwa kila hali, kupewa mikopo na hawajikwamui kumbe wanachokosa ni elimu ya fedha’’ Alisema Bw. Kimaro.

Wizara ya Fedha ilianza kutoa elimu ya fedha katika maeneo ya Mijini kupitia Maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha kwa Mikoa ya Dar Es Salaam, Mwanza na Arusha, ambapo kwa sasa programu hiyo imejikita kuwafikia wananchi walioko Vijijini kwa lengo la kuwaongezea uelewa wa masuala ya fedha ili waweze kufanya maamuzi sahihi katika mahitaji na matumizi ya Huduma za Fedha.
Posted by MROKI On Thursday, May 30, 2024 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo