Katika jitihada za kuzuia na kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa watoto nchini, wazazi na walezi wametakiwa kufanya uchaguzi sahihi na kuwatambua bodaboda wanaowapeleka watoto wao shule ili kuepuka vitendo hivyo.
Rai hiyo ilitolewa Februari 22, 2024 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP THEOPISTA MALLYA wakati akitoa elimu kwa wanafunzi wa shule ya Msingi QUEEN OF THE APOSTLES iliyopo Wilaya ya Mbozi Mkoani Songwe.
Kamanda Mallya amesema “Serikali imeendelea na mikakati mbalimbali ya kuhakikisha vitendo vya unyanyasaji na ukatili wa kijinsia vinatokomezwa katika jamii hivyo wazazi hawana budi kuchagua bodaboda mmoja au wawili wanaowafahamu ili kuzuia ukatili wa kijinsia.
Aidha, Kamanda Mallya amekemea tabia ya wazazi kuwapakiza watoto kwenye Bodaboda bila ya uangalizi wa mtu mkubwa, "mwanafunzi yeyote mwenye umri chini ya miaka 09 asipande pikipiki akiwa peke yake na ukimuona mtu anakuita ili akupe lift unatakiwa kukataa na kutoa taarifa kwa mwalimu au mzazi ili aweze kuchukuliwa hatua za kisheri" alisema Kamanda Mallya.
Sambamba na hayo, ameitaka jamii kutambua kuwa, kila mzazi/mlezi ana jukumu la kuhakikisha ulinzi wa mtoto wake ikiwemo kumpa mahitaji muhimu kama vile chakula, malazi, mavazi na ulinzi ili kuepuka kuongezeka kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia katika maeneo yetu.
Kamanda Mallya Alihitimisha kwa kuwataka wanafunzi hao kutoa taarifa ya vitendo vya ukatili wa kijinsia pindi waonapo au wafanyiwapo vitendo hivyo kwa Jeshi la Polisi, Wazazi, Walimu, Viongozi wa dini au mtu yoyote wanaemuamini ili kutokomeza vitendo hivyo katika maeneo yao.
0 comments:
Post a Comment