Nafasi Ya Matangazo

January 30, 2024

Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akijibu swali la Mbunge wa Kisesa, Mhe. Luhaga Mpina, kuhusu kiasi cha fedha ambacho Serikali imewalipa wazabuni na wakandarasi wa ndani baada ya kuwasilisha madai yao na kufanyiwa uhakiki, bungeni Jijini Dodoma.

Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akiteta jambo na Waziri wa Ujenzi, Mhe. Innocent Bashungwa (kulia), bungeni Jijini Dodoma.(Picha na Kitengo cha Mawasiliano, WF, Dodoma)
*************
Na. Khadija Ibrahim, WF, Dodoma
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb), ameliambia Bunge, Mjini Dodoma kuwa katika kipindi cha Mwaka wa Fedha 2016/2017 hadi Desemba 2023, imewalipa wazabuni na wakandarasi wa ndani zaidi ya shilingi trilioni 2.1 kati ya madai ya zaidi ya shilingi trilioni 3.1 yaliyowasilishwa.
 
Dkt. Nchemba amesema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Kisesa, Mhe. Luhaga Mpina, aliyetaka kufahamu kiasi cha fedha ambacho Serikali imewalipa ama kukataa kuwalipa wazabuni na wakandarasi wa ndani baada ya kuwasilisha madai yao na kufanyiwa uhakiki.
 
“Jumla ya madeni ya wazabuni na wakandarasi yaliyowasilishwa kwa uhakiki yalikuwa zaidi ya sh. bilioni 3,110.33kati ya kiasi hicho madeni yaliyolipwa ni zaidi ya sh. bilioni 2,128.54 ambapo sh. bilioni 1,032.13 ni madeni ya wazabuni na sh. bilioni 1,096.41 ni madeni ya wakandarasi” alisema Dkt. Nchemba
 
Alisema kuwa madeni ya sh. bilioni 981.79 yalikataliwa kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo kukosekana kwa nyaraka, madeni kubainika kulipwa tayari, pamoja na makosa ya ukokotoaji. 
 
Mhe. Dkt. Nchemba aliongeza kuwa Serikali kwa kutambua umuhimu na mchango wa Sekta Binafsi katika maendeleo na uchumi wa Taifa, imeendelea kutenga na kulipa madeni ya wazabuni na wakandarasi yaliyohakikiwa na kukubaliwa.
 
Alifafanua kuwa Serikali imeongeza bajeti ya kulipa madeni kutoka wastani wa shilingi bilioni 400 hadi shilingi bilioni 700 kwa mwaka na kuahidi kuwa  madai ya wazabuni na wakandarasi yataendelea kulipwa kadri watakavyowasilisha hati zao za kukamilisha kazi (certificates).

Posted by MROKI On Tuesday, January 30, 2024 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo