Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na
Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis amewataka wananchi kutunza vyanzo vya maji
ili viwanufaishe na kuhifadhi mazingira.
Amesema hayo wakati akizungumza na wananchi akiwa
kwenye ziara ya kikazi ya kukagua Mradi wa Kuhifadhi Ardhi (SLM) katika Bonde
la Ziwa Nyasa wilayani ya Ludewa mkoani Mbeya.
Mhe. Khamis amesema shughuli mbalimbali za uzalishaji
mali zinazofanyika kupitia mradi huo zikiwemo ufugaji wa samaki ni matunda ya
uwepo wa vyanzo vya maji
Amesema Wilaya ya Ludewa na Mkoa wa
Njombe ni miongoni mwa maeneo yenye vyanzo vingi vya maji hivyo ametoa rai kwa
viongozi kuhakikisha vyanzo hivyo vinatunzwa.
“Ndugu zangu Mwenge wa Uhuru si umepita
huku kwenu?..Na mmeona ujumbe wake ulihimiza namna ya kutunza mazingira na kuhifadhi
vyanzo vya maji sasa leo hii yale mabwawa ya samaki yasingekuwepo kama
tusingekuwa na vyanzo vya maji, leo hii nimepita kule nimeona mnafanya kilimo
cha irrigation yanafanyika haya kwasababua tuna vyanzo maji, tuvitunze” amesisitiza.
Naibu Waziri Khamis amewataka wananchi
kuwa walinzi wa vyanzo vya maji vitunze ili wanufaike kinyume na hapo watakuwa
wanategemea tu mvua inyeshe ndipo wapate maji.
Sanjari na vyanzo vya maji, pia Mhe.
Khamis amewataka wananchi kuitunza miradi hiyo walioyonufaika nayo ikiwemo
kupanda miti kwa wingi ili iwanufaishe.
Amewatahadharisha wananchi kulinda amani
iliyopo kuepuka madhara yanatokana na migogoro mbalimbali inayoweza kujitokeza
endapo amani itachezewa.
Kwa
upande wake Diwani wa Kata ya Lugarawa Mhe. Erasto Mhagama akizungumzia
mradi wa ufugaji wa samaki unaotekelezwa kupitia SLM katika kata hiyo ameshukuru
Serikali kwa kuwapelekea mradi huo katika wilaya yao.
Ameiomba Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais
inayotekeleza mradio huo chini ya ufadhili wa Mfuko Mazingira wa Dunia (GEF)
kuongeza wigo wa utekelezaji wa mradi ili uwafikie wananchi wnegi zaidi.
Nae Bw. Longinus Mgani ambaye ni mwenyekiti wa Kikundi
cha INAWEZEKANA kinachojishughulisha na mradi wa ufugaji wa samaki amesema wameitumia
fursa ya mradi kujikwamua kimapato.
Amesema kuwa mradi huo umewapa hamasa ya kuacha
kufanya shughulli za kilimo cha kuhamahama kisicho endelevu na kukata miti ambazo
husababisha uharibifu wa mazingira.
Mradi wa Kuhifadhi Ardhi (SLM) katika Bonde la Ziwa
Nyasa unatekelezwa katika halmashauri za wilaya tano zikiwemo ya Kyela (Mbeya),
Makete na Ludewa (Njombe), Mbinga na Nyasa (Ruvuma).
Lengo la mradi, pamoja na kuhifadhi ardhi katika eneo
hilo lakini pia kuisaidia jamii kufanya shughuli za kujipatia kipato bila
kuathiri mazingira na kulinda hifadhi ya Bonde la Ziwa Nyasa.
0 comments:
Post a Comment