Mkutano huo utafuatiwa na Mkutano Ngazi ya Makatibu Wakuu
utakaofanyika tarehe 31 Agosti 2023 ambapo kwa pamoja mikutano hiyo inafanya
maandalizi ya Mkutano Ngazi ya Mawaziri utakaofanyika tarehe 1 Agosti
2023.
Ujumbe wa Tanzania katika mkutano ngazi Wataalam umeongozwa na
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi
Dkt. Samwel Shelukindo na kwa upande wa Algeria umeongozwa na Mkurugenzi Idara
ya Afrika, Wizara ya Mambo ya Nje ya Algeria, Balozi Selma Haddadi Malika.
Akifungua mkutano huo Balozi Shelukindo ameeleza kuwa ushirikiano
uliopo kati ya Tanzania na Algeria ni wa kihistoria na uliojengwa katika
misingi imara na waasisi wa mataifa hayo mawili, Hayati Mwl. Julius Kambarage
Nyerere wa Tanzania na Hayati Ahmed Ben Bella.
Pia amesema Tanzania imejikita katika mageuzi ya kisekta hususan
katika sekta za kilimo, utalii na taasisi za fedha ili kuiwezesha sekta binafsi
kukuza uchumi wa Taifa. Pia inaendelea na ujenzi wa miundombinu ili kurahisisha
mawasiliano kupitia usafiri wa barabara, reli, maji na anga.
‘’Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais,
Dkt. Samia Suluhu Hassan imeweka msisitizo wa kuimarisha sekta za uzalishaji na
kuweka mpango wa usimamizi katika masuala ya biashara, uwekezaji na uchumi wa
viwanda,’’ Alisema Balozi Shelukindo.
Naye Mwenyekiti Mwenza, Balozi Selma Malika katika hotuba yake
ameeleza kuwa mkutano huu wa tano unaonesha utayari wa pande zote mbili katika
kukuza ushirikiano wenye tija kwa maslahi ya watu wake.
‘’Serikali ya Algeria itaendelea kuhuisha na kuimarisha
ushirikiano na Serikali ya Tanzania katika masuala ya diplomasia, biashara,
mafunzo ya kujenga uwezo na tafiti, ufadhili katika elimu ya juu na kuongeza
maeneo mapya ya ushirikiano kila inapohitajika ili kujenga uchumi imara wa
mataifa yetu,’’ alisema Balozi Selma Malika.
Aidha, kupitia mkutano huu Balozi Shelukindo amewasilisha salamu
za pole kwa Serikali ya Algeria kufuatia tukio la janga la moto lililotokea
katika mikoa ya Bejaia, Jijel, Bouira, Media, Skikda na Tiziozou
ulilosababishwa na kuongezeka kwa joto kali.
Tanzania na Algeria zinashirikiana katika sekta za Biashara,
viwanda, kilimo, miundombinu, nishati, madini, utalii, sanaa na utamaduni,
elimu, sayansi na teknolojia, ulinzi na usalama, siasa na diplomasia,
mawasiliano, uvuvi, uwekezaji na maendeleo ya jamii.
0 comments:
Post a Comment