Nafasi Ya Matangazo

July 31, 2023

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa akitoa maelekezo kwa Meneja wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) Mkoa wa Kigoma, Mhandisi Narcis Choma baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Barabara ya Chankere hadi Mwamgongo inayojengwa kwa kiwango cha zege, Mkoani Kigoma.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa akisisitiza jambo kwa Viongozi wa Wilaya ya Buhingwe, Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) na Mkandarasi wa Kampuni ya ZCCC mara baada kukagua barabara ya Kasulu-Buhigwe- Manyovu yenye urefu wa kilomita 56, Mkoani Kigoma.
Muonekano wa hatua iliyofikiwa ya mradi wa barabara ya Kasulu-Buhigwe- Manyovu yenye urefu wa kilomita 56 inayojengwa kwa kiwango cha lami, Mkoani Kigoma.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa akimsikiliza Mkandarasi wa kampuni ya Synohydro Corporation Limited inayojenga barabara ya Kanyani Junction hadi Mvungwe yenye urefu wa Kilomita 70.5, wakati Waziri huyo alipokagua barabara hiyo, Mkoani Kigoma.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa akitoa maelekezo kwa Wakandarasi Kampuni ya Synohydro Corporation Limited mara baada ya kukaugau mradi wa ujenzi wa barabara ya Kanyani Junction hadi Mvungwe yenye urefu wa Kilomita 70.5inayojengwa na kampuni hiyo, Mkoani Kigoma.
Muonekano wa hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa Daraja la Mto Maragarasi ambalo ni sehemu ya mradi wa Barabara ya Kabingo-Kasulu hadi Manyovu yenye urefu wa Kilomita 260.6 inayojengwa kwa Kiwango cha Lami mkoani Kigoma.
*****************
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa amemtaka Meneja wa Wakala Barabara Nchini (TANROADS) Mkoa wa Kigoma kuhakikisha barabara ya Kasulu-Buhigwe- Manyovu yenye urefu wa kilomita 56 Sehemu ya Kasulu hadi Buhigwe KM 35 inakamilika kwa kiwango cha lami ifikapo oktoba mwaka huu.
 
Barabara hiyo ambayo ni sehemu ya Barabara ya Kabingo-Kasulu hadi Manyovu yenye urefu wa Kilomita 260. 6 inatarajiwa kuufungua na kuunganisha mkoa wa Kigoma na Kagera kwa barabara ya lami na hivyo kuchochea shughuli za kilimo, biashara na uwezekezaji katika ukanda wa magharibi mwa Tanzania.
 
“Hakikisheni TANROADS Kigoma na TANROADS Makao Makuu mnakagua miraid hii mara kwa mara ili kufahamu changamoto za wakandarasi na kuzipatia ufumbuzi wa haraka kabla ya msimu wa mvua kuanza’ amesema Prof. Mbarawa.
 
Prof. Mbarawa ameelezea kuridhishwa kwake na kasi ya ujenzi wa barabara hiyo katika sehemu ya Kasulu hadi Manyovu yenye urefu wa Kilomita 56 na Mvugwe hadi Nduta Junction yenye urefu wa kilomita 59.35 na Nduta Junction-Kibondo Junction hadi Kabingo yenye urefu wa kilomita 62.5 ambayo kasi ya ujenzi wake inaridhisha na kumuonya Mkandarasi anayejenga sehemu ya Kanyani Junction hadi Mvungwe yenye urefu wa Kilomita 70.5 ambaye bado yuko nyuma ya muda.
 
“Serikali imedhamiria kuufungua mkoa wa Kigoma kwa barabara zake zote ili kuimarisha shughuli za biashara, kilimo na usalama hivyo haitamvumilia Mkandarasi anayefanya kazi nje ya mkataba kwa kuwa lengo la Serikali ni kuwahakikishia wananchi wake wanapata huduma bora kwa wakati ‘amesisitiza Waziri Prof. Mbarawa.
 
Prof. Mbarawa amewataka wakazi wa Kigoma na wa mwambao wa Ziwa Tanganyika kutumia uwekezaji wa miundombinu kuibua fursa za biashara na maendeleo ili kupunguza umasikini.
 
Katika hatua nyingine Prof. Mbarawa amekagua barabara ya Chankere hadi Mwamgongo katika Jimbo la Kigoma Kaskazini ambayo inapita kwenye mlima mkali na maeneo yenye uzalishaji wa mazao ya biashara na kuwataka wakazi wa maeneo hayo kuzingaia alama za barabarani na kujenga nje ya hifadhi ya barabara ili kuepuka usumbufu na kulinda usalama.
 
“TANROADS hakikisheni ujenzi huu unaofanywa hauathiri wananchi pindi utakapokamilika na barabara kuanza kutumia’ amesema Prof. Mbarawa.
 
Kwa upande wake Meneja TANROADS Kigoma, Mhandisi Narcis Choma amesema wamejipanga kuhakikisha wakandarasi wote wanne wanaojenga barabara ya Kabingo-Kasulu hadi Manyovu KM 260.6 wanasimamiwa kikamilifu na hakutaongezwa muda kwa mkandarasi atakayezembea na kushindwa kumaliza kazi kwa wakati.
 
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kasulu Kanali Isaac Mwakisu ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa namna inavyosimamia ujenzi wa barabara mkoani Kigoma na kuahidi ushirikiano mkubwa kwa wakandarasi ili watimize majukumu yao kwa wakati na ubora unaotakiwa.
 
Prof. Mbarawa yuko katika ziara ya siku tatu Mkoani Kigoma ya kukagua miundombinu ya barabara, reli, viwanja vya ndege na Bandari.
 
(Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi)
Posted by MROKI On Monday, July 31, 2023 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo