Nafasi Ya Matangazo

August 06, 2016

TUKIO la kupatwa kwa jua kipete ambalo linataraji kutokea mwezi Septemba mwaka huu nchini hasa Mkoani Mbeya katika Wilaya ya Mbarali Kata ya Rujewa ni tukio la kisayansi ambalo kama nchi italitumia vyema ni fursa pekee ya kuweza kukuza uchumi kupitia sekta ya utalii. Mwandishi Mroki Mroki "Father Kidevu" anaadika zaidi juu ya tukio hilo na mahusiano yake katika utalii. 
Mtaalam wa Astronomia (Astronomy) kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) Dk. Noorali Jiwaji wa  Kitivo cha Sayansi, Teknologia na Elimu ya Mazingira, akionesha kifaa maalum cha kutazamia jua linapo patwa. Kulia ni Kaimu Mkuu wa chuo hicho kikuu Huria, Profesa Elifas Tozo Bisanda.
***********
KUPATWA  kwa jua kunatokea wakati mwezi unafunika jua.

Matokeo yake ni kupungua kwa jua hadi kutoonekana tena na kufika kwa giza wakati wa mchana. Muda wa kufunikwa kabisa ni dakika chache tu.

Kupatwa kwa jua kunatokea kama dunia, mwezi na jua vyote kwa pamoja vitakaa kwenye mstari mmoja mnyoofu yaani wakati mwezi unapita kati ya dunia na jua.

Katika hali hiyo kuna kivuli cha mwezi kwenye uso wa dunia. Kivuli hiki hakifuniki dunia yote. Kwa hiyo kupatwa kwa jua kunaonekana kwa watu wengi kama kupungua kwa mwanga wa jua.

Kisayansi kuna aina mbalimbali za kupatwa kwa jua. Miongoni mwa aina hizo ni kupatwa kwa jua kabisa;  hii jua ninapotea kabisa kwa dakika chache. Hali hii huonekana kwenye kanda nyembamba duniani kinapopita kitovu cha kivuli.

Aina nyingine ya kupatwa kwa jua ni kupatwa kipete; hapa mwezi huonekana mdogo kuliko jua. Hivyo duara la kung'aa kwa jua huonekana kubwa kuliko duara la mwezi na mwanga wa jua waonekana kama pete.

Pia aina nyingine ni kupatwa kwa jua kisehemu; hapa ni kuwa eneo kubwa la kivuli cha kando watu huona upungufu wa mwanga. Kiasi chake hutegemea umbali na kitovu cha kivuli. Ukitazama jua kwa filta kwa mfano kioo kilichopakwa dohani katika moshi wa mshumaa huwa wanaona sehemu ya duara ya jua imefunikwa.


Miongoni mwa aina hizo tatu za kupatwa kwa jua, huenda msomaji ulisha wahi kuona aina hizi kutegemea na umri wako. Laiki kwa kizazi cha sasa sina hakika sana kama wamewahi kuona aina hizo za kuaptwa na jua.

Mwezi Septemba mwaka huu kunatarajiwa kutokea tukiko kubwa la angani la kipekee la kupatwa kwa jua usawa wa Tanzania ambalo litatokea Septemba 1, mwaka huu, kuanzia saa 4:17 asubuhi hadi Saa 7:56 adhuhuri.

Washabiki na wanataaluma wa anga kutoka duniani kote pamoja na wanasansi, wanafunzi pamoja na jamii ya watanzania wataelekea Wilayani Mbarali katika Kata ya Rujewa, mkoani Mbeya kushuhudia duara la jua linavyobadilika kuwa pete ya jua.

Ugeni huo mbali na kuwa wanakuja katika tukio la kisayansi lakini pia, ni fursa pekee katika sekta ya utalii kwani wageni wengi watakao kuja nchini wanahitaji kushawishwa kuweza kutembelea vivutio mbalimbali vilivyopo nchini hasa vile vya mikoa ya Morogoro, Iringa na Mbeya. BOFYA HAPA KUSOMA ZAIDI MAKALA HAYA
Nchini kote Tanzania mamilioni ya watu watashangaa kuona jua kali la utosi likimegwa kwa zaidi ya asilimia 90 kwa kufunikwa na mwezi katika kupatwa kwa jua, lionekane kama hilali nyembamba au kama mwezi mwandamo.

Katika tukio hili la kupatwa kwa jua, watu wanaoishi ndani ya ukanda wenye upana wa kilomita 100 unaokatisha Kusini ya Tanzania kutoka Congo kuelekea Katavi, mbeya, Ruvuma hadi Masasi na kuingia Msumbuji, siku hiyo jua kama duara jembamba kama pete kwa vile asilimia 98 ya jua litakuwa limejificha nyuma ya mwezi.

Tayari wa taalam wa elimu ya mambo ya anga ya Astronomia (Astronomy) kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), wameaza mkakati wa jinsi Chuo hicho kinavyoweza kwenda na wakati hasa katika mambo ya kisayansi na kutoa elimu kwa wananchi juu ya tukio hilo kubwa la kihistoria litakalo tokea nchini.

Kaimu Mkuu wa Chuo hicho cha OUT, Profesa Elifas Tozo Bisanda amesema kuwa watatoa mafunzo hayo ya Sayansi katika kitivo chao cha Sayansi ili kusaidia jamii  kwenda na teknolojia ikiwa ni pamoja na kutoa elimu hususani mashuleni ili jamiii itambue juu ya tukio hilo la jua kupatwa kipete, kwa kutumia wataalam wa Chuo hicho.

Aidha watanzania wametakiwa kujiandaa kufuatilia tukio hilo sambamba na kutengeneza fursa za kujiongezea fursa za kiuchumi kutokana na ugeni mkubwa wa ndani na nje ya nchi utakaoshuhudia tukio hilo.

Inaelezwa kuwa, kwa mara ya mwisho kutokea kwa tukio la kupatwa kwa jua lilionekana nchini Aprili 18, 1977 na kwamba litatokea tena Mei 21, 2031.

Mhadhiri wa Fizikia, Kitivo cha Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Mazingira kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Dk Noorali Jiwaji alisema tukio hilo litawafundisha wanafunzi kwa vitendo sayansi ya astonomia na kuelewa namna jua na mwezi vinavyopangika angani.

Dkt. Jiwaji anasema, tayari wanaendelea na taratibu zote ikiwemo suala la kutoa elimu katika eneo hilo la  Rujewa Mkoani Mbeya hususani kwa wananchi kuwa na tahadhari kuangalia jua hilo ikiwemo kutakiwa kutumia kitazama jua ambacho ni kifaa maalum  kitakachokuwa kinachuja nguvu ya jua ambacho pia kinaondoa mionzi haribifu kwa asilimia 99.999.

“Kupatwa huko kwa jua kunaweza kuonekana kwa usalama na watazamaji, lakini inabidi kutumia vichuja maalum vya mwanga wa jua,” alieleza Dk Jiwaji.

Tukio la kupatwa ni la kusisimua na la nadra sana kutokea katika maisha ya mtu. Hasa kwa kizazi hiki kipya ambacho kimechangamka kitasisimuliwa sana na tukio la ajabu kama hili na watajifunza Sayansi ili kuelewa kwa nini kinatokea kile wanachokiona.

Dk Jiwaji anaeleza kuwa tukio hilo linaweza kutumiwa na shule na taasisi za elimu kuendeleza Sayansi na kuvuta wanafunzi kujiendeleza kisayansi na hasa kuelewa mizunguko mbalimbali iliyopo katika mfumo wetu wa sayansi pamoja na anga za juu kwa ujumla. Kuongeza uelewa wa sayansi ni muhimu katika kuelewa maumbile ya ulimwengu wetu.

Kupatwa huku kutatokea siku ya Alhamisi ambapo wanafunzi wengi watakuwa mashuleni na ni wakati wa masomo.

Kwavile mchakato wote utaendelea kwa Saa nne  hivi , kati ya Saa 4 asubuhi hadi Saa 8 mchana wanafunzi wataweza kushirikiana  kuangalia na kusimulia na kujadili tukio ili kulielewa vizuri na kuandika ripoti madarasani kwao.

Tukio jingine kubwa la kupatwa kwa jua kama hili halitatokea jingine kwa miaka 15 ijayo, kwa hiyo tunahitaji kutumia fursa hili kwa ukamilifu.

Mtaalaam huyo kutoka OUT, Dk Jiwaji anasema ili kuangalia kupatwa huko, kila mmoja atahitaji kutumia kikinga macho kinachochuja mwanga wa jua kiitwacho kitazamia jua.  Nihatari sana kuangalia jua kwa macho ya moja kwa moja au hata kutumia vichujio vingine vya kiza vilivyotengenezwa kibinafsi.

Kitazamia jua maalum ni kifaa rahisi kilichotengenezwa kutokana na kichuja nguvu ya jua ambacho kinaondoa mionzi haribifu kwa asilimia 99.999. Miwani hiyo maalum ya jua inaweza kutengenezwa Tanzania kwa gharama isiyozidi 500/= kila moja, ikiwemo kuchapa fremu za kadbodi na kichuja nguvu ya jua (polymer filter) kinachoagizwa kutoka Marekani.

Aidha, alisema kuna madhara makubwa endapo wananchi hawatahamasishwa kutoangalia jua kwa kutumia njia za asili ikiwemo chupa na X-ray au negative za mikanda ya picha badala yake watumie kichuja mwanga maalumu kilichotengenezwa kitaalam.
 Utalii kutokana na kupatwa kwa jua kipete
Kupatwa kwa Jua kipete pia kuna weza kutumika kama sehemu ya kuongeza mapato ya ndani kwa njia ya utalii. Kwani wapo watu wengi kutoka nje ya nchi katika mataifa mbalimbali duniani hasa wanasayansi watakao kuja nchini kwa lengo la kujionea tukio hilo.

Huu ni utalii wa anga. Hivyo wananchi wa Rujewa na Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya hawana budi kuandaa mazingira ya kupokea ugeni huo kwa kuwaandalia mazingira mazuri na ujuo huo ni wazi kuwa utaongeza pato la taifa na wananchi wa Rujewa pia endapo watachangamkia fursa hiyo ya ugeni.

Ni vyema sasa vyombo husika ikiwepo serikali kuanza kampeni ya kuhamasisha jamii za ndani na nje ya nchi kuweza kufika katika eneo hilo Septemba mosi mwaka huu kujionea tukio hilo la kihistoria.

Wizara ya Maliasili na Utalii, pia inaweza kutumia fursa hiyo kwa kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo katika mikoa ya Kanda ya Nyanda za juu kuzini kama vile, Hifadhi ya Taifa Kitulo, Hifadhi ya Ruaha na hata Hifadhi ya taifa Mikumi.

Tanapa itumie fursa hiyo pia kuhamasisha watalii kuja nchini na kwenda mkoani Mbeya kujionea kupatwa huko kwa jua kipete pamoja na kutembelea vivutio vilivyopo katika ukanda huo.

Kufanya hivyo kutaifaidisha nchi kiuchumi kwa kupata watalii kutoka nchi za nje ambao watakuja kushuhudia tukio hilo na kuiingizia nchi fedha za kigeni.


Kampuni za utalii zinatakiwa zitumie fursa kwa kutangaza kwa njia mbalimbali huduma zao na namna ya kuweza kufiskisha wageni Rujewa kuangalia jua likipatwa kipete pamoja na fursa ya kutembelea hifadhi kama Kitulo. 
Posted by MROKI On Saturday, August 06, 2016 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo