HIFADHI ya Jamii ni mfumo ambao jamii husika
ujiwekea kiasi cha fedha kwa lengo la kujikinga dhidi ya majanga
yasiyotarajiwa, majanga hayo ni kama maradhi, ulemavu, kupoteza kazi, kuacha
kazi kwa sababu ya uzee (kustaafu).
Kumekuwa na malalamiko ya mara kwa mara kutoka kwa
watumishi mbalimbali nchini kuanzia mashirika ya umma, binafsi na sekta
nyingine juu ya waajiri kuto peleka makato ya watumishi wao katika mifuko ya
hifadhi za jamii kwa wakati, pamoja na kuwa watumishi hao wamekatwa kwenye
mishahara yao.
Hili hufanywa na waajiri ambao si waaminifu ambao
ni watekelezaji wa mikataba wanayoingia baina ya mfanyakazi, mwajiri na mfuko
husika wa hifadhi ya Jamii ambayo hupokea makato hayo na kumtunzia mfanyakazi
hadi atakapo staafu, kupata dharula au vinginevyo.
Tanzania bara kuna Mifuko ya pension ya lazima
mitano ambayo ni Mfuko wa kustaafu wa GEPF, Mfuko wa Pensheni wa LAPF, Mfuko wa
Taifa wa Hifadhi ya Jamii wa NSSF, Mfuko wa Pensheni wa PPF na Mfuko wa
Pensheni wa PSPF.
Mfanyakazi hashurutishwi kujiunga na mfuko wowote
kati ya hiyo bali anapaswa kuchagua mwenyewe na hii ni kwa mujibu wa kifungu
cha 30 cha Sheria ya Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya
Jamii (SSRA), kila mwajiriwa mpya ana
haki ya kuchagua Mfuko ni mfuko upi ajiunge nao tena ni kosa la kisheria kwa mwajiri
au mtu yoyote kumchagulia mwanachama mpya mfuko wa kujiunga nao.
Lakini waajiri hawa wamekuwa hawapeleki makato ya
watumishi wao katika mifuko hiyo na pindi ikitokea mtumishi ameacha kazi,
kupata ajali, ugonjwa au kustaafu kwa uzee na akaenda katika mfuko husika
kufutailia mafao yake huishia kuambiwa kuwa mwajiri alikuwa hapeleki makato
yake.
Mstaafu huyu huanza tena kazi ya kusaga soli kufuatilia
mafao yake na mwisho wa siku wengi hupoteza maisha bila hiyo haki yao
kupatikana.
Jana SSRA imetoa agizo kwa mifuko hii ya hifadhi
za jamii kuhakikisha inawalipa wafanyakazi mafao yao hata kama waajiri
hawajapeleka makato. BOFYA HAPA KUSOMA ZAIDI
SSRA imefanya hivyo baada ya Mamlaka hiyo kupokea
malalamiko mengi kuhusu ucheleweshwaji wa mafao kwa Wanachama jambo ambalo ni
kinyume cha Sheriaya Mamlaka Na. 8 ya mwaka 2008 iliyorekebishwa na Sheria Na.
5 ya Mwaka 2012 pamoja na Sheria zote za Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.
Mamlaka imewataarifu wanachama wa Mifuko ya
Hifadhi ya Jamii kwamba kwa mujibu wa Kifungu cha 35 cha Sheria ya Mamlaka,
kulipwa mafao ni haki ya Mwanachama pale anapokidhi vigezo vilivyowekwa kwa
mujibu wa Sheria.
Pia ana haki ya kulipwa mafao yake kwa wakati. Hivyo,
Mamlaka imekemea vikali tabia iliyozuka ya kuchelewesha mafao kwa Wanachama kwa
kisingizio cha kutopokea michango toka kwa Waajiri.
Mifuko mingi imesahau kabisa kwamba ni jukumu la Mfuko husika kwa mujibu wa
Sheria kukusanya michango kutoka kwa Waajiri. Jukumu hili si la mwanachama.
Hivyo nadhani wakati umefika sasa wa maofisa wa mifuko hii kuwazungukia waajiri
ambao waliingia makubaliano na kuhakikisha makato ya watumishi yanawafikia.
Aidha, Mamlaka inatabanaisha kuwa Sheria zote za
Mifuko zimeainisha wajibu wa kila Mfuko kulipa mafao kwa wakati. Vile vile
Mfuko unapochelewesha mafao kwa Mwanachama aliyekidhi vigezo unapaswa
kumlipa Mwanachama Tozo kwa kiwango cha
asilimia 15 kwa kila kiasi cha Mafao kilichocheleweshwa.
Mamlaka imeitaka mifuko hii ya hifadhi za jamii kulipa
mafao kwa wanachama wote waliokidhi vigezo kwa wakati na kuwalipa wanachama
wote ambao mafao yao yamecheleweshwa kwasababu yoyote ile. Malipo haya
yafanyike ndani ya kipindi cha siku 21 kuanzia tarehe ya taarifa hii.
Bilashaka sasa utakuwa ni wakati muafaka kwa
mifuko kuwabana vilivyo waajiri ambao hawawasilishi michango ya watumishi wake
kwa wakati ili wafanye hivyo.
Ni vyema sasa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii
kuwachulia hatua za kisheria waajiri ambao wanalimbikiza na wakati mwingine
hawapeleki kabisa makato ya watumishi wao na fedha hizo kufanyia vitu vingine,
kwani michango hiyo inakatwa kwenye mishahara yao kwa wakati.
0 comments:
Post a Comment