Katika siku za hivi
karibuni kumekuwa na taarifa za kuwepo kwa Programu (Application) ya simu
ikijulikana kama SOFTBOX TANZANIA
iliyosemekana iko kwenye Google PLAYSTORE.
Ilidaiwa kuwa program (Application)
hiyo ya SOFTBOX TANZANIA
ilikuwa na uwezo wa kunasa au kuingilia mazungumzo ya simu, ujumbe mfupi pamoja
na mawasiliano ya WhatsApp kutoka kwenye simu ya mtu binafsi.
Kwa yeyote aliyekuwa na nia
hiyo ya kunasa au kuingilia mazungumzo ya simu, ujumbe mfupi pamoja na
mawasiliano ya WhatsApp kutoka kwenye simu ya mtu mwingine alihitajika kulipia
fedha kiasi cha Tshs 35,000/= kupitia mitandao ya simu ili kupata namba ya siri
kwa ajili ya kuwezesha nia hiyo.
Mamlaka ya Mawasiliano
imefanya uchunguzi kubaini kuwepo kwa programu hiyo na ukweli kuhusu uwezo wake
wa kufanya kilichodaiwa, ikiwa ni pamoja na kuangalia madhara ya program hiyo
na sheria inasema nini kuhusu suala hili. Baada ya kufanya uchunguzi wa kina,
Mamlaka ya Mawasiliano ilibaini na imejiridhisha kuwa program (Application)
hiyo haina uwezo huo wa kunasa au kuingilia mazungumzo ya simu, ujumbe
mfupi pamoja na mawasiliano ya WhatsApp kutoka kwenye simu ya mtu binafsi kama
ilivyodaiwa.
Aidha Mamlaka imebaini kuwa
watengenezaji (Developers) wa programu hiyo walikuwa na nia ya kutapeli na
kujipatia fedha hiyo kiasi cha Tshs 35,000/= kwa njia ya udanganyifu wakitumia
kivutio cha kunasa au kuingilia mazungumzo ya simu, ujumbe mfupi pamoja na
mawasiliano ya WhatsApp kutoka kwenye simu za watu binafsi.
Programu (Application)
nyingine ya aina hiyo iliibuka tena ikiitwa SIMNET Tanzania ikiwa na maelezo kama ya awali.
Wakati Mamlaka ya Mawasiliano
Tanzania pamoja na Jeshi la Polisi wakiendelea na uchunguzi zaidi, tunapenda
kuuarifu umma wa Watanzania kuepuka
kufanya mambo yafuatayo:
- Kuvutiwa na matendo yaliyo kinyume na sheria na maadili ya matumizi mazuri ya mawasiliano kama hili la kunasa au kuingilia mazungumzo ya simu, ujumbe mfupi pamoja na mawasiliano ya WhatsApp kutoka kwenye simu ya mtu binafsi. Kitendo hiki ni kosa la jinai kwa mujibu wa kifungu cha 6 na 10 cha Sheria ya Makosa ya Mtandao ya Mwaka 2015 na kifungu cha 123 cha Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (EPOCA) ya Mwaka 2010. Sheria katika vifungu hivyo inakataza mtu yeyote kuingilia mawasiliano ya mtu mwingine. Adhabu kali ya makosa haya ni faini isiyopungua shilingi milioni tano au kutumikia kifungo kwa kipindi kisichopungua mwaka mmoja au vyote kwa pamoja.
- Mamlaka inawatahadharisha watumiaji wa huduma za mawasiliano kutokuwa wepesi na kudanganyika kufanya malipo yoyote kwa njia ya mitandao kwa huduma wasiyokuwa na uhakika nayo au bila kujiridhisha na uwepo wa huduma hiyo. Ni vizuri kutoa taarifa kwa mtoa huduma wako au kuwasiliana na Mamlaka ya Mawasiliano kupitia barua pepe malalamiko@tcra.go.tz au kupiga simu namba 0784558270/1.
Imetolewa na:
Mkurugenzi Mkuu
Mamlaka ya
Mawasiliano Tanzania
04/12/2015
0 comments:
Post a Comment