Jaji mkuu wa mahakama ya katiba nchini Misri ameapishwa kama rais wa
muda baada ya jeshi kumng'oa madarakani Rais Mohammed Mursi huku
kiongozi mkuu wa udugu wa kiislamu akikamatwa baada ya agizo la
mwendesha mashitaka.
Rais wa muda wa Misri Adly Mansour
Adly Mansour ameapishwa leo katika mahakama ya katiba katika sherehe
zilizoonyeshwa moja kwa moja kupitia televisheni ya kitaifa na kulingana
na mamlaka za kijeshi, atahudumu kama kiongozi wa muda wa Misri hadi
rais mpya atakapochaguliwa.
Katika hotuba yake ya kwanza Mansour
ameyasifu maandamano
yaliyosababisha kung'olewa madarakani kwa Mursi na kuwasifu vijana
walioshiriki katika maandamano hayo yaliyoanza tarehe 30 mwezi uliopita.
Mansour amechukua mahala pa Mursi aliyeng'olewa madarakani hapo jana na
jeshi baada ya mwaka mmoja uliogubikwa na misukosuko chungu nzima
madarakani. Kwa sasa Mursi yuko chini ya kifungo cha nyumbani mahali
kusikojulikana.
Viongozi wa kiislamu wasakwa
Mwendesha mashitaka nchini Misri leo alitoa agizo la kukamatwa kwa
kiongozi wa chama cha Udugu wa Kiislamu, Mohammed Badie, na makamu wake,
Khairat el Shater, na kupanua msako dhidi ya vuguvugu hilo, Hata hivyo
katika hotuba yake ya kwanza, Mansour ametoa fursa kwa viongozi hao wa
kiislamu kushirikishwa katika kile alichokiita ujenzi wa taifa na
kuongeza kuwa hakuna atakayeachwa nje ya juhudi za kuijenga Misri iwapo
watakubali wito huo.
Hali ya utulivu imerejea mjini Cairo leo baada ya umati mkubwa wa
waandamanaji kukita kambi kwa siku tano hadi hapo jana na kusherehekea
usiku kucha baada ya tangazo la jeshi la kupinduliwa kwa serikali ya
Mursi.
Umoja wa Mataifa, Marekani na nchi nyingine zenye nguvu duniani
hazikulaani kuondoelwa kwa Mursi kama mapinduzi ya kijeshi. Rais wa
Marekani, Barack Obama, ambaye nchi yake inatoa msaada wa dola bilioni
1.3 kila mwaka kwa jeshi la Misri, ameelezea wasiwasi wake kwa
kuondolewa kwa Mursi na kutaka kurejea haraka iwezekanvyo kwa serikali
ya kidemokrasia iliyochaguliwa na wananchi.
Waandamanaji washerehekea baada ya kung'olewa madarakani kwa Mursi nchini Misri
Umoja wa Ulaya pia umetaka mchakato wa kidemokrasia kutekelezwa haraka
iwezekanavyo. Mkuu wa sera za kigeni wa umoja huo, Catherine Ashton,
amesema hilo lina maana kuwa kufanywe chaguzi za urais na bunge
zitakazokuwa huru na haki na kuidhinishwa kwa katiba.
Nchi mbali mbali zazungumzia mapinduzi Misri
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle, amesema hatua ya
jeshi ni kurejesha nyuma hatua zilizopigwa za kidemokrasia na kutaka
kuwe na majadiliano.
Chama cha rais wa Tunisia, Moncef Marzouki, kimelaani mapinduzi hayo ya
kijeshi na kusema ni pigo kwa demokrasia na kwamba ni jaribio la
kurejesha utawala wa zamani.
Maafisa wa idara ya mahakama nchini Misri leo wameanzisha uchunguzi
dhidi Mursi na viongozi wengine 15 wa kiislamu kwa madai kuwa
waliidunisha mahakama. Jaji Tharwat Hammad ametangaza marufuku ya
kusafiri kwa wote hao. Hili ni agizo la pili la kumzuia Mursi kusafiri
tangu jana.
Mwandishi: Caro Robi/afp/reuters/apMhariri: Josephat Charo
0 comments:
Post a Comment