By Mtuwa Salira,EANA
Matokeo ya kwanza ya utafiti juu ya Jumuiya ya Afrika
Mashariki (EAC) umeonyesha kwamba jumuiya hiyo iliundwa kama chombo
kilichoandaliwa kuwepo kwa maslahi ya serikali na wafanyabiashara wakubwa.
Jumuiya
hiyo yenye wananchama watano ingawa ilianzishwa upya kuwa ‘’jumuiya yenye
misingi ya watu’’ wenyewe wa Afrika Mashariki, imebainika ushiriki wa raia wa
kawaida katika mchakato wa mtagamano huo ni mdogo mno. Wanachama wa EAC ni
pamoja na Kenya, Uganda, Tanzania, Rwanda na Burundi.
Taarifa
iliyotolewa na Jukwaa la Wataalam la Afrika Mashariki (VEAF),lililofanya
utafiti huo imebaini pamoja na mambo mengine kwamba mpaka sasa mwenendo wa
ushirikiano huo ni kutoka juu kwa watawala kwenda chini huku raia wengi wakawaida
wakiwa hawana taarifa juu yake, Shirika Huru la Habari la Afrika Mashariki
linaripoti.
‘’Theluthi
moja ya watu kama wa Tanzania na Kenya hawajahi kusikia juu ya mtangamano wa
EAC,’’ ilisema taarifa hiyo iliyotiwa saini na Mwenyekiti wa Bodi ya
Wakurugenzi ya VEAF, Dr Azaveli Lwaitama.
‘’Ni kwa
kuboresha uelewa wa raia juu ya mwenendno mzima wa ushirikiano kwa
kushughulikia hofu za wananchi wa pande zote za nchi husika, ndipo awamu hii ya
pili ya kihistoria ya kurejesha upya jumuiya hiyo inaweza kufanikiwa,’’ taarifa
ilisisitiza.
EAC
ilizinduliwa upya mwaka 1999 baada ya jumuiya ya kwanza kuvunjika mwaka 1977
kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo tofauti za kisiasa na kiuchumi miongoni
mwa wanachama watatu wa awali wa jumuiya hiyo, Kenya, Uganda na Tanzania.
Ripoti
kamili ya utafiti huo kwa mujibu wa taarifa hiyo itazinduliwa rasmi leo na Rais
wa zamani wa Tanzania Alli Hassan Mwingi katika hoteli ya Holiday Inn, jijini
Dar es Salaam ambapo pia Katibu Mkuu wa zamani wa EAC, Balozi Juma Mwapachu
atakuwa mmoja wa washiriki muhimu katika uzinduzi huo.
Sherehe
za uzinduzi na matokeo ya kwanza ya utafiti huo umefadhiliwa na Taasisi ya moja
ya Ujerumani ya Frieddrich-Ebert-Stifstung (FES) tawi la Tanzania.
0 comments:
Post a Comment