Na Ezekiel Kamwaga, Kwanza Sul, Angola
KOCHA
Mkuu wa Simba, Patrick Jean Elysee Liewig, amesema ana matumaini timu
yake itapata matokeo mazuri katika mchezo wa kesho baina ya Wekundu wa
Msimbazi na Libolo ya Angola.
Mechi
hiyo imepangwa kuchezwa leo kuanzia saa tisa alasiri katika Uwanja wa
Estadio Libolo, uliopo katika mji mdogo wa Calulo jimbo la Kwanza Sul.
Katika
mechi ya kwanza baina ya timu hizo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa
jijini Dar es Salaam wiki mbili zilizopita, Simba ilifungwa 1-0 na
mabingwa hao wa Angola.
Hata
hivyo, Liewig alisema ingawa matokeo ya kufungwa nyumbani hayakuwa
mazuri, ana imani Simba nayo inaweza kufanya vizuri ugenini.
“Kama
wao walitufunga kwetu kwanini sisi tusiwafunge kwao. Ukiangalia kwenye
ile mechi ya kwanza wao walipata nafsi moja tu ya maana na wakaitumia.
Sisi tulipata nafasi kama tatu hivi na hatukutumia vizuri hata moja,”
alisema.
Liewig
alisema ameridhishwa na ari na mazoezi mazuri ambayo Simba imefanya kwa
wiki nzima kujiandaa na mechi hiyo na kwamba kuna dalili kuwa timu yake
inaweza kufanya lisilotarajiwa.
Akizungumza
na wachezaji katika kikao kilichofanyika katika Hoteli ya Anisaan Ritz
ambako Simba imefikia, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Simba, Zacharia
Hans Poppe, alitoa ahadi ya Sh milioni 10 iwapo watafanikiwa kuitoa
Libolo.
Aliwataka
wachezaji wa Simba kuwakumbuka mamilioni ya washabiki wao waliopo
Tanzania ambão hawalali wala kula vizuri wakati timu yao kipenzi
inapokuwa na matokeo mabaya.
Poppe
ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba na pia kundi la
Friends of Simba, alisema ana imani kubwa na wachezaji wa timu yake kwa
vile ndiyo bora Tanzania na kama wataamua kucheza kwa nguvu zao zote,
matokeo mazuri yanawezekana.
“Nyie
ni wachezaji wazuri sana. Kama nyote mtacheza kama timu na mkacheza kwa
uwezo wenu wote, ni wazi kwamba mnaweza kuibuka na ushindi,” alisema.
Akizungumzia
mechi hiyo, nahodha msaidizi wa Simba, Shomari Kapombe, alisema mechi
baina yao na Libolo itakuwa tofauti na ya kwanza kwa sababu ya kuwepo
kwa mshambuliaji Mzambia, Felix Sunzu.
“Tulimkosa
sana Sunzu kwenye mechi ya Dar es Salaam. Mipira ilikuwa haikai kule
mbele na hilo lilikuwa tatizo kubwa, kubwa sana na hiyo ni kwa sababu
Sunzu hakuwepo. Nadhani sasa tuna nafasi zaidi kuliko mara ya kwanza,”
alisema.
0 comments:
Post a Comment