Na Mwandishi Wetu
Msondo Ngoma na Mlimani Park Orchestra
“Sikinde” leo mchana zitachuana vikali katika ukumbi wa Equator Grill, Temeke.
Mpambano huo wa kusherekea sikukuu ya
Krismasi litakuwa la kufunga mwaka 2012 na pia litaamua ni bendi gani bora kati
ya magwiji hao wa muziki wa dansi nchini mwaka huu.
Mratibu wa mchuano huo Joseph Kapinga
amesema pambano hilo litanzaza saa tisa alasiri hadi majogoo.
Bendi hizo zitapiga katika jukuwaa moja
lakini kila moja itatumia vyombo vyake vipya walivyopewa na Konyagi hivi
karibuni ili kuondoa malalamiko ya hujuma.
Kapinga alisema kila bendi itapiga kwa
muda wa saa moja kabla ya kuipisha bendi nyingine.
Kiongozi wa Msondo Ngoma Saidi Mabera
alisema jana kuwa watapiga nyimbo zao zote kali ili kuhakikisha wanaibuka
kidedea.
Alitaja baadhi ya nyimbo ambazo
watazipiga kuwa ni 'Nimuokoe Nani', 'Zarina', 'Mwanaidi', 'Kanjelenjele',
'Bahati', 'Sesilia', 'Usiue Usiibe', 'Asha Mwana Seif', 'Kauka Nikuvae', Chuma
Chikoli Moto', 'Kilio cha Mzima', 'Ajali' na 'Suluhu'.
Baadhi ya wanamuziki wanaounda Msondo
Ngoma ni Shaaban Dede, Mabera, Abdul Ridhiwani Pangamawe, Saad Ally 'Mashine',
Eddo Sanga, Huruka Uvuruge, Zahoro Bangwe, Ibrahim Kandaya, Ismail Mapanga,
James Mawilla, Muhidini Gurumo, Eddo Sanga, Juma Katundu, Hamisi Mnyupe, Roma
Mng’ande `Romario’ na Hassan Moshi.
Naye kiongozi wa Sikinde Hamisi Mirambo
alijigamba kuwa wataibuka na ushindi mnono.
“Tuna waimbaji wazuri na vyombo vipya na
hakuna kitakachotuzuia kushinda,” alisema Mirambo.
Alitaja baadhi ya nyimbo ambazo
watazipiga kuwa ni 'Selina', Wiki endi', 'Penzi la Fukara', 'Hiba', 'MV
Mapenzi’, 'Supu Umelitia Nazi' na 'Jinamizi la Talaka'.
Sikinde inaundwa na wanamuziki kama
Hassan Rehani Bitchuka, Hassan Kunyata, Kaingilila Maufi, Tonny Karama, Shaaban
Mabuyu, Habib Abassi, Juma Choka, Ally Jamwaka, Athumani Kambi, Mbaraka Othman,
Hamisi Milambo, Shaaban Lendi, Joseph Benard, Ramadhani Mapesa na Habibu Jeff.
Pambano umeandaliwa na Bob Entertainment
na Keen Arts chini ya udhamini wa Konyagi.
0 comments:
Post a Comment