Nafasi Ya Matangazo

May 10, 2025

 Papa Leo xiv



Posted by MROKI On Saturday, May 10, 2025 No comments

May 09, 2025

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiagana na Mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Msumbiji Mhe. Daniel Francisco Chapo mara baada ya kuhitimisha Ziara yake ya Kiserikali, Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 09 Mei, 2025. 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Jamhuri ya Msumbiji, Mhe. Daniel Francisco Chapo wamekubaliana kuendeleza ushirikiano wa kiuchumi baina ya Tanzania na Msumbiji hususan katika eneo la biashara na uwekezaji kwa kuanzisha Tume ya Pamoja ya Uchumi (JEC) ili kutatua changamoto za kiuchumi.

Makubaliano hayo yamefikiwa leo katika majadiliano ya mazungumzo rasmi baina ya Marais hao wawili yaliyofanyika, Ikulu jijini Dar es Salaam.

Aidha, Rais Dkt. Samia na Rais Chapo wamekubaliana kuendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji kati ya nchi hizo mbili, ikiwemo kuwawezesha wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo na wa kati kufanya biashara kwa urahisi (Simplified Trade Regimes - STRs). 

Kwa kutambua kuwa asilimia kubwa ya uchumi wa Msumbiji na Tanzania unategemea kilimo, nchi hizo mbili zimekubaliana kuimarisha ushirikiano kwenye sekta hiyo, ikiwemo kubadilishana
uzoefu na kufanya tafiti za pamoja, hususan kwenye zao la korosho ili kufaidika na bei ya soko la dunia na kuanzisha Umoja wa nchi zinazozalisha korosho na kuuza korosho zilizochakatwa.

Mbali na kuimarisha ushirikiano kwenye sekta ya gesi ambayo Msumbiji amepiga hatua kubwa katika sekta hiyo, Rais Dkt. Samia na Rais Chapo wamekubaliana kushirikiana katika fursa zinazotokana na uchumi wa buluu, zikiwemo uvuvi, utalii, madini na usafirishaji, kufanya kazi kwa karibu na kubadilishana uzoefu kwenye masuala ya uvuvi wa bahari kuu.

Vile vile, wamekubaliana kuimarisha ushirikiano katika sekta ya ulinzi na usalama hasa katika kukabiliana na uhalifu unaovuka mipaka.

Kwa upande mwingime, Rais Dkt. Samia amempongeza Rais Chapo kwa jitihada alizozifanya ndani ya muda mfupi, hususan katika kujenga umoja wa kitaifa na kurejesha amani na utulivu nchini Msumbiji.

Mara baada ya mazungumzo hayo, Rais Dkt. Samia na Mgeni wake Rais Chapo walishuhudia utiaji wa saini wa Mikataba miwili ya Uanzishwaji wa Kituo cha Huduma cha Pamoja Mpakani (OSBP) kwenye mpaka wa Mtambaswala na Negomano, ili kurahisisha ufanyaji biashara pamoja na Mkataba wa Kubadilishana Wafungwa.

Vilevile walishuhudia utiaji saini wa Hati nne za Makubaliano (MOU) ya Ushirikiano katika Sekta ya Elimu, Sekta ya Utamaduni, Udhibiti wa Madawa, pamoja na ushirikiano katika Redio ya Taifa ya Msumbiji na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) Wakizungumza na vyombo vya habari, Rais Chapo amesema ipo haja ya kuzidisha mahusiano katika uchumi na biashara kwa kuimarisha miundombinu ya usafiri na usafirishaji, hivyo ameeleza umuhimu wa kuendelea na ujenzi wa barabara zinazounganisha Msumbiji na Tanzania.

Rais Chapo pia amesema ni muhimu kufanya mapitio ya Mkataba wa Ushirikiano wa Usafiri Anga kwa Mashirika ya ndege ya Msumbiji na Tanzania ili kutoa huduma kwenye miji mikubwa pamoja na kuimarisha usafiri wa baharini.

Rais Chapo alieleza umuhimu wa nchi hizo mbili kuimarisha vikao vya ujirani mwema katika mikoa ya mpakani ya Ruvuma na Mtwara kwa upande wa Tanzania na Nyasa na Cabo Delgado kwa upande wa Msumbiji.

Katika hatua nyingine, Msumbiji imejitoa rasmi kuwa mbia wa Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim (CFR) kwa kuwa wameanzisha Chuo chao wenyewe na hivyo nchi hizo mbili zitaendelea kubadilishana uzoefu kupitia vyuo hivyo.

Wakati huo huo, Rais Dkt. Samia ameridhia mualiko wa Rais Chapo wa kuhudhuria sherehe za Maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa Msumbiji yatakayofanyika tarehe 25 Juni, 2025.

Rais Chapo anatarajia kuhitimisha ziara yake nchini hapo kesho ambapo ataagwa rasmi na Rais Dkt. Samia katika Ikulu ya jijini Dar es Salaam.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa amesimama na Mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Msumbiji, Mhe. Daniel Francisco Chapo wakati wimbo wa Taifa wa Tanzania na ule wa Msumbiji ukiimbwa katika viwanja vya Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 09 Mei, 2025.



Posted by MROKI On Friday, May 09, 2025 No comments

Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Lindi, imewatoa hofu watumiaji wa barabara kuu ya kutokea Lindi kwenda Dar es Salaam eneo la Somanga - Mtama kuwa linapitika vizuri na halijakatika kutokana na mvua zinazoendelea mkoani hapo.

Meneja wa TANROADS Lindi, Mhandisi Emil Zengo ametoa kauli hiyo leo tarehe 09 Mei, 2025, katika eneo hilo ambalo linaendelea na ujenzi wa daraja lenye urefu wa mita 60.

Mha. Zengo amesema eneo hilo la barabara ni njia ya mchepuko ambayo inatumika sasa na magari kupita wakati ujenzi ukiendelea wa daraja kwenye barabara ya kawaida.

“Pamoja na mvua kubwa kuendelea kunyesha mkandarasi yupo site anaendelea na ujenzi na haya maji yanayoonekana kwenye video iliyosambazwa na watu sio kwamba yamekatiza barabara kwa kuzidiwa kwa daraja la hasha hii imetengenezwa mahususi kitaalam kwa kuwekwa mawe makubwa pamoja na zege na pia eneo hili limesanifiwa kwa kuruhusu maji yapite juu ya barabara yanapokuwa mengi na muda huo tunashirikiana na askari wa usalama barabarani tunazuia magari kwa muda na maji yakishapungua magari yanaendelea na safari,” amesema Mha. Zengo.

Mha. Zengo amesema ujenzi wa daraja hili utahusisha nguzo 43 na hadi sasa wameshakamilisha ujenzi wa nguzo za chini 34 zilizopo mita 12 kwenda chini, na baadaye zitajengwa nguzo kubwa tatu ambazo ndizo zitakazoonekana juu.

Hatahivyo, ameshauri wananchi kufuatilia taarifa sahihi katika mitandao ya kijamii ya TANROADS na sio kuzusha hofu kwa watumiaji wa barabara hiyo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Lindi, SP James Makumu amesema wanahakikisha usalama wa watu na mali zao kwa kufanya doria ya mara kwa mara eneo hilo, kutokana na mvua kubwa kuendelea kunyesha.

“Sisi tumejipanga kila wakati kunakuwa na askari anayeruhusu magari hapa kila maji yanapokuwa mengi tunayazuia na baada ya kupungua tunayaruhusu ili kuondoa changamoto za foleni, na tunahakikisha hakuna kabisa msongamano,” amesema SP. Makumu.

Hivi karibuni TANROADS Mkoa wa Lindi ilitangaza kusitisha matumizi ya barabara ya Somanga Mtama kwa muda baada ya mvua kubwa zilizonyesha katika Wilaya ya Kilwa mkoani Lindi, kuleta mafuriko makubwa yaliyoharibu eneo la barabara iliyo kwenye njia ya mchepuko (diversion) ya ujenzi wa daraja la Somanga Mtama.
Posted by MROKI On Friday, May 09, 2025 No comments

Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga amezindua Kituo Mama cha Gesi Asilia iliyoshindiliwa (CNG) ambacho kina uwezo wa kujaza Gesi Asilia kwenye magari 1200 kwa siku huku kikifanya kazi kwa muda wa saa 24. 

Kapinga amezindua kituo hicho tarehe 9 Mei, 2025 jijini Dar es Salaam akimwakilisha Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ambapo uzinduzi huo ulienda sambamba na uzinduzi wa basi la mfano la Kampuni ya Mabasi Yaendayo Haraka (UDART) ambalo litaendeshwa kwa kutumia nishati ya Gesi Asilia.

Akizungumza na halaiki iliyohudhuria hafla hiyo, Kapinga amemshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maono, mtazamo na maelekezo yake kwa Wizara ya Nishati ambayo yanaleta matokeo chanya kielelezo mojawapo kikiwa ni uzinduzi kwa kituo hicho cha CNG.

Pia, amemshukuru Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko kwa uongozi wake ambao unapelekea upatikanaji wa nishati ya uhakika ambayo ni rafiki kwa mazingira na afya za wananchi.

“ Hapo nyuma kumekuwa na malalamiko ya uwepo wa foleni kubwa za ujazaji wa gesi kwenye vyombo vya moto katika vituo vya CNG ikiwemo kituo cha Ubungo Maziwa, lakini uwepo wa kituo hiki  unaonyesha jinsi Serikali inavyotekeleza kwa vitendo ahadi inazotoa kwa wananchi za kupunguza kero ya upatikanaji wa CNG, nampongeza Rais Samia kwa kuendelea kutatua changamoto za wananchi na pia naipongeza Bodi na Menejimenti ya TPDC kwa hatua hii.” Amesema Kapinga

Ameeleza kuwa, kituo hicho kitakuwa na uwezo wa kujaza Gesi kwenye magari nane kwa wakati mmoja, kuchochea ongezeko la vituo vingine vya CNG na kuwapatia huduma ya gesi watumiaji wengine kama viwanda, shule, hoteli n.k

Kapinga ameiagiza TPDC kuhakikisha kuwa, kituo hicho kinakuwa mfano wa kutoa huduma bora na za viwango kwa wateja huku kikizingatia masuala ya usalama na utunzaji wa mazingira.

Pia ameiagiza TPDC kuendelea kujenga vituo vya CNG katika maeneo mengine ya nchi ikiwemo Lindi na Mtwara, pia kutoa ushirikiano kwa sekta binafsi ili kuendelea kuchochea uwekezaji kwenye sekta ya CNG. 
Naibu Waziri Kapinga pia ameishukuru Sekta binafsi kwa kuendelea kuiunga mkono Serikali kwenye ujenzi wa vituo vya CNG.

Aidha, amewaasa Watanzania kuchangamkia fursa ya kuweka mifumo ya matumizi ya gesi kwenye magari yao kwani mifumo hiyo haiharibu magari hayo na pia watapata nafuu ya gharama za uendeshaji. 

Kuhusu kampuni ya UDART ambayo kwa mara ya kwanza imezindua basi jipya linalotumia Gesi Asilia, ikiwa ni moja ya mabasi mengi yakayotumia gesi hiyo,  Kapinga amesema kuwa ushirikiano kati ya TPDC na UDART utaendelea kuchochea uwekezaji kwenye CNG na kuendelea kuboresha huduma za usafiri jijini Dar es Salaam.

Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, ameipongeza wizara ya Nishati kwa kazi kubwa inayofanyika ili kupata matokeo makubwa kwenye sekta na kuahidi ulinzi katika miundombinu hiyo ambayo ni muhimu katika kutoa huduma kwa wananchi.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe.Kilumbe Ng’enda amesema Bunge limeridhishwa na hatua zinazochukuliwa kwa kasi na Serikali katika kuendeleza Sekta ya Gesi akieleza kuwa unapotumia gesi asilia kuendesha gari unapata unafuu kwa asilimia 40 ukilinganisha na mafuta. 

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Dkt. James Mataragio ameipongeza Bodi na Menejimenti ya TPDC kwa kutekeleza mradi huo kwa mafanikio, pia ameipongeza UDART ambao watakuwa wateja wakubwa wa CNG.

Amesema mradi huo ni wa kujivunia kwani kituo hicho kilichozinduliwa ni cha Pili kwa ukubwa barani Afrika na cha kwanza kwa ukubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki

Mwenyekiti Bodi TPDC, Mhe. Balozi Ombeni Sefue amesema Bodi na Menejimenti ya Taasisi hiyo itahakikisha changamoto ya  wananchi kupanga foleni ndefu kwenye vituo vya CNG inaisha na watahakikisha rasilimali ya gesi asilia inapatikana wakati wote kupitia huduma mbalimbali ikiwemo ya kupikia na kuendeshea vyombo vya moto.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Francis Mwakapalila amesema kuwa katika kuchochea matumizi ya Gesi Asilia kwenye vyombo vya moto nchini, TPDC imeamua kuweka mkazo kwa kuwekeza katika ujenzi wa vituo vya kujazia gesi  asilia kwenye vyombo vya moto ikiwemo magari na bajaji kwenye maeneo mbalimbali nchini na kwa sasa tayari wameanza mchakato wa manunuzi ya vituo vitano vya CNG vinavyohamishika ambavyo vitawejwa kwenye mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro na Dodoma.

Awali Mkurugenzi wa Idara ya Biashara ya Mafuta kutoka TPDC, Mhandisi Emmanuel Gilbert alisema kuwa kituo hicho kina uwezo wa kuzalisha CNG kiasi cha futi za ujazo milioni 4.2 sawa na kilo 120 kwa siku, kina pampu nne zenye jumla ya nozeli nane na hivyo kukifanya kituo kuwa na uwezo wa kuhudumia magari nane kwa wakati mmoja ambapo  kwa siku  kitatoa huduma kwa magari takriban 1200.

Ameongeza kuwa, kituo kina pampu maalum tatu kwa ajili ya kujaza magari maalum ya kusafirisha CNG kwenda  kwenye vituo vidogo vya kujaza gesi kwenye magari (Offline CNG Filling Stations), viwandani, taasisi na majumbani.













Posted by MROKI On Friday, May 09, 2025 No comments

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa leo Mei 09, 2025 ameongoza Kikao cha Kamati ya Kitaifa ya Mazishi ya aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais na Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Hayati Cleopa David Msuya kilichofanyika katika Ofisi ya ndogo za Waziri Mkuu, Magogoni Jijini Dar es Salaam.




Posted by MROKI On Friday, May 09, 2025 No comments



Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa Serikali  imeendelea kuboresha, kuimarisha, kurahisisha na kuwezesha upatikanaji wa umeme na nishati safi ya kupikia kwa gharama nafuu ili kupunguza athari za kiafya, mabadiliko ya tabia nchi  na kuboresha maisha ya wananchi.

Dkt. Biteko amesema hayo leo Mei 9, 2025 ofisini kwake jijini Dar es salaam wakati alipotembelewa na Balozi wa Japan nchini Tanzania, Mhe. Youichi Mikami.

“ Serikali imedhamiria kuwezesha matumizi ya nishati safi ya kupikia kutoka asilimia 21 hadi asilimia 75  ifikapo mwaka 2030 tumewashirikisha sekta binafsi ili kufikia azma hii,” amesema Dkt. Biteko.

Ameongeza kuwa Serikali imeandaa Mpango mahsusi wa Taifa wa Nishati kwa kipindi cha miaka mitano (National Energy Compact 2025 - 2030). Mpango ambao umeandaliwa kwa ushirikiano wa sekta binafsi na wameahidi kuchangia fedha mfano Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo ya Afrika.

Dkt. Biteko amesema fedha hizo zitasaidia kufikia malengo ya Mpango huo wenye lengo la kuhakikisha watu milioni 300 waliopo kwenye Ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara wanapata huduma ya umeme ifikapo mwaka 2030.

Katika mazungumzo yake na Balozi wa Japan, Mhe. Mikami Dkt. Biteko ameishukuru Serikali ya Japan kwa ushirikiano wake katika utekelezaji wa miradi ya umeme nchini.

“Tunawashukuru kwa ushirikiano wenu na kwa kufadhili mradi wa uunganishaji umeme kutoka Singida hadi nchini Kenya ambao tayari umekamilika. Tunapenda pia kushirikiana nanyi katika miradi ya gesi. Nchi zetu zimekuwa na ushirikiano mzuri na nia ya dhati ya kuhudumia wananchi wake” amesema Dkt. Biteko.

Kwa upande wake, Balozi wa Japan nchini Tanzania, Mhe. Youichi Mikami amesema kuwa nchi yake na Tanzania zimekuwa na uhusiano wa muda mrefu na kuwa Japan itaendelea kuimarisha uhusiano huo.

Pia, ameipongeza Tanzania kwa kuwa mwenyeji wa mkutano wa wakuu wa nchi na Serikali (Mission 300) uliofanyika hivi karibuni ambao ulilenga kujadili kuhusu usambazaji wa nishati ya umeme barani Afrika.
Posted by MROKI On Friday, May 09, 2025 No comments

May 08, 2025







Waziri wa uchukuzi Profesa Makame Mbarawa, amewasihi Watanzania kushirikiana na Shirika la Reli Tanzania (TRC), kuilinda na kuitunza miundombinu ya treni ya kisasa ya Umeme (SGR).

Prof. Mbarawa, ametoa wito huo katika stesheni ya Magufuli Dar es Salaaam, muda mchache baada ya kumsindikiza Rais wa Msumbiji Fransisco Chapo, aliyesafiri kwa SGR kutoka Stesheni ya Magufuli kwenda stesheni ya Pugu na kisha kurejea stesheni ya Magufuli, kwa lengo kushuhudia mradi huo ambao ni wa kielelezo barani Afrika.

Waziri wa Uchukuzi amesema Rais Chapo, aliyeko nchini kwa ziara ya kiserikali ya siku tatu aliyoaianza Mei 07, 2028 ameeleza kufurahishwa na mradi huo aliosema ni wa kiwango cha dunia na kuwataka Watanzania, kuulinda kwa wivu.

Katika hatua nyingine Mkurugenzi Mkuu wa TRC Bw. Masanja Kadogosa,  alisema kuwa ujio wa Mhe. Chapo ni ishara tosha ya kwamba Afrika inajua nini kinachoendelea Tanzania na pia kuzidi kudumisha mahusiano baina ya nchi za Afrika na kuimarisha katika ufanyaji biashara kwa ukaribu.

“Kikubwa zaidi katika nchi za Afrika ni kufanya biashara na wenzetu wa nchi nyingine wanatutazama tofauti, na nchi ya Msumbiji tumekua tukishiriana katika Nyanja mbalimbali ikiwemo siasa, ulinzi na vilevile kijamii ukizungumza mmakonde wa Msumbiji na Tanzania hawana tofauti” alisema Ndugu Kadogosa.
Posted by MROKI On Thursday, May 08, 2025 No comments
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, akiwaongoza Wajumbe wa Sekreterieti ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, kusimama kimya kwa dakika moja, kwa ajili ya heshima ya Hayati Mzee David Cleopa Msuya, Makamu wa Kwanza wa Rais na Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye pia aliwahi kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu na Mbunge wa CCM. Sekreterieti hiyo chini ya uenyekiti wa Balozi Nchimbi, imekutana katika kikao maalum kilichofanyika Ofisi ya Makao Makuu ya CCM, jijini Dodoma, leo Alhamis tarehe 8 Mei 2025.

Posted by MROKI On Thursday, May 08, 2025 No comments
Na Mwandishi wetu, Dodoma
Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Dkt. Janet Reuben Lekashingo, amehitimu shahada ya uzamivu (Doctorate in Business Administration) kutoka Georgia State University – Robinson College of Business nchini Marekani. Aliporejea nchini, Dkt. Lekashingo alipokelewa kwa shangwe na pongezi kutoka kwa menejimenti na watumishi wa Tume ya Madini katika ofisi za Makao Makuu, Dodoma.

Akizungumza mara baada ya kupokelewa, Dkt. JR Lekashingo alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuweka mazingira wezeshi kwa wanawake kushiriki katika usimamizi wa Sekta ya Madini, jambo lililomhamasisha kujiendeleza kielimu. 

Alisema kuwa uongozi wa Rais Samia umeweka mazingira rafiki yanayohamasisha maendeleo binafsi na ya kitaaluma, jambo lililompa motisha wa kutimiza ndoto yake ya kielimu.

Aidha, Dkt. JR Lekashingo aliwapongeza viongozi wengine kwa msaada na motisha waliompa, wakiwemo Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko, aliyekuwa Waziri wa Madini wakati alipoanza masomo yake ya uzamivu, Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba, Naibu Katibu Mkuu, Msafiri Mbibo, na Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo.

“Nawashukuru sana viongozi na watumishi wa Tume ya Madini kwa kuniunga mkono na kunitia moyo wakati wa safari yangu ya kielimu. Ushirikiano wenu umenipa nguvu ya kufikia ndoto yangu bila kuathiri majukumu yangu ya kikazi,” alisisitiza Dkt. Lekashingo.

Dkt. JR Lekashingo pia aliwapongeza Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa na watumishi wote wa Tume ya Madini kwa jitihada zao za kuboresha ukusanyaji wa maduhuli, hali iliyosaidia kuchangia kwa asilimia 10.1 kwenye Pato la Taifa, hatua inayoakisi maendeleo endelevu ya sekta hiyo.

Aliendelea kusema kuwa, atahakikisha anatumia ujuzi mpya katika usimamizi wa Sekta ya Madini sambamba na kuwa mfano bora kwa watumishi anaowasimamia ndoto yake ikiwa ni Sekta ya Madini kuendelea kuwa na mchango mkubwa kwenye uchumi wa nchi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Usimamizi wa Rasilimaliwatu na Utawala wa Tume ya Madini, Nsajigwa Kabigi, akizungumza kwa niaba ya Katibu Mtendaji, alimpongeza Dkt. JR Lekashingo kwa hatua kubwa ya kuhitimu masomo yake na kuongeza kuwa uongozi wa Tume ya Madini na watumishi wote, wataendelea kumpa ushirikiano kwa ajili ya mafanikio zaidi ya Sekta ya Madini nchini.

Watumishi wa Tume ya Madini kwa nyakati tofauti walimpongeza Dkt. JR Lekashingo kwa mafanikio hayo, wakiongeza kuwa hatua yake imeleta hamasa kwa wengine kujiendeleza kitaaluma ili kuimarisha zaidi usimamizi wa sekta hii muhimu kwa uchumi wa Taifa.













Posted by MROKI On Thursday, May 08, 2025 No comments
  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo