Kikosi kamili cha Mtibwa Suger ya Mjini Turiani ambacho kimewacharaza Mabingwa wa Kagame 2012, Yanga SC ya Jijini Dar es Salaam magoli 3-0 katika uwanja wa Jamhuri Mjini Morogoro.
Kikosi kamili cha Yanga ambacho kimekubali kubebeshwa tani 3-0 za Sukari na Mtibwa Suger hii leo.
Na Father Kidevu Blog na Bongostaz Blog, Morogoro
TIMU ya Yanga SC yenye maskani yake Mtaa wa Jangwani jijini Dar es Salaam leo wameshindwa kupenya katika Mashamba ya Miwa ya Mtibwa Suger FC ya Turiani mjini Morogoro baada ya kuambulia kichapo cha aibu cha magoli 3-0 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom.
Wakati Yanga ikiambulia kichapo hicho Mabingwa watetezi Simba SC ya Mtaa wa Msimbazi na mahasimu wakubwa wa Yanga leo wamefanikiwa kuipindisha mitutu ya Askari wa Jeshi la Kujenga Taifa kutoka Ruvu mkoani Pwani (JKT Ruvu) kwa magopli 2-0, mchezo uliochezwa uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam.
Yanga iliyochini ya udhamini mnono wa Kilimanjaro Lager na inayonolewa na Kocha Mbelgiji Tom Saintfiet, ilishindwa kufurukuta kwa wakata miwa hao wa Manungu Turiani wanao nolewa na Kocha Mzalendo na mchezaji wa zamani wa kikosi hicho na kile cha Taifa Stars Meck Mexime.
Yanga ambayo imevuma sana katika magazeti kuwa imefanya usajili wa uhakika kwa kuimarisha safu yake ya Ulinzi ilianza kushushiwa Mvua ya magoli katika dakika ya 11 kipindi cha kwanza.
Goli hilo la kwanza la wana Tam Tam Mtibwa Sukari lilipachikwa kimiani na na beki wa kati, Dickson Daudi akiunganisha kwa kichwa kona ya beki wa kushoto Malika Ndeule.
Niuzembe wa wazi wa mabeki wa Yanga ndio uliosababisha goli hilo baada ya kushindwa kumuweka ulinzi mchezaji mrefu kuliko wote, Daudi.
Yanga walijaribu kutaka kusawazisha, lakini mipango yao ilikuwa hafifu na kujikuta wakiendelea kushambuliwa na dakika ya 43, Hussein Javu aliwainua tena vitini mashabiki wa Simba waliokuwa wakiwashangilia kwa nguvu leo kwa kufunga bao la pili.
Kwa ujumla kipindi cha kwanza, Yanga walicheza ovyo- pasi zao nyingi zilikuwa hazifiki, walishindwa kuwabana wapinzani wao na zaidi Haruna Niyonzima alishindwa kuiongoza vema timu, jambo ambalo lilifamnya kiungo mkabaji Athumani Iddi ‘Chuji’ kupanda mbele zaidi kusaidia, ingawa haikusaidia.
Mabeki wawili wa kati wa Mtibwa, Daudi na Salvatory Ntebe waliwadhibiti vema washambuliaji wawili wa Yanga, Hamisi Kiiza na Saidi Bahamnuzi katika dakika 45 za kipindi cha kwanza.
Kipindi cha pili, Kocha wa Yanga, Mbelgiji Tom Saintfiet alianza kwa mabadiliko akiwatoa Frank Damayo na David Luhende na kuwaingiza Simon Msuva na Stefano na Mwasyika, lakini bado ukuta wa Mtibwa ulikuwa mgumu mbele ya Watoto wa Jangwani.
Katika kuongeza mashambulizi, Mtakatifu Tom alimtoa beki Mbuyu Twite na kumuingiza na mshambuliaji Didier Kavumbangu, lakini bado mambo yaliendelea kuwa magumu kwa Yanga.
Dakika ya 86 Hussein Javu aliifungia Mtibwa bao la tatu kwa shuti la mbali, wakitoka kushambuliwa na kufikia hapo, Yanga ‘walikufa’ na mashabiki wao wakaanza kuuacha Uwanja wa Jamhuri.
Huu unakuwa mchezo wa pili kwa Yanga tangu kuanza kwa ligi wakiwasononesha mashabiki wao, baada ya mechi ya kwanza kulazimishwa sare ya bila kufungana na Prisons kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.
Waswahili wanasema siku ya kufa nyani, miti yote huteleza, Hamisi Kiiza alipaisha mkwaju wa penalti dakika ya 89, baada ya Daudi kuunawa mpira kwenye eneo la hatari.
Yanga SC; Ally Mustafa ‘Barthez’, Juma Abdul, , Mbuyu Twite/Kavumbangu, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Athumani Iddi ‘Chuji’, Frank Domayo/Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Said Bahanuzi, Hamisi Kiiza na David Luhende/Stefano Mwasyika.
Mtibwa Sugar; Shaaban Hassan Kado, Malika Ndeule, Issa R Issa, Dickson Daudi, Salvatory Ntebe, Shaaban Nditi, Jamal Mnyate/Babu Seif Ally, Awadh Juma, Hussein Javu, Shaaban Kisiga ‘Malone’ na Vincent Barnabas/Ally Mohamed 'Gaucho'.
Matokeo ya Mechi nyingine za ligi hii leo ni, Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza Azam imelazimishwa sare ya 2-2 na wenyeji Toto African, Uwanja wa Kaitaba Bukoba, wenyeji Kagera Sugar wametoka sare ya bila kufunga na JKT Oljoro ya Arusha, wakati Uwanja wa Sokoine Mbeya, wenyeji Prisons wametoka sare ya 1-1 na Coastal Union ya Tanga na kwenye Uwanja wa Chamazi, African Lyon imeifunga Polisi Morogoro 1-0, wakati Uwanja wa Mabatini, Mlandizi, Ruvu Shooting imeifunga 2-1 Mgambo
Ulaya mchezaji akitolewa kwa mkopo hawezi cheza dhidi ya timu iliyomuazima ambayo ndiyo inayolipa mshahara.Kwa case ya Kado sijui imekaaje hii
ReplyDelete