Nafasi Ya Matangazo

June 06, 2012

Katibu Mkuu Ikulu, Peter Ilomo (Katikati) akimkabidhi bendera ya Taifa Mtanzania mpanda milima Respicius Baitwa (kushoto) anayetarajiwa kuondoka nchini Juni 23 mwaka huu kuelekea Amerika Kaskazini kupanda mlima McKinley wenye urefu wa ft 20,320. Baitwa ana ndoto za kupanda vilele vya milima saba duniani ambapo huu utakuwa mlima wa tano kwake na ndoto yake anatarajia kuitimiza Machi mwakani kwa kupanda mlima Everest.Anayeshuhudia kulia ni Mkurugenzi wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) Aloyce Nzuki.
xxxxxxxxxx
SERIKALI imesema itaendelea kuwaunga mkono wadau wa Sekta ya Utalii katika kutekeleza kwa vitendo mpango wake wa kuhakikisha sekta hiyo inaimarika na kuchangia ipasavyo katika pato la taifa.

Katibu Mkuu Ikulu, Peter Ilomo aliyasema hayo jana Dar es Salaama katika hafla fupi ya kumkabidhi bendera mtanzania Respicius Baitwa ambaye baadaye mwezi huu anatarajiwa kupanda mlima McKinley (Denali) uliopo Amerika Kaskazini.

Mtanzania huyo mwenye ndoto za kupanda vilele vya milima mirefu saba duniani tayari amepanda milima minne tofauti duniani na kwamba mwakani anatarajia kukamilisha ndoto yake kwa kupanda mlima wa saba.

Milima ambayo tayari ameipanda kwa ufadhili wa kampuni ya Highest Peaks Mountaineering Sports (HPMS) ya nchini ni pamoja na Kilimanjaro (ft 19,340) mwaka 1998,Elbrus (ft 18,510) uliopo Ulaya mwaka 2008,Aconcagua (ft 22,840) uliopo Afrika ya Kusini mwaka 2009 na Kosciusko (ft 7,310) uliopo Australia mwaka 2011.

Katika hotuba yake, Ilomo alisema serikali ina dhamira ya dhati katika kuhakikisha sekta zinazochangia katika pato la taifa zinaimarika hivyo wadau wote watakaoonyesha nia ya kuunga mkono jitihada hizo serikali itawapa nguvu kuhakikisha malengo yanafikiwa.

“Serikali imekuwa na malengo na mikakati tofauti ya kuimarisha vyanzo vya pato la taifa kwa maana hiyo tutafanya kila tunachoweza kuhakikisha tunafanikiwa na wale wote watakaonyesha nia ya kuiunga mkono serikali nasi tutawapa nguvu,” alisema.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) Aloyce Nzuki ambaye alimkabidhi bendera mtanzania huyo kwa niaba ya serikali alisema ndoto za Baitwa zitasaidia kwa kiasi kikubwa kuitangaza Tanzania ulimwenguni.

Alisema pamoja na kuhamasisha utalii wa ndani lakini pia upandaji milima unaofanywa na mtanzania huyo utasaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza idadi ya watalii nchini ambao kwa namna moja au nyingine wataifahamu Tanzania kupitia tukio hilo.

Alisema TTB kama mdau wa uhamasishaji wa utalii nchini itaendelea kuunga mkono jitihada zote zinazoonyeshwa na wadau mbalimbali ambapo alitoa rai kwa watu, kampuni na mashirika ya umma kuona umuhimu wa kuwekeza katika sekta hiyo.

“TTB inaendelea na kazi ya kuhamasisha utalii ndani na nje ya nchi ambapo pamoja na hilo pia tunawaunga mkono wale wote wanaonyesha nia au kuwekeza katika sekta hii hivyo tunatoa rai kwa watanznaia kuwekeza katika hili ili tusaidie kukuza pato la taifa,” alisema Nzuki

Akizungumzia maamuzi hayo Baitwa alisema kwa upande mmoja ni msukumo binafsi unolenga kumjenga yeye binafsi katika soko la ajira ya kutembeza watalii katika milma lakini pia maamuzi hayo yamejengwa na uzalendo alionao kwa nchi yake ambapo tukio hilo litakuwa na faida lukuki katika sekta ya utalii nchini.

Baitwa anatarajiwa kuondoka nchini Juni 23 mwaka huu kuelekea Marekani kwa ajili ya tukio hilo linalotarajiwa kumchukua siku 21 ambapo baada ya hapo mwezi Novemba mwaka huu anatarajiwa kupanda mlima Vinson Massif uliopo bara la Antarctika na atamalizia kwa kupanda mlima Everest ulipo nchini Nepali mwezi Machi mwakani.
Posted by MROKI On Wednesday, June 06, 2012 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo