Nafasi Ya Matangazo

June 05, 2012

Mbunge wa Jimbo la Bahi, Omary Badwel (CCM), akisindikizwa na askari polisi kutoka Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam leo, baada ya kusomewawa mashitaka akituhumiwa kushawishi na kupokea rushwa ya sh. milioni 1. Kesi hiyo imehairishwa hadi juni 18 mwaka huu.
MBUNGE wa Bahi (CCM), Omary Badwel amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa mashtaka mawili ya kuomba rushwa na kupokea rushwa.

Hatua hiyo imekuja baada ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kumtia mbaroni mbunge huyo kwa tuhuma za kutaka kuomba rushwa kutoka kwa mtumishi mmoja wa Serikali baada  ya kumuwekea mtego mwishoni mwa wiki.

Jana, mbunge huyo alifikishwa mahakamani hapo jana majira ya saa nne. Akiwa amevalia suti yenye rangi ya ugoro na viatu vyeusi, Badwel alipandishwa kizimbani saa 4:47 na kusomewa mashtaka hayo yanayomkabili mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Faisal Kahamba.

Akiwa amekaa kwenye kiti kidogo cheusi cha kuzunguka chenye matairi, Badwel alisomewa mashtaka hayo na Mwendesha Mashtaka  wa Takukuru, Janeth Machullya akisaidiana na Ben Lincolin.

Katika shtaka la kwanza, Machullya alidai kwamba  mshtakiwa huyo aliomba rushwa ya Sh8miloni kutoka kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga, Sipora Jonathan Liana.
Machullya alisema mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo kwa nyakati tofauti kati ya Mei 30 na Juni 2, mwaka huu katika maeneo tofauti ya Dar es Salaam.

Katika shtaka la pili, Machullya alidai kuwa mshtakiwa huyo alikamatwa Juni 2, mwaka huu katika Hoteli ya Peacock, Dar es Salaam akipokea rushwa ya Sh1milioni kutoka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Mkuranga.

Alidai kuwa mshtakiwa huyo akiwa ni Mbunge wa Bahi na  Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), aliomba kiasi hicho cha fedha ili kuwashawishi wajumbe wa kamati hiyo waweze kupitisha taarifa yake ya fedha ya mwaka 2011/2012.

Machullya alidai kuwa mshtakiwa huyo alitenda makosa yote hayo kinyume cha Kifungu cha 15(1) (a) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, namba 11 ya mwaka 2007.Alisema kwa Sheria ya Takukuru, Mbunge huyo ni mtumishi wa umma na  kitendo hicho ni kinyume cha kanuni zake za kazi.

Baada ya Machullya kumaliza kumsomea mashtaka hayo, Lincolin alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo namba 146 ya mwaka 2012 umekamilika.

“Hivyo, tunaomba tarehe nyingine ya kutajwa kwa ajili ya kupanga tarehe ya PH (usikilizwaji wa awali ambao mshtakiwa atasomewa maelezo ya awali ya kesi),” alidai Lincolin.

Kabla kupangwa tarehe ya kutajwa tena kesi hiyo, Wakili wa mshtakiwa huyo, Mpale Mpoki aliiomba mahakama impe dhamana mteja wake akidai kuwa makosa yanayomkabili yanadhaminika.Hakimu Kahamba alikubaliana na maombi ya Wakili Mpoki kuwa mashtaka yote yanayomkabili mshtakiwa yanadhaminika na kusema dhamana yake iko wazi.

Alimtaka mshtakiwa huyo kutimiza masharti ya kuwa na wadhamini wawili ambao watasaini mali yenye dhamana yenye thamani ya Sh4milioni, kila mmoja na kwamba wote watawasilisha mahakamani hati zao za kusafiria.
Mshtakiwa alipata wadhamini hao na Hakimu Kahamba aliahirisha kesi hiyo hadi Juni 18, mwaka huu.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Serikali za Mitaa (LAAC), Iddi Azzan amesema kila mbunge atavuna alichokipanda.

Katika hatua nyingine, CCM Wilaya ya Bahi, Dodoma kinasubiri uamuzi wa mahakama juu ya mbunge wao Badwel kabla ya kutoa tamko la nini cha kufanya yake.Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Bahi, Philimon Mdate alisema kuwa hadi jana walikuwa wakisubiri kama Badwel atapandishwa kizimbani.
Source:Mwananchi & Fullshangwe Blog.
Posted by MROKI On Tuesday, June 05, 2012 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo