Nafasi Ya Matangazo

April 18, 2024




SERIKALI Mkoa wa Njombe imetoa onyo kwa makampuni ya uchimbaji wa madini mkoani humo kuepuka mara moja tabia ya kuwaajiri watoto wadogo katika migodi yao.

Agizo hilo lilitolewa na Katibu Tawala Mkoa wa Njombe, Judica Omari wakati akifungua mafunzo kwa wadau na wachimbaji wa madini yaliyoandaliwa na Tume ya Madini mkoani humo.

“Tuangalie ajira tunazotoa ziwe nzuri zenye manufaa na zenye faida kwa wote, tusiende tukatumie ajira kwa watoto haitakiwi kuna baadhi ya taarifa kwenye migodi baadhi inatumia watoto wadogo,” alisema Omari.

Alifafanua kuwa, “Unawatoa shuleni kabla hawajamaliza unawalipa ujira mdogo sana lakini umemtoa mtoto kwenye huduma sasa ya kupata elimu wakati shule zipo kila mahali, vijiji vyote vina shule watoto wanatakiwa wakasome wamalize muda wao kwanza,” alisema.

Aidha Omari alitoa rai kwa wanawake mkoani humo kuchangamkia fursa mbalimbali ambazo zinapatikana kwenye migodi sambamba na kuingia ubia na makampuni ambayo yana vifaa vya kuchimbia.

Alisema kuwa  sekta ya madini katika pato la taifa inachangia asilimia tisa kutoka asilimia nne kwa kipindi cha miaka ya nyuma.

“Na tunategemea ipande zaidi kwa sababu upekee ulipo katika mkoa wa Njombe inaweza ikachangia kwa kiasi kikubwa sana hili pato la taifa liweze kuongezeka kwa kiwango cha juu,” alisema Omari.

Kwa upande wake, Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Njombe, Zabibu Napacho alisema katika mkoa wa Njombe yapo madini ya kimkakati kama dhahabu, makaa ya mawe na shaba.

“Pamoja na shughuli za madini lakini mkoa wa Njombe una takribani leseni 400 lakini leseni ambazo zinafanya kazi ni takribani leseni 40 tu kwa hiyo tunahitaji kuendelea kutoa elimu na kuhamasisha ili kila mmiliki ajue wajibu wake,” alisema Napacho.

Alisema kuwa katika mkoa huo pia kuna ongezeko la makusanyo kuanzia mwaka wa fedha 2017 ambao tume imeanza kazi hadi mwaka 2024.

“Katika migodi ya makaa ya mawe inafanya vizuri na mapato ya serikali hususan mrabaha pamoja na ada ya ukaguzi yanaendelea kuongezeka ukiangalia lengo la mwaka 2017 hadi mwaka 2018 makisio tulipewa kukusanya sh. milioni 450 na tuliweza kukusanya sh. milioni 434 lakini ukiangalia kwa mwaka 2022/23 tulipewa lengo la makusanyo sh. bilioni mbili ambapo tuliweza kukusanya sh. bilioni 2.17 sawa na asilimia 100.9,” alisema Napacho.

Alisema kwa mwaka wa fedha ulioanza julai lengo la makusanyo lilikuwa bilioni 3.85 ambapo hadi sasa wamekusanya kiasi cha shilingi bilioni 3.5 sawa na asilimia 91.

Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo akiwemo Mtafiti wa Madini na Mchimbaji  Michael Mng'ong'o aliiomba serikali kuachia sehemu ya Kigugwe iliyopo ndani ya hifadhi ya Mpanga Kipengere wilayani Wanging'ombe yenye madini ya Copper na kuwasaidia kupata leseni za biashara ili kufanya machimbo katika eneo hilo.
Posted by MROKI On Thursday, April 18, 2024 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo