Nafasi Ya Matangazo

January 21, 2010

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mheshimiwa Bernad Membe-MB (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Bodi mpya wa Wakurugenzi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC) Waliokaa kutoka kushoto ni Mkurugenzi Mwendeshaji wa AICC, Elishilia Kaaya, Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Balozi Christopher Liundi, Rose Lugembe na Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu. Waliosimama nyuma ni Shabani Mnubi, Nuru Milao, Joseph Chilambo, Wilfred Nyachia, Makumba Kimweri, Dkt Aggrey Mlimuka na Issa Suleiman. Waziri Membe alizindua Bodi hiyo Jumanne usiku katika ofisi za AICC Arusha.

Na Mwandishi wetu, Arusha
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mheshimiwa Bernard Membe, ametoa changamoto kwa Bodi Mpya ya Wakurugenzi ya Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC) na uongozi wa kituo hicho kushirikiana ili kufikia malengo ya kukuza utalii wa mikutano na kuongeza pato la taifa.

Waziri Membe ametoa changamoto hiyo jijini Arusha juzi usiku wakati akizindua bodi mpya ya Wakurugenzi iliyoteuliwa hivi karibuni ambayo Mwenyekiti wake ni Balozi Christopher Liundi. Uzinduzi huo ulifanyika katika ofisi za AICC.

Amesema kuwa pamoja na kwamba AICC inajiendesha kwa faida na kwa kiwango cha ufanisi unaoridhisha, bado bodi hiyo kwa kushirikiana na uongozi wa kituo hicho wanayo nafasi ya kufanya vizuri zaidi.

“Napenda kuchukua fursa hii kumpongeza Mkurugenzi Mwendeshaji, menejimenti na wafanyakazi wote wa AICC kwa kazi nzuri ambayo wameendelea kuifanya. Nawataka waendeleze mshikamano na kuzingatia maelekezo ya Bodi ya Wakurugenzi ili kudumisha heshima ya AICC na mchango wake kwa taifa,” alisema Membe.

Ameitaka AICC kutumia uzoefu na uelewa wa biashara ya utalii wa mikutano kuishauri serikali ili iweze kujenga misingi ya kuufanya utalii wa mikutano kuwa injini ya ukuaji wa uchumi wa taifa na kupanua maendeleo ya nchi katika nyanja ya kidiplomasia kupitia mikutano.

Aidha Waziri Membe amesema AICC inapokea wageni wengi kwa niaba ya serikali na kwamba kauli mbiu ya “We Bring the World to Tanzania” iwe changamoto kubwa katika kuendelea kupeperusha vema bendera ya taifa na kwa uaminifu.

Amesema kutokana na sekta ya utalii wa mikutano kimataifa kuchangia zaidi ya dola za kimarekani milioni 672 kwa mwaka na kukisiwa kuendelea kukua kwa wastani wa asilimia 4.2 kwa mwaka kufikia mwaka 2016, wizara imepokea kwa shauku mapendekezo ya ujenzi wa kituo kipya cha kimataifa cha mikutano cha Mount Kilimanjaro International Convention Centre (MKICC) kitakachojengwa Arusha na kwamba mapendekezo hayo yapo katika ngazi ya waraka wa Baraza la Mawaziri.

Akizungumza kwa niaba wa wajumbe wa Bodi, Mwenyekiti wa Bodi hiyo Balozi Christopher Liundi amepongeza Mwenyekiti aliyemaliza muda wake, Profesa Mwajabu Possi kwa namna alivyoweza kuingoza AICC na kuahidi kuendeleza mikakati ya kukifanya kituo hicho kuwa cha kupigiwa mfano kimataifa.

Mbali na Balozi Liundi ambaye ndiye Mwenyekiti, wajumbe katika Bodi hiyo ni Mbunge wa Singida Kaskazini Lazaro Nyalandu, Dkt Aggrey Mlimuka, Rose Lugembe, Wilfred Nyachia, Issa Suleiman, Nuru Milao, Shabani Mnubi, Joseph Chilambo na Makumba Kimweri.
Posted by MROKI On Thursday, January 21, 2010 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo