Nafasi Ya Matangazo

March 19, 2024

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto  Biteko leo anashiriki Sherehe ya kuwekwa Wakfu na Kusimikwa kwa Askofu Mpya wa Jimbo jipya la Mafinga, Ndg. Vincent Cosmas Mwagala.

Sherehe zinafanyika katika viwanja vya Kanisa Kuu la Kiaskofu jimboni Mafinga, Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa.

Jimbo hilo jipya la Mafinga limezaliwa kutoka Jimbo la Iringa.




Posted by MROKI On Tuesday, March 19, 2024 No comments
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji (Rufaa) Mhe. Jacobs Mwambegele akizungumza jijini Dar es Salaam leo tarehe 19 Machi, 2024 wakati akitoa Risala ya Uchaguzi Mdogo wa Udiwani katika kata 22 za Tanzania Bara.
***********
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam.
Wagombea Udiwani 127 kutoka vyama 18 vya siasa wanatarajiwa kupigiwa Kura katika Uchaguzi Mdogo wa Udiwani katika kata 22 za Tanzania Bara unaotarajiwa kufanyika kesho tarehe 20 Machi, 2024.
 
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji (Rufaa) Mhe. Jacobs Mwambegele jijini Dar es Salaam wakati akitoa Risala ya Uchaguzi Mdogo wa Udiwani katika kata 22 za Tanzania Bara.
 
Jaji Mwambegele amesema kati ya wagombea hao 127 wagombea wanaume ni 89 na wanawake ni 38 na kuongeza kuwa wapiga kura 128,157 walioandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura watashiriki katika uchaguzi huo mdogo na jumla ya vituo 373 vya kupigia kura vitatumika.
 
"Tume inatoa pongezi kwa wadau wote wakiwemo wapiga kura na wananchi katika kata (22) zenye uchaguzi kwa utulivu waliouonesha wakati wote wa kipindi cha kampeni,” amesema Jaji Mwambegele.
 
Jaji Mwambegele wasimamizi wa uchaguzi katika kata husika wamekamilisha taratibu zinazoweka mazingira yanayowawezesha mawakala wa vyama vya siasa kufuatilia mchakato mzima wa uchaguzi.
 
"Mawakala wanawajibika kulinda maslahi ya vyama na wagombea wao na katika utekelezaji wa majukumu yao vituoni, wanapaswa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu za uchaguzi na Maelekezo ya Tume.", amefafanua Jaji Mwambegele.
 
 Aliwataka wapiga kura katika uchaguzi huu mdogo, kujitokeza kwa wingi kwenye vituo vya kupigia kura hapo kesho, ili kuwachagua viongozi wanaowataka huku akivikumbusha vyama vya siasa, wagombea na wadau wengine wa Uchaguzi kujiepusha na vitendo vinavyoashiria uvunjifu wa amani.
 
 "Mafanikio ya uchaguzi huu yatatokana na kuwepo kwa hali ya utulivu na amani katika maeneo yote yenye uchaguzi. Hivyo, Tume inatarajia kuona hali ya amani na utulivu iliyopo sasa inaendelea kuwepo hadi shughuli za uchaguzi zitakapokamilika.", aliongeza Jaji Mwambegele.
 
Alivikumbusha vyama vya siasa, wagombea, mawakala, wapiga kura na wananchi wote kwa ujumla kuzingatia kuwa kampeni za uchaguzi mdogo wa Udiwani katika kata 22, zinahitimishwa rasmi leo tarehe 19 Machi, 2024, hivyo vyama vya siasa, wagombea na wafuasi wao hawatakiwi kufanya kampeni za aina yeyote zaidi ya saa kumi na mbili kamili (12:00) jioni ya leo.
 
Ametaja mambo mengine ambayo hayaruhusiwi kufanyika baada ya saa 12:00 na siku ya uchaguzi kuwa ni pamoja na kutumia alama za vyama vya siasa zinazoashiria kampeni kama vile vipeperushi, bendera na mavazi na kwamba upigaji kura katika maeneo yote ya uchaguzi, utafanyika katika vituo vile vile vilivyotumika wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020.
 
Alikumbusha kuwa vituo vya Kupigia Kura vitafunguliwa saa moja kamili (1:00) asubuhi na kufungwa saa kumi kamili (10:00) jioni. Iwapo, wakati wa kufunga kituo watakuwepo wapiga kura katika mstari ambao wamefika kabla ya saa kumi kamili jioni (10:00) na hawajapiga kura, wataruhusiwa kupiga kura na mtu yeyote hataruhusiwa kujiunga katika mstari wa wapiga kura baada ya saa kumi kamili (10:00) jioni.
 
"Watakaoruhusiwa kupiga kura ni wale tu ambao wamo kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwenye kata husika na wana kadi zao za mpiga kura. Hata hivyo, Tume kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 62 (a) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292, imeruhusu wapiga kura ambao wamepoteza kadi zao au kadi kuharibika kutumia vitambulisho mbadala kama vile, Pasi ya Kusafiria, Leseni ya Udereva au Kitambulisho cha Uraia kinachotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) ili mradi majina yaliyopo katika vitambulisho hivyo, yawe sawa na yaliyokuwepo katika kadi ya mpiga kura.", amefafanua Jaji Mwambegele na kuongeza kuwa:
 
"Mpiga Kura aliyepoteza kadi yake au kadi yake kuharibika ataruhusiwa kutumia kitambulisho mbadala, iwapo tu; atakuwa ameandikishwa kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na jina lake lipo katika orodha ya wapiga kura katika kituo anachokwenda kupiga kura. Aidha, majina yake yaliyopo katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura yawe yanafanana na yale yaliyopo katika kitambulisho mbadala."
 
Jaji Mwambegele alieleza kuwa kutakuwa na majalada ya nukta nundu katika vituo vya kupigia kura kwa ajili ya kuwawezesha watu wenye uoni hafifu na wenye ulemavu wa kuona ili yawasaidie kupiga kura bila usaidizi na kwa wapiga kura wenye ulemavu wa kuona na ambao hawawezi kutumia majalada hayo, wataruhusiwa kwenda vituoni na watu ambao wanawaamini na ambao watawachagua wenyewe kwa ajili ya kuwasaidia kupiga kura.
 
Kuhusu kipaumbele kwa wapiga kura, Jaji Mwambegele alisema katika vituo vya kupigia kura, kipaumbele kitatolewa kwa wagonjwa, watu wenye ulemavu, wazee, wajawazito na akina mama wanaonyonyesha watakaofika na watoto wao vituoni.
 
Alisisitiza kuwa kwa mujibu wa maelekezo yaliyomo kwenye Maadili ya Uchaguzi ya Mwaka 2020, wapiga kura watatakiwa kuondoka vituoni mara tu baada ya kupiga kura. Hivyo, Tume inawashauri wananchi kujiepusha na mikusanyiko katika maeneo ya vituo vya kupigia kura.
 
Kata zinazofanya uchaguzi ni Kimbiji (Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni), Kasingirima (Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma/Ujiji), Ndevelwa (Halmashauri ya Manispaa ya Tabora), Mshikamano (Halmashauri ya Manispaa ya Musoma), Msangani (Halmashauri ya Mji Kibaha), Utiri (Halmashauri ya Mji Mbinga), Fukayosi (Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo), Mlanzi (Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti) na Mbingamhalule (Halmashauri ya Wilaya ya Songea).
 
Kata nyingine ni Isebya (Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe), Kibata (Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa), Busegwe (Halmashauri ya Wilaya ya Butiama), Kamwene (Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba), Chipuputa (Halmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu), Buzilasoga (Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema), Mhande (Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba), Kabwe (Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi), Bukundi (Halmashauri ya Wilaya ya Meatu), Mkuzi (Halmashauri ya Wilaya ya Muheza) na Boma, Mtimbwani na Mayomboni (Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga)."
Posted by MROKI On Tuesday, March 19, 2024 No comments









Na Mwandishi wetu, Chalinze 
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imekagua utekelezaji wa miradi ya usambazaji umeme vijijini inayotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini ( REA) mkoani Pwani.

Mara baada ya ukaguzi huo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Dkt. David Mathayo ameishauri Serikali kuangalia gharama za uunganishaji umeme kwa wananchi wanaoishi katika maeneo yanayotambulika kama Vijiji Miji  ili kuwawezesha wananchi wengi zaidi kuunganisha umeme kwenye maeneo yao.

Ameshauri kuwe na usawa wa gharama za uunganishaji umeme kati ya wananchi wa vijijini na Vijiji Miji kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo za kiuchumi.

Dkt. Mathayo ameyasema hayo tarehe 18 Machi, 2024 mkoani Pwani ambapo katika ukaguzi huo, Kamati iliambatana na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya  Nishati, Dkt. James Mataragio.

 Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Judith Kapinga amewashauri wakazi wa vijijini kutumia  umeme kwa shughuli za maendeleo na kuchangamkia uunganishaji wa umeme kwenye maeneo yao mara baada ya Serikali kufikisha miundombinu ya umeme.

Kapinga amesema wakazi wa vijijini hulipia gharama za umeme wa REA kwa shilingi 27,000 baada ya Serikali kulipia gharama nyinginezo huku wakazi wa Vijiji  Miji wakilipia shilingi 320,000 sawa na wakazi wa mijini.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa  Wizara ya Nishati, Dkt. James Mataragio alitoa rai kwa wananchi vijijini kuchangamkia fursa  ya kuunganishiwa umeme kwa bei ya chini kwani Serikali inatumia fedha nyingi kuhakikisha umeme unafika kwenye maeneo hayo.

Awali Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi Hassan Saidy  alisema zaidi ya shilingi Bilioni 44 zimetumika katika kutekeleza miradi ya REA  na kufanikisha kusambaza umeme katika vijiji zaidi ya 100 kati ya vijiji 110 vilivyopo mkoani Pwani.
Posted by MROKI On Tuesday, March 19, 2024 No comments


Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu,  Utamaduni na Michezo chini ya Mwenyekiti wake Mhe. Husna Sekiboko (Mb) imeielekeza Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo iongeze bajeti ya Mfuko wa Utamaduni na Sanaa ili Mfuko huo uweze kukopesha Wasanii wengi zaidi.
 
Mhe. Husna ametoa maelekezo hayo Machi 18, 2024 Jijini Dar es Salaam baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa Mfuko huo ambapo amesema Mfuko huo unapaswa kuwa na Sheria, hivyo wizara ianze mchakato wa kuhakikisha sheria hiyo inapatikana.
 
"Dhamira ya Mfuko huu ni kuendeleza Wasanii, hakikisheni fedha wanazokopa ni kwa ajili ya kufanya kazi ya sanaa na si vinginevyo, Benki ambazo zinatoa mikopo hii hakikisheni mnatoa masharti yanayofanana na kazi wanazofanya Wasanii na Wizara pia endeleeni kuweka mazingira bora ya upatikanaji wa soko la kazi hizo", amesisitiza Mhe. Husna.
 
Awali Naibu Waziri wa wizara hiyo, Mhe. Hamis Mwinjuma amesema wizara imefanikiwa kusimamia mfuko huo ili utekeleze majukumu yake kwa kuendelea kuongeza vyanzo vipya vya mapato tofauti na ruzuku ya Serikali pekee kwa kuwa wahitaji ni wengi.
 
Ameongeza kuwa, tangu kuanza kwa utekekezaji wa kukusanya kodi kwenye vifaa vya kuhifadhia kazi za sanaa ambayo ni asilimia 1.5, hadi sasa kiasi cha shilingi milioni 465 zimekusanywa ambapo asilimia 10 ya fedha hizo zinaenda kwenye Mfuko huo kwa lengo la kuongeza vifaa vingine ambayo vinatumika kuhifadhia kazi hizo.
Posted by MROKI On Tuesday, March 19, 2024 No comments

March 18, 2024

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Balozi Dk. Emmanuel John Nchimbi (kushoto) kwenye picha ya pamoja na Katibu Mkuu wa Chama cha SWAPO (Namibia) Komredi Sophia Shaningwa (katikati) na Katibu Mkuu wa Chama cha ANC (Afrika Kusini), Komredi Fikile Mbalula (kulia), wakionesha alama ya salaam za CCM, Chama cha ANC na Chama cha SWAPO, leo Jumatatu, Machi 18, 2024, pembezoni mwa siku ya kwanza ya Mkutano wa 11 wa Makatibu Wakuu wa Vyama Rafiki vya Ukombozi Kusini mwa Afrika, unaofanyika katika Mji wa Victoria Falls, nchini Zimbabwe. Makatibu Wakuu  wa Vyama wengine wanaoshiriki mkutano huo ni pamoja na Komredi Roque Silva Samuel (FRELIMO - Msumbiji), Komredi Paulo Pombolo (MPLA - Angola), Komredi Kavis Kario (BDP – Botswana) na Komredi Albert Mpofu (ZANU – PF - Zimbabwe), ambaye ni mwenyeji wa mkutano huo.

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel John Nchimbi akijadiliana jambo na wajumbe wa msafara wake aliombatana nao kushiriki Mkutano wa 11 wa Makatibu Wakuu wa Vyama Rafiki vya Ukombozi Kusini mwa Afrika (FLMS), leo Jumatatu, Machi 18, 2024. Kutoka kushoto ni Gilbert Kalima (Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi), Fack Lulandala (Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM – UVCCM), akifuatiwa na Tunu Juma Kondo (Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake – UWT – Zanzibar). Mkutano huo unaofanyika katika Mji wa Victoria Fall, nchini Zimbabwe, umewakutanisha Makatibu Wakuu wengine wa vyama hivyo rafiki, ambao ni pamoja na Katibu Mkuu wa Chama cha SWAPO (Namibia) Komredi Sophia Shaningwa, Katibu Mkuu wa Chama cha ANC (Afrika Kusini), Komredi Fikile Mbalula, Komredi Roque Silva Samuel (FRELIMO - Msumbiji), Komredi Paulo Pombolo (MPLA - Angola), Komredi Kavis Kario (BDP – Botswana) na Komredi Albert Mpofu (ZANU – PF - Zimbabwe), ambaye ni mwenyeji na mwenyekiti wa mkutano huo.

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel John Nchimbi akizungumza wakati wa kutoa salaam za CCM za mshikamano kwenye Mkutano wa 11 wa Makatibu Wakuu wa Vyama Rafiki vya Ukombozi Kusini mwa Afrika (FLMS), leo Jumatatu, Machi 18, 2024. Mkutano huo unaofanyika katika Mji wa Victoria Falls, nchini Zimbabwe, umewakutanisha Makatibu Wakuu wengine wa vyama hivyo rafiki, ambao ni pamoja na Katibu Mkuu wa Chama cha SWAPO (Namibia) Komredi Sophia Shaningwa, Katibu Mkuu wa Chama cha ANC (Afrika Kusini), Komredi Fikile Mbalula, Komredi Roque Silva Samuel (FRELIMO - Msumbiji), Komredi Paulo Pombolo (MPLA - Angola), Komredi Kavis Kario (BDP – Botswana) na Komredi Albert Mpofu (ZANU – PF - Zimbabwe), ambaye ni mwenyeji na mwenyekiti wa mkutano huo.
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel John Nchimbi akizungumza wakati wa kutoa salaam za CCM za mshikamano kwenye Mkutano wa 11 wa Makatibu Wakuu wa Vyama Rafiki vya Ukombozi Kusini mwa Afrika (FLMS), leo Jumatatu, Machi 18, 2024. Mkutano huo unaofanyika katika Mji wa Victoria Falls, nchini Zimbabwe, umewakutanisha Makatibu Wakuu wengine wa vyama hivyo rafiki, ambao ni pamoja na Katibu Mkuu wa Chama cha SWAPO (Namibia) Komredi Sophia Shaningwa, Katibu Mkuu wa Chama cha ANC (Afrika Kusini), Komredi Fikile Mbalula, Komredi Roque Silva Samuel (FRELIMO - Msumbiji), Komredi Paulo Pombolo (MPLA - Angola), Komredi Kavis Kario (BDP – Botswana) na Komredi Albert Mpofu (ZANU – PF - Zimbabwe), ambaye ni mwenyeji na mwenyekiti wa mkutano huo.
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Balozi Dk. Emmanuel John Nchimbi (wa pili kutoka kushoto) akiwa kwenye picha ya pamoja, leo Jumatatu, Machi 18, 2024, pembezoni mwa siku ya kwanza ya Mkutano wa 11 wa Makatibu Wakuu wa Vyama Rafiki vya Ukombozi Kusini mwa Afrika, unaofanyika katika Mji wa Victoria Falls, nchini Zimbabwe. Makatibu Wakuu wengine pichani, (kutoka kulia) ni Komredi Roque Silva Samuel (FRELIMO - Msumbiji), Komredi Paulo Pombolo (MPLA - Angola), Komredi Albert Mpofu (ZANU – PF - Zimbabwe, mwenye suti), Komredi Sophia Shaningwa (SWAPO – Namibia) na Komredi Fikile Mbalula (ANC – ANC).

Mkutano wa 11 wa vyama rafiki vya Ukombozi Kusini Mwa Afrika (FLMS), unaowakutanisha wajumbe wake, ambao ni pamoja na Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel John Nchimbi, Katibu Mkuu wa Chama cha SWAPO (Namibia), Komredi Sophia Shaningwa, Katibu Mkuu wa Chama cha ANC (Afrika Kusini), Komredi Fikile Mbalula, Katibu Mkuu wa Chama cha FRELIMO (Msumbiji), Komredi Roque Silva Samuel, Katibu Mkuu wa Chama cha MPLA (Angola), Komredi Paulo Pombolo, Katibu Mkuu wa Chama cha BDP (Botswana), Komredi Kavis Kario na Katibu Mkuu wa Chama cha ZANU – PF (Zimbabwe), Komredi Albert Mpofu, (mwenyeji na mwenyekiti wa mkutano), ukiendelea kujadili agenda, leo Jumatatu, Machi 18, 2024, katika ukumbi ulioko Mji wa Victoria Falls, nchini Zimbabwe, unakofanyikia.
Posted by MROKI On Monday, March 18, 2024 No comments
Waziri Mavunde na CEO wa Barrick wakikata utepe kuzindua chuo, katikati ni mkuu wa wilaya ya Kahama, Mboni Mhita
***********
Waziri wa Madini, Mhe. Antony Mavunde, ameipongeza Kampuni ya Dhahabu ya Barrick ambayo inaendesha shughuli zake nchini kwa ubia na Serikali kupitia kampuni ya Twiga Minerals, kwa kufanya uwekezaji unaoendelea kuchangia kukuza uchumi na kufanikisha miradi ya kijamii ambayo inaendelea koboresha maisha ya wananchi.

Mh. Mavunde, ametoa pongezi hizo leo Jumatatu Machi 18,2024 wilayani Kahama wakati wa uzinduzi wa Chuo cha mafunzo cha Barrick chenye hadhi ya kimataifa kijulikanacho kama Barrick Academy, katika mgodi wa zamani wa Buzwagi wilayani Kahama ambao umefungwa ambacho kitakuwa kinatoa mafunzo kwa wafanyakazi wa Barrick wa nchini na nje ya nchi kupata utaalamu wa kuendesha shughuli zao kwa weledi.

Waziri Mavunde amesema ulimwengu wa sasa ni wa sayansi na teknolojia hivyo chuo hicho kimeanzishwa katika wakati muafaka ambapo sekta ya madini nchini inakua kwa kasi sana na kuhitaji wataalamu wa kutosha.

Ametoa wito kwa uongozi wa Barrick kuangalia uwezekano wa kuanzisha kozi za kuwasaidia wachimbaji wadogowadogo nao wapate maarifa ya kuendesha kazi zao kwa maarifa.

“Barrick mmeanza kwa kufungua chuo katika eneo hili la Ukanda Maalum wa Kiuchumi la Buzwagi la Serikali, nina imani wawekezaji wengi watajitokeza kujenga viwanda ili kuziba athari za kiuchumi zilizotokana na kufungwa kwa mgodi wa Buzwagi”,amesisitiza.

Kwa upande Rais na Afisa Mtendaji Mkuu wa Barrick, Mark Bristow, amesema Barrick itaendelea kufanya kazi na Serikali kuhakikisha ubia wake unanufaisha pande zote na kuchangia kukuza uchimi wa nchi,

Bristow amesema Barrick, inalipa umuhimu kubwa suala la elimu na itaendelea kuwekeza katika sekta hiyo ili kuhakikisha watanzania wanapata elimu na ndio maana imeamua kufungua chuo kikubwa cha kimataifa cha Barrick Academy nchini.

“Tutaendelea kuhakikisha kuwa ubia wetu na Serikali ya Tanzania unakuwa wa kuigwa katika sehemu mbalimbali duniani kwa kufanikisha kuleta mafanikio na maendeleo chanya kwa wananchi”, alisisitiza Dkt. Bristow.

Bristow amesema Chuo cha Barrick kimebuniwa na Barrick ili kutoa programu maalumu za mafunzo zinazoandaliwa kulingana na mahitaji zinazolenga kuandaa mameneja wa mstari wa mbele wa Barrick ili wakue kama watu binafsi na viongozi katika nyanja zao huku kozi hizo zikiwapa ujuzi wa kusimamia timu zao kwa ufanisi zaidi na kuboresha utendaji.

“Chuo cha Barrick kitakuwa kikitoa mafunzo kwa mafomeni, wasimamizi na warakibu zaidi ya 2,000 kutoka Kannda ya Afrika Mashariki na Kati katika kipindi cha miezi 24 ijayo. Tukiwa na maono ya mbele, tunajitayarisha pia kuwajumuisha Wakandarasi wetu na kupanua mtaala ili kufikia taaluma nyingi zaidi ikiwa ni pamoja na kutoa kozi za uongozi katika masuala ya fedha, ujuzi wa ngazi ya juu wa Kompyuta na katika masuala ya usalama”,ameongeza Bristow.

Ameeleza kuwa, ufunguzi wa chuo cha Barrick unafuatia ujenzi wa jengo la abiria katika uwanja wa ndege wa Buzwagi Kahama mnamo mwezi Januari 2024 lililofungua fursa kwa ajili ya huduma za ndege zilizopangwa ambalo linaweza kuhudumia zaidi ya abiria 200 kwa wakati mmoja ambapo jengo hilo linatarajiwa kuwa kichocheo kikubwa cha ukuaji uchumi katika Manispaa ya Kahama.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Afisa Mkuu wa Uendeshaji wa Barrick katika Kanda ya Afrika Mashariki na Kati, Sebastiaan Bock amesema uwanja wa ndege na Chuo katika mgodi uliofungwa wa Buzwagi ni sehemu ya mpango wa Barrick wa kuibadili Buzwagi kuwa Ukanda Maalum wa kiuchumi.

“Upembuzi yakinifu uliofanyika mwaka 2021 ulionesha kuwa uundwaji wa Kanda maalumu ya kiuchumi ulikuwa na uwezo wa kuchukua nafasi ya mgodi wa Buzwagi kama kichocheo cha uchumi wa eneo hili na unaweza kutengeneza ajira zipatazo 3,000 kila mwaka, kuzalisha zaidi ya dola 150,000 kila mwaka kutokana na tozo za huduma kwa Manispaa ya Kahama na kutoa takribani dola milioni 4.5 kwa mwaka kama kodi ya ajira”,amesema Sebastiaan.

Amesema Serikali ya Tanzania iliidhinisha ubadilishaji wa mgodi wa Buzwagi kuwa ukanda maalum wa kiuchumi (SEZ) kupitia tangazo la Serikali ilitolewa mwezi Februari 2024 na tayari Wawekezaji wameanza mchakato wa kuanzisha viwanda katika eneo hilo.

“Namna tunavyofunga migodi yetu ni muhimu kwetu kama ambavyo tunaijenga na kuiendesha. Mgodi wetu wa Buzwagi ulikuwa kitovu cha uchumi katika ukanda huu kwa takribani miaka 15 kabla ya kutoa dhahabu yake ya mwisho mwaka 2021. Hata hivyo, mtazamo wetu huo siyo mwisho wa hadithi hii kwa Buzwagi tunapoibadilisha kuwa mali mbadala yenye tija ambayo itahudumia jamii kwa miongo kadhaa ijayo”,amesema Bock.

Naye Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Uwekezaji kwa Mauzo ya Nje (EPZA) Charles Itembe, ameipongeza Kampuni ya Barrick kwa kubuni wazo la kuanzisha Chuo cha Barrick huku akiwaomba wawekezaji mbalimbali kujitokeza kuwekeza katika eneo hilo ili kuongeza thamani ya madini na vitu vingine kwenye eneo la Buzwagi ambako kutakuwa na viwanda zaidi ya 100 na mpaka sasa kuna wawekezaji wanane.

Mkuu wa Wilaya ya Kahama Mhe. Mboni Mhita amesema kuanzishwa kwa Chuo cha Barrick ni matokeo mazuri ya ushirikiano baina ya Serikali ya Tanzania na Kampuni ya Barrick ili kukuza uwekezaji nchini.
Mbunge wa Jimbo la Kaham Mjini Mhe. Jumanne Kishimba amewapongeza Barrick kuwa wawekezaji wa kwanza katika Mgodi uliofungwa wa Barrick huku akiomba chuo hicho pia kitumike kutoa mafunzo ya madini kwa wachimbaji wadogo na jinsi ya kufanya biashara ya madini huku Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kahama Thomas Myonga akisema uwekezaji unaofanyika katika eneo hilo ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya CCM katika kukuza uwekezaji nchini.

Waziri wa Madini, Mhe. Antony Mavunde
Rais na Afisa Mtendaji Mkuu wa Barrick, Mark Bristow
Afisa Mkuu wa Uendeshaji wa Barrick katika Kanda ya Afrika Mashariki na Kati, Sebastiaan Bock
Meneja wa Barrick nchini, Melkiory Ngido
Waziri wa Madini Antony Mavunde na CEO wa Barrick wakibadilishana mawazo wakati wa hafla hiyo
Sehemu ya wageni waalikwa
Wanafunzi wa awamu ya kwanza katiika chuo katika picha ya pamoja na Waziri Mavunde na Rais na Afisa Mtendaji Mkuu wa Barrick, Mark Bristow na viongozi wengine wa mkoa wa Shinyanga.
Posted by MROKI On Monday, March 18, 2024 No comments
 






Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Biteko ameagiza Watendaji wa Wizara ya Nishati kuanzisha Kitengo maalum cha usimamizi wa Nishati Safi ya Kupikia ili kutekeleza kwa ufanisi ajenda ya Nishati Safi ya Kupikia na siyo tu kuishia kwenye kuandaa na kushiriki makongamano kisha masuala yote yanaishia hapo.

Amesema hayo tarehe 18 Machi, 2024 jijini Mwanza wakati akifungua Mkutano wa Tano wa Baraza la Wafanyakazi la Wizara  ya Nishati wenye lengo mahsusi la kupitia na kupitisha rasimu ya Bajeti ya Wizara ya Nishati kwa mwaka 2024/2025.

 “Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ndiye kinara wa utekelezaji wa ajenda ya Nishati Safi ya Kupikia Afrika hivyo wizara lazima iweke mkakati wa kitaasisi na kimfumo ili kufanikisha ajenda hiyo ili utekelezaji wa suala hili usiwe ni jambo la zimamoto.” Amesema Dkt. Biteko

Vilevile, Dkt.Biteko amesema kuwa, Wizara ya Nishati ina jukumu la kuihamisha nchi kutoka matumizi ya mafuta na kuhamia kwenye matumizi ya gesi (CNG) kwa kutengeneza mazingira ambayo yatapunguza utegemezi wa mafuta na hivyo kufanya nchi kujiendesha kwa kutumia CNG hivyo, ameagiza Watendaji wa Wizara kusimamia pia utekelezaji wa suala hilo.

Kuhusu Watumishi wa Wizara ya Nishati, Dkt. Biteko  amewakumbusha Watumishi kufanya kazi kwa bidii huku wizara ikiangalia stahiki zao ikiwemo motisha.

Amesema kuwa, Watumishi wa Wizara ya Nishati wana deni la kuwatumikia Watanzania kwani ndio waliopewa dhamana ya kusimamia Sekta ya Nishati kwa niaba yao hivyo watimize wajibu huo.

Vilevile, ametoa wito kwa  Wizara ya Nishati kuwa na utaratibu wa kuwapa motisha watumishi wanaofanya vizuri katika kazi na wale wazembe na wasiotumikia wananchi kwa weledi na kwa wakati watambuliwe pia na kuchukuliwa hatua stahiki.

Aidha, ametoa angalizo kwa wenye mamlaka ndani ya Wizara na Taasisi zake kutoona fahari ya kutumia vyeo vyao kwa ajili ya kuabudiwa na kutukuzwa kwani nafasi walizonazo ni za muda tu, hivyo wajijengee marafiki zaidi kuliko maadui na kujikita katika kuhudumia wananchi na hivyo kuepuka kuchafua utendaji wa Wizara ya Nishati na Taasisi zake.

Pia, amewataka Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi Wizara ya Nishati kupitia bajeti hiyo kwa umakini kabla haijafika katika ngazi ya Kamati ya Bunge na baadaye  katika Bunge la Bajeti.

Ameongeza kuwa, kama kuna changamoto zozote ambazo Baraza hilo wanaona kuwa zipo katika Sekta basi wazijadili na kutoa njia mbadala ya kutatua changamoto hizo.

“Mfano, pamoja na mradi wa Julius Nyerere kuanza kuzalisha umeme lakini bado tunapaswa kuendeleza miradi mingine kwani JNHPP ni holiday ya muda mfupi, kama tunafikiria miaka 50 mbele lazima tutambue kuwa lazima tuendeleze vyanzo vingine vya umeme ili kuwa na umeme wa ziada., hivyo mna wajibu wa kuja na njia mbadala” Amesema Dkt. Biteko

Awali Mwenyekiti wa Baraza hilo  ambaye ni Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, alisema kuwa baada ya Baraza hilo kupitisha Bajeti ya Wizara kwa mwaka 2024/ 2025 hatua inayofuata ni kupitishwa kwenye Kamati za Bunge na baadaye Waziri wa Nishati ataisoma bungeni kwa ajili ya kupitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kuhusu bajeti ya mwaka 2023/2024, Mhandisi Mramba amesema kuwa masuala yaliyopangwa kufanyika kwenye bajeti hiyo yametekelezwa kwa kiasi kikubwa na hii ikitoa mwanga kuwa bajeti ijayo pia itatekelezwa vizuri. 

Ameongeza kuwa, kwa sasa Sekta ya Nishati inatazamwa upya kwa kuangalia mchango wa nishati jadidifu katika Sekta, nishati bora ya kupikia, uhifadhi way nishati na matumizi bora ya nishati lengo likiwa ni kuiboresha zaidi Sekta husika kwenye nyanja mbalimbali.
Posted by MROKI On Monday, March 18, 2024 No comments







Na Mwandishi wetu, Dodoma
Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba amesema kuwa Serikali kupitia  Tume  ya Madini itaendelea kuweka mazingira mazuri kwa wachimbaji wadogo wa madini nchini  kama mkakati wa kuhakikisha mchango wao kwenye Sekta ya Madini unaendelea kukua sambamba na kuzalisha ajira zaidi.

Mhandisi Samamba ameyasema hayo leo Machi 18, 2024 kwenye kikao cha sita cha Baraza la Wafanyakazi wa Tume ya Madini kilichofanyika jijini Dodoma ambacho kimeshirikisha Wakurugenzi, Mameneja, Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa, watumishi na wageni waalikwa kutoka TUGHE, na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).

Amesema kuwa, mchango wa wachimbaji wadogo kwenye mapato yatokanayo na Sekta ya Madini umeendelea kukua kutoka asilimia tano (5) hadi asilimia arobaini (40) Mwaka 2022/2023 na kusisitiza kuwa Tume ya Madini itaendelea kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji kwa wachimbaji wadogo sambamba na kutatua changamoto mbalimbali.

Akielezea mafanikio yaliyopatikana tangu kuanzishwa kwa Tume ya Madini, Mhandisi Samamba amesema kuwa ni pamoja na ongezeko la ukusanyaji wa maduhuli kutoka shilingi bilioni 213.3 katika kipindi cha mwaka wa fedha  2016/17 hadi shilingi bilioni 677.7 katika kipindi cha mwaka wa fedha 2022/2023.

“Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2022/2023 kama Tume ya Madini tulipewa lengo la kukusanya kiasi cha shilingi bilioni  822 na kufanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 677.7  ikiwa ni (82.45%) na katika kipindi cha mwaka wa fedha 2023/2024 tumepewa lengo la kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 882 ambalo ninaamini kabisa tutalivuka,” amesema Mhandisi Samamba.
 
Mhandisi Samamba ameendelea kusema kuwa  siri ya mafaniko kwenye ukusanyaji wa maduhuli ni pamoja na uzalendo na ubunifu wa  watumishi wa Tume ya Madini Makao Makuu, Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa, Maafisa Migodi Wakazi na ushirikiano mkubwa kutoka kwa viongozi wa Wizara ya Madini.

Ameendelea kueleza mafanikio mengine kuwa ni pamoja na uanzishwaji wa  masoko ya madini 42 na vituo vya ununuzi wa madini 100 nchini,  ongezeko la utoaji wa leseni za madini  kutoka leseni 5094 katika mwaka wa fedha 2018/2019 hadi leseni 9642 katika mwaka wa fedha 2022/2023, kudhibiti utoroshaji wa madini na kupungua kwa ajali kwenye migodi ya madini kutokana na kaguzi zinazofanywa mara kwa mara kwenye shughuli za uchimbaji wa madini sambamba na kutolewa kwa elimu.

Amefafanua mafanikio mengine kuwa ni pamoja na ongezeko la ushiriki wa kampuni za kitanzania kwenye utoaji wa huduma kwenye migodi kutokana na maboresho ya kanuni za ushirikishwaji wa watanzania katika Sekta ya Madini ambapo hadi  kufikia mwaka 2022 asilimia 86 ya bidhaa na huduma zinatolewa na kampuni za kitanzania kwenye kampuni kubwa za uchimbaji wa madini huku asilimia 14 zikitolewa na kampuni za nje ya nchi kupitia kibali maalum kinachotolewa na Tume ya Madini na kwa upande wa ajira katika migodi ya madini asilimia 97 ni watanzania huku raia wa kigeni wakiwa ni asilimia (3) tatu.

“Mchango wa Sekta ya Madini kweye Pato la Taifa uliongezeka kutoka asilimia 4.4 mwaka 2017 hadi asilimia 9.1 mwaka 2022; tumejipanga kuhakikisha tunavuka lengo lililowekwa la asilimia 10 kabla ya mwaka 2025,” amesema Mhandisi Samamba.

Katika kikao hicho mbali na kujadili, kutatua changamoto mbalimbali katika Sekta ya Madini na kuweka mikakati ya baadaye, wajumbe wamepata fursa ya kupata elimu kutoka kwa wataalam kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).
Posted by MROKI On Monday, March 18, 2024 No comments
  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo