Nafasi Ya Matangazo

October 04, 2009

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Mheshimiwa RAIS Jakaya Mrisho Kikwete (pichani akihutubia leo) Jumapili, Oktoba 4, 2009, amelazimika kupumzika kwa dakika chache katika chumba cha mapumziko kwenye Uwanja wa Kirumba, mjini Mwanza, mara tu baada ya kumaliza hotuba yake wakati wa sherehe za miaka 100 tokea kuanzishwa kwa Kanisa la African Inland Church (AIC) katika Tanzania.

Mhe. Rais amelazimika kupumzika kutokana na kuzidiwa na uchovu kufuatia shughuli nyingi mfululizo katika siku za karibuni. Baada ya mapumziko hayo, Mhe. Rais aliendelea kushiriki katika shughuli hizo hadi mwisho wa shughuli hiyo ya AICT.

“Nguvu imerudi…napenda sasa kuchukua nafasi hii kuzindua rasmi uchangiaji wa shughuli za Kanisa lenu na mimi naanza na mchango wa sh. 1,000,000,” Rais Kikwete amewaambia maelfu ya waumini wa AICT huku wakimshangilia kwa nguvu mara aliporejea jukwaani.

Rais Kikwete amekuwa na shughuli nyingi na hajapumzika katika miezi kadhaa iliyopita kutokana na kazi nyingi na ratiba ya shughuli za mfululizo. Aidha ndani ya siku 15 zilizopita, Rais Kikwete amekuwa New York nchini Marekani kuhudhuria Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UN) mjini New York, na juzi na jana alikuwa mjini Arusha na jana na leo mjini Mwanza.

Rais ameanza kusikia uchovu wakati akisoma hotuba yake mbele ya maelfu ya waumini wa Kanisa hilo.

Baada ya kuwa amemaliza hotuba hiyo ameingia katika chumba cha kupumzika kwa dakika chache na baadaye akarudi kujiunga na waumini hao kuendelea na sherehe hizo.

Rais Kikwete ameendelea kubakia kwenye sherehe hizo hadi mwisho wa ratiba yake na wakati akiwaaga waumini hao amesema:

“Kwa kweli mshituko huu wa leo ni matokeo ya ubishi wangu. Nilishauriwa na wasaidizi wangu nipumzike baada ya kurejea nyumbani kutoka Marekani. Niliambiwa nisiende Arusha ama kuja hapa. Lakini nikakataa. Siku nyingine nitawasiliza zaidi.”

Rais Kikwete aliondoka kwenda Marekani kuhudhuria Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) Septemba 20 na tokea hapo hajapata kupumzika.

Alirejea nchini kutoka Marekani saa saba usiku wa kuamkia Ijumaa baada ya kuwa amesafiri kwa zaidi ya masaa 19 na asubuhi ya Ijumaa akasafiri kwenda Arusha kufungua Mkutano wa 55 wa Wabunge wa Jumuia ya Madola.

Rais alikuwa amepangiwa kurejea Dar es Salaam baada ya shughuli ya Arusha, lakini akalazimika kwenda Mwanza kwa shughuli ya Kanisa la AICT kwa sababu Waziri Mkuu aliyekuwa amepangiwa na Rais kushiriki shughuli hiyo alipewa kazi nyingine na Rais.

Wakati huo huo, Ofisi Binafsi ya Rais (OBR) imetangaza kuwa itaangalia upya ratiba ya Mhe. Rais kwa namna ya kumpungumzia mlundiko wa shughuli hata kama yeye binafsi ni mpenzi mkubwa wa kuchapa kazi na kutumikia wananchi.



Ofisi hiyo ndiyo husimamia kupanga ratiba za Mhe. Rais na baada ya tukio la leo imetangaza kuwa inaangalia upya ratiba nzima ya matukio yajayo ya Mhe. Rais kwa namna ya kuyapunguza na kumpa muda zaidi wa kupumzika.

Hata hivyo, Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu inapenda kuwahakikishia wananchi kwamba Mhe. Rais ni mzima wa afya na anaendelea vizuri.

Imetolewa na:
Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweimamu akizungumza na waandishi wa habari jioni kuhusiana na taarifa hiyo.

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
Posted by MROKI On Sunday, October 04, 2009 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo