Katika kuelekea kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Queen Sendiga, leo tarehe 4 Machi 2025 ameweka jiwe la msingi kwenye mradi wa ujenzi wa miundombinu ya uvunaji wa maji ya mvua kupitia paa la jengo katika Shule ya Sekondari Malimbika, wilayani Gairo, mkoa wa Morogoro.
Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali, akiwemo Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Ramadhan, wabunge wanawake wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira, viongozi wa Chama cha Mapinduzi, watendaji wa Wizara ya Maji, pamoja na kina mama wa mjini Gairo.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Sendiga amewapongeza watumishi wanawake wa Wizara ya Maji kwa kuunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutoa nguvu kazi na rasilimali fedha ili kuwezesha utekelezaji wa mradi huo pamoja na miradi mingine minane ya aina hiyo, inayolenga kuboresha upatikanaji wa maji katika shule na maeneo mengine nchini.
Aidha, Mhe. Sendiga ameweka wazi kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imewekeza zaidi ya shilingi trilioni 2 katika miradi ya sekta ya maji, hatua ambayo imeongeza upatikanaji wa maji nchini kutoka wastani wa 84% mwaka 2021 hadi kufikia 91%.
0 comments:
Post a Comment