Nafasi Ya Matangazo

June 14, 2024

TUME ya Madini imewataka watumishi wake nchini kutumia muda mwingi kufanya kazi huku wakitenga muda wa kufanya mazoezi na kushiriki michezo mbali mbali ili kuimarisha afya ya mwili kupambana na magonjwa yasiyoambukiza.

Akizungumza leo Juni 14, 2024 kwa niaba ya Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini Mhandisi Yahya Samamba,  Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Migodi na Mazingira, Mhandisi Ramadhan Lwamo amesema siku zote afya ndio kazi , afya mgogoro hakuna kazi.

Mhandisi Lwamo ameyasema hayo akifunga Bonanza la Wakurugenzi, Mameneja kutoka Tume ya Madini Makao Makuu Dodoma na Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa lililofanyika kwenye uwanja wa Donge TFF jijini Tanga.

 ‘Michezo ni furaha, inaimarisha mahusiano na kuboresha afya zetu  watumishi, baada ya bonaza ‘reflection’ yake tunaiona kwenye matokeo ya kuimarisha ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali,”amesema Lwamo.

Naye, Mkurugenzi wa Huduma za Tume CPA. William Mtinya akizungumza amesema, Tume imeweka utaratibu wa kuhamasisha watumishi wake kufanya mazoezi na kushiriki michezo mbali mbali ili  kuwaweka vyema kiafya na kuwa  imara  katika utendaji kazi wao.

Amesema pia Tume inatekeleza maagizo ya Serikali kwamba kila Taasisi idumishe michezo ili kupunguza magonjwa yasiyoambukiza ambayo yamekuwa yakisumbua  jamii na kwamba bonanza hilo pia huleta mshikamano wa wafanyakazi na kubadilishana mawazo.

“Tumekutana kujadili mikakati ya kukusanya maduhuli ya Serikali, kuimarisha afya zetu  na Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa, kimsingi mchezo ulikuwa upande wetu na tumefanikiwa kuwafunga magoli mawili bila,”amesema  CPA Mtinya.

Naye Afisa Madini Mkazi wa Kahama, Mhandisi  Joseph Kumburu  akizungumzia matokeo ya kufungwa mabao mawili kwa bila amesema kuwa wamekubali  matokeo, walizidiwa na mchezo.

“Kipindi cha kwanza wenzetu wa Makao Makuu wamecheza vizuri kipindi cha pili tulikuwa na majeruhi, mpira ulikuwa mzuri bahati haikuwa ya kwetu,”amesema Mhandisi Kumburu.

Katika Bonanza hilo lililofanyika kwenye uwanja wa Donge TFF jijini Tanga, Timu ya soka ya Tume ya Madini kutoka Makao Makuu Dodoma iliibugiza RMO’s mabao 2-0 na kutwaa Kombe.

Katika bonanza hilo vikombe na medani zimetolewa kwa washindi ikiwa ni pamoja na mfungaji bora katika mchezo wa mpira wa miguu  Azihar Kashakara kutoka Tume Makao Makuu,  mlinda mlango bora  CPA Wiliam Mtinya kutoka Tume Makao Makuu na  mchezaji bora Mhandisi Sabai Nyansiri kutoka Ofisi ya Afisa Madini Mkazi- Singida.

Mbali na mpira wa miguu pia bonanza hilo limehusisha michezo ya kuvuta kamba, kukimbia mita 100 na kufukuza kuku ambapo washindi wamekabidhiwa medani mbalimbali.
Posted by MROKI On Friday, June 14, 2024 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo