Nafasi Ya Matangazo

June 14, 2024

Na Mwandishi wetu, Tabora
TARURA Mkoa wa Tabora imepokea fedha za dharura  kiasi cha shilingi milioni 790  kwaajili ya kurejesha mawasiliano ya miundombinu ambayo yameathiriwa na mvua za Elnino mkoani humo.

Meneja wa TARURA Mkoa wa Tabora, Mhandisi Lusako Kilembe amesema kwamba fedha hizo zitatumika kurejesha mawasiliano ya barabara ambazo zilikatika kutokana na mvua hizo ili wananchi waweze kuendelea na shughuli zao za kawaida.

“Sasa hivi tumeanza kurejesha mawasiliano ya miundombinu katika Manispaa ya Tabora, pia katika wilaya nyingine kazi ya kurejesha mawasiliano ya miundombinu inaenda kuanza hivyo wananchi wataweza kupata huduma za kijamii na kuendelea na shughuli zao za kiuchumi”, alisema.

Aidha, Mhandisi Kilembe alitaja fedha hizo za dharura zimepelekwa katika wilaya zote, barabara ya Igunga-Itumba-Simbo milioni 100 (Igunga), milioni  73 barabara ya Kazaroho-Mpandamlowoka (Kaliua), barabara ya Mwangoye-Senge-Nindo-Mwamala milioni 92 (Nzega), barabara  ya Kitangili-Mbogwe-Nhele milioni 64.8 (Nzenga TC) barabara ya Usunga-Imalampaka na Urafiki-Mwanasongezya milioni 57 (Sikonge) na barabara ya Ndeyelwa na Kakola-Ikomwa na Igombe-Igambilo milioni 275 (Manispaa ya Tabora).

Amesema fedha hizo zitatumika kufukia mashimo kwa kujaza vifusi, ujenzi wa Kalavati, kunyanyua tuta za barabara, kuweka changarawe, kurekebisha kingo za maji, ujenzi wa boksi kalavati, kuimarisha kingo za madaraja pamoja na kuondoa maji kwenye mitaro ya barabara. 

Hata hivyo Meneja huyo amewataka wananchi kutunza miundombinu kwani fedha nyingi zinatumika kujenga barabara hivyo wanapaswa kulinda miundombinu ili kusitokee watu watakaoharibu kingo za barabara pamoja na alama zake na endapo itatokea hivyo ni vyema wakatoa taarifa kwenye mamlaka za serikali.

“Nitoe rai kwa wananchi waweze kulinda miundombinu hii kwakuwa wapo baadhi ya watu wana tabia ya kukata bomba na vifaa vingine kwenye kingo za madaraja pamoja na alama za barabarani, watambue kwamba serikali inatumia fedha nyingi kurejesha miundombinu hiyo na wao kama  watumiaji wa barabara hizo wanapaswa kuzilinda ili ziweze kutumika kwa muda mrefu", alisema.


TARURA  mkoa wa Tabora unahudumia mtandao wa barabara wenye urefu wa km. 8,404.88 kati ya hizo km.112 za lami, km. 620 barabara za udongo, km. 2007 barabara za changarawe. 

Naye, Mtendaji wa kijiji cha Magoweko Bw. Onesmo Halinga amesema wanaishukuru sana serikali chini ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan  kwa kuwapatia fedha na hivyo kurejesha mawasiliano ambayo kipindi cha masika barabara zilikatika.

Amesema mvua hizo zilisababisha gharama za usafiri kupanda ila kwa sasa mawasiliano yamerudi na wanaendelea na shughuli zao za kawaida na pia  wanaishukuru TARURA kwa usimamizi wao mzuri kwani sasa hivi barabara zinapitika.
Posted by MROKI On Friday, June 14, 2024 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo