Nafasi Ya Matangazo

March 26, 2024



Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), haijaridhishwa na utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Shule Mpya ya Sekondari ya Kamugegi katika Halmashauri ya Wilaya ya Butiama.
 
Kamati hiyo ikiongozwa na Makamu Mwenyekiti Mheshimiwa Stanslaus Mabula ilitembelea na kukagua mradi huo pomoja na mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Butiama Mkoani Mara.
 
Akizungumza kwa niaba ya Kamati, Mheshimiwa Mabula alisema  pamoja na mapungufu mengi lakini pia Halmashauri haikufanya tathimini katika mchakato wa kupata mafundi kwa ajili ya mradi huo.
 
“Kamati imebaini kuwa hakukuwa na Kamati ya Tathimini katika mchakato wa kupata mafundi na wala hakukuwa na mpango wa manunuzi ,kutokana na dosari hizi majengo mengi hayajakamilika na mengine yamejengwa katika kiwango kisichoridhisha,” alisema.
 
Alisema Kamati inaagiza dosari zote zilizobainishwa zifanyiwe marekebisho ikiwemo kuondoa milango isiyokidhi vigezo pamoja na sakafu ili kuifanya shule hiyo idumu katika miaka mingi ijayo.
 
Kwa upande wa mradi wa Hospitali, Kamati iliagiza Halmshauri kuhakikisha inakamilisha ujenzi wa majengo katika Hospitali hiyo ikwemo jengo la mama na mtoto ili hospitali hiyo iweze kufanya kazi katika ukamilifu wake na thamani ya fedha ionekane.
 
Kamati ya LAAC pia ilitumia fursa hiyo katika ziara yake Wilayani Butiama Mkoa wa Mara, kutembelea Kaburi la Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na kufanya misa fupi ya kumuombea.
Posted by MROKI On Tuesday, March 26, 2024 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo