Naibu
Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko akibonyeza kitufe kuashiria
upatikanaji wa huduma za usafiri wa dharura ya M-mama kwa wajawazito na watoto
katika vituo vyote vya kutoa huduma ya afya msingi katika mikoa yote ya
Tanzania Bara.Kulia kwake ni Naibu
Waziri Ofisi ya Rais - TAMISEMI anaeshughulikia Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe,
Mhe. Festo Dugange na wa kwanza kulia Naibu Waziri wa Afya, Mhe. Dkt. Godwin
Mollel. *******************
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa
Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa umefika wakati wa kuweka Mpango
Mkakati wa kuhakikisha uwekezaji wa miundombinu uliofanywa na Serikali katika
vituo ngazi ya Afya ya Msingi inatunzwa.
Dkt. Biteko ametoa agizo hilo
wakati akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt.
Samia Suluhu Hassan kufungua Mkutano wa Kwanza wa Kimataifa wa Afya ya Msingi
nchini Tanzania tarehe 25 Machi, 2024 jijini Dodoma ambapo amesema kuwa
miundombinu bora inawezesha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi kwa
urahisi zaidi.
Dkt. Biteko amewataka kujadili kwa
kina namna bora ya kubuni mbinu zitakazowezesha kuongeza kasi ya kuajiri
wataalam wa kada mbalimbali za afya hasa zile zenye upungufu mkubwa.
Pia, ameagiza kuainisha
mikakati ya utoaji wa elimu ya afya kwa jamii ili wananchi waelimishwe
kuhusu njia za kuzuia magonjwa, umuhimu wa chanjo na njia zingine za kudumisha
afya bora.
Dkt. Biteko amesisitiza kuimarisha
mifumo ya ufuatiliaji na tathmini ya huduma za afya ya msingi ili kuweza
kufahamu maendeleo ya utekelezaji wa Afua mbalimbali za afya na kutambua maeneo
ya kuboresha.
Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko
ameupongeza Mfumo wa M-mama uliobuniwa na Watanzania .
"Kwa furaha kubwa nasimama
mbele yenu siku ya leo nikifurahia kuona maono ya Serikali ya Awamu ya Sita ya
kuhakikisha mfumo wa usafiri wa dharura kwa wajawazito, waliojifungua na
watoto," amesema Dkt. Biteko.
Amesema, M-mama inaratibiwa katika
hospitali za mikoa kupitia waratibu waliopewa mafunzo kwa kupiga namba 115
ambapo waratibu wa m-mama katika kila mkoa wanaweza kutoa huduma hizo.
"Napenda kuwashukuru wadau wetu
wa maendeleo Vodacom Tanzania, Vodafone Foundation, USAID, Benki ya Dunia na
wadau watekelezaji wa mfumo wa 'Touch Health' na 'Pathfinder International' kwa
mchango wao katika kushirikiana na Serikali kuleta huduma hii inayohitajika kwa
wote," amesisitiza Dkt. Biteko.
Katika hatua nyingine amesema,
serikali imeweza kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kuimarisha miundombinu ya
utoaji huduma ambapo kuanzia mwaka 2017 hadi Januari 2024, jumla ya vituo 2,799
vimejengwa na vingine kufanyiwa ukarabati, zikiwemo Zahanati 1,762, Vituo vya
Afya 910, na Hospitali za Halmashauri 127.
Pia, majengo 83 ya kutolea huduma za
dharura na majengo 28 kwa ajili ya wagonjwa mahututi na nyumba za watumishi
150 zimejengwa. Gharama ya ujenzi na ukarabati huo imefikia shilingi
bilioni 937.2 ikiwa ni hatua muhimu katika kuhakikisha kuwa huduma za afya
zinapatikana kwa kila mtu katika jamii yetu.
Awali, Dkt. Biteko amehimiza
kuwezesha watu, familia na jamii kwa ujumla kuzingatia afya bora na kuhamasisha
utekelezaji wa sera na miongozo inayolenga kulinda afya ya jamii.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa
Afya, Mhe. Godwin Mollel amesema kuwa wataalam wa sekta hiyo wamejitoa
kuhakikisha wanatoa huduma bora ya afya nchini hususan ya msingi na kuwataka
washikamane kujenga sekta hiyo muhimu.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais -
TAMISEMI anaeshughulikia Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe, Mhe. Festo Dugange
amemshukuru Rais Samia kwa kufanya mageuzi katika Sekta ya Afya. Amesema
mkutano huo unawezesha kujadiliana masuala mbalimbali na kubadilishana uzoefu
na namna ya kuboresha afya ya msingi kwa watu wote.
0 comments:
Post a Comment