Nafasi Ya Matangazo

November 18, 2015


Msemaji wa Wizara ya Nishati na Madini Bi. Badra Masoud akiwaeleza waandishi wa habari (hawapo pichani)mapema leo jijini Dar es Salaam kuhusu mpango wa Serikali wa kuunda kikosi maalum cha kukabiliana na tatizo la wizi wa umeme na kuimarisha ukaguzi ili kubaini wateja wasio waaminifu na kuwachukulia hatua za kisheria. Kulia ni Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Habari (MAELEZO) Bi. Zamaradi Kawawa. (Picha na Fatma Salum- Maelezo).
***************
Na Greyson Mwase, Dar es Salaam
Kutokana na wizi wa umeme kukithiri na kuliingizia hasara Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Wizara ya Nishati na Madini imeliagiza Shirika hilo kuimarisha kikosi chake cha ukaguzi wa watumiaji wa umeme ili kubaini wateja wasio waaminifu wanaoiba umeme na kuwachukulia hatua za kisheria.

 Hayo yamesemwa na Msemaji wa Wizara ya  Nishati na Madini Badra Masoud alipofanya mkutano na waandishi wa habari  kwa  ajili ya kuendelezea  mafaniko na changamoto katika usimamizi  wa sekta ya  umeme.

Masoud alisema Wizara inatarajia kuunda kikosi maalum kitakachojumuisha wataalam kutoka katika taasisi mbalimbali kwa ajili  ya  kukabiliana na tatizo hilo linalolikosesha mapato shirika la TANESCO.

Alisema  kikosi hicho kitajumuisha wataalam kutoka TANESCO, Wizara ya Nishati pamoja na vyombo vya usalama na kuongeza kuwa hatua hii imekuja baada ya Wizara kubaini kuwa kuna  baadhi ya watu wanaohujumu miundombinu ya TANESCO kama vile kuchoma nguzo za umeme, kuiba mafuta ya transfoma pamoja na nyaya za umeme  na kuwataka  kuacha kufanya hujuma hizo kwani watakaogundulika wataendelea kuchukuliwa hatua za kisheria.

Akielezea  zoezi  hilo, Masoud alisema kuwa  hivi sasa sasa vyombo vya dola katika mkoa wa Lindi vinaendelea kuwasaka na kuwatia nguvuni wale wote waliohusika kuchoma nguzo za umeme wa msongo mkubwa unaosafirisha umeme kutoka Mtwara kwenda Lindi katika vijiji vya Hingawali na Njonjo mkoani Lindi na kusababisha mikoa hiyo miwili kukosa umeme na kusababisha hasara kwa TANESCO.

Masoud alizitaka  Taasisi mbalimbali za Serikali na zisizo za Kiserikali kuzingatia matumizi bora ya umeme ili kudhibiti upotevu wa nishati ya umeme na kusisitiza kuwa  utaratibu huu wa matumizi bora ya umeme hufanywa pia na nchi nyingi duniani kwa ajili ya kukabiliana na upotevu wa umeme.

Aliongeza kuwa kuna baadhi ya taasisi huwa zinaacha umeme ukiendelea kupotea baada ya muda wa kazi kama vile kuacha  viyoyozi, taa, kompyuta na vifaa vingine vinavyotumia umeme vikiendela kutumia umeme hivyo  kusababisha  upotevu mkubwa  wa umeme ambao  ungetumika katika maeneo mengine au kuokoa fedha ambazo hutumika kuzalisha umeme huo.

Akielezea hali ya upatikanaji wa umeme nchini  Masoud alisema kuwa  hali ya umeme nchini ni nzuri na hakuna mgawo wowote unaoendelea hivi sasa kwani hali ya uzalishaji ni nzuri pamoja na mabwawa ya maji ambayo hutumika kuzalisha umeme kukauka.

Alisisitiza kuwa kiasi cha umeme kinachopatikana kwa sasa ni megawati 1500 huku matumizi ikiwa ni kati ya megawati 800 na 900 kutokana na umeme huo kuzalishwa kwa kiasi kikubwa kutokana na gesi asilia pamoja na mafuta mazito na dizeli.
Posted by MROKI On Wednesday, November 18, 2015 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo