Dar es Salaam
Kundi la wataalamu wa masuala ya nyaraka na uhifadhi wa kumbukumbu kutoka Algeria jana limetembelea Makumbusho ya Taifa la Tanzania kwa lengo la kujifunza mbinu mbalimbali za uhifadhi wa urithi wa kihistoria, nyaraka na kumbukumbu zinazohifadhi historia ya taifa na jamii kwa ujumla.
Ziara hiyo imefanyika sambamba na matembezi yao ya kitaaluma nchini Tanzania yaliyolenga kujifunza mifumo ya usimamizi wa nyaraka na kumbukumbu katika taasisi mbalimbali, ikiwemo Ofisi ya Taifa ya Kumbukumbu. Wakiwa Makumbusho ya Taifa, wageni hao walipata fursa ya kutembelea maonesho mbalimbali yanayoeleza historia ya Tanzania kuanzia enzi za kale, harakati za ukombozi, maendeleo ya kijamii na kiuchumi, pamoja na urithi wa tamaduni za makabila mbalimbali nchini.
Wageni hao walieleza kuvutiwa na namna Makumbusho ya Taifa yanavyotekeleza jukumu la kuhifadhi na kuwasilisha historia kwa njia zinazowezesha kizazi cha sasa na kijacho kujifunza na kuthamini urithi wa taifa. Walibainisha kuwa uzoefu walioupata umeongeza maarifa kuhusu umuhimu wa kuunganisha uhifadhi wa nyaraka, vielelezo vya kihistoria na elimu kwa umma katika kulinda kumbukumbu mbalumbali za kitaifa.
Kwa upande wake, uongozi wa Makumbusho ya Taifa ulieleza kuwa ziara hiyo ni ishara ya kuimarika kwa ushirikiano wa kimataifa katika maeneo ya uhifadhi wa kumbukumbu, historia na urithi wa utamaduni. Aidha, ulisisitiza kuwa makumbusho yanaendelea kuwa kitovu muhimu cha elimu, utafiti na uhifadhi wa kumbukumbu zinazobeba historia na utambulisho wa Tanzania.
Kupitia ziara hiyo, pande zote mbili zimepata fursa ya kubadilishana uzoefu na kujadili mbinu bora za kuhifadhi taarifa na vielelezo vya kihistoria, hatua ambayo inachangia kuimarisha juhudi za kulinda urithi wa kizazi cha sasa na kijacho.
Makumbusho ya Taifa inaendelea kupokea wageni na wataalamu kutoka ndani na nje ya nchi wanaotaka kujifunza historia, utamaduni na mifumo ya uhifadhi wa urithi wa Tanzania, jambo linalodhihirisha nafasi yake muhimu kama taasisi ya kitaifa yenye mchango mkubwa katika elimu, utafiti na uhifadhi wa kumbukumbu za taifa.















0 comments:
Post a Comment