Nafasi Ya Matangazo

February 13, 2025

Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi stadi (VETA) kupitia chuo chake cha VETA Arusha, imezindua Mradi wa kuzalisha Gesi Asilia kwa kutumia Samadi (Biogas), kwa ajili ya matumizi ya wanafunzi na watumishi, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa adhma ya Serikali ya Tanzania ya kuhakikisha matumizi ya nishati safi na endelevu.

Mradi huo wenye thamani ya takribani shilling milioni 156 umezinduliwa rasmi jana, tarehe 12 Februari, 2025, na Profesa Ledislaus Mnyone ambaye ni Mkurugenzi wa Sayansi, Teknolojia na Ubunifu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, akimwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Prof. Carolyne Nombo.

Mradi huo una uwezo wa kuzalisha gesi asilia kiasi cha 50 cc kwa siku, ambayo ina uwezo wa kutumika kupika chakula cha wanafunzi zaidi ya 400 kwa siku na kutumika katika nyumba sita za walimu pamoja na kantini ya chuo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Profesa Ledislaus Mnyone amesema Mradi huo ni sehemu muhimu ya juhudi za Serikali ya Tanzania katika kufanikisha mpango wake wa kuhakikisha matumizi ya nishati safi na endelevu.

“Serikali imejidhatiti kuimarisha matumizi ya nishati safi inayochangia kupunguza utegemezi wa nishati kutoka vyanzo visivyo endelevu kama vile kuni, mkaa na mafuta” amesema Profesa Mnyone.

Amesema Mradi huo unaenda kuleta manufaa makubwa kwa jamii hasa katika kupunguza uchafuzi wa mazingira na kusaidia katika kutunza rasilimali za asili.

“Nawapongeza sana VETA kwa ubunifu huu, kinachoonekana hapa ni matokeo ya agizo alilolitoa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, ambalo nyie mmelitekeleza kwa vitendo, naomba mradi huu uwe endelevu na kuondokana na ile kasumba mradi ukishazinduliwa haufuatiliwi hadi unakufa. Hii imekuwa ikiipatia Serikali hasara kubwa sana, na sasa tutakuwa tunafuatilia maendeleo ya miradi hii,”amesema.

Aidha ametoa wito kwa taasisi zilizokuwa chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuhakikisha teknolojia hiyo inasambazwa kote nchini ili kuokoa gharama kubwa ya matumizi ya kuni, lakini pia kuokoa uharibifu wa mazingira.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa VETA nchini, CPA. Anthony Kasore amesema VETA imeanza kutekeleza Mpango wa Serikali katika kuhakikisha matumizi ya nishati safi ya kupikia katika vyuo vyake hasa katika matumizi ya gesi.

“Kupitia mradi huu tunaenda kupunguza gharama za uendeshaji hasa katika kununua kuni, na mkaa, lakini pia tutahakikisha mradi huu unakuwa endelevu na wenye kuleta matokeo,” Amesema CPA. Kasore.

Hata hivyo, CPA. Kasore amesema kwa kupita mradi huu ameona kuna umuhimu wa kuanzisha kozi ya ufugaji, hasa ufugaji wa ng’ombe na ili kupata samadi kwa ajili ya kulisha mtambo huo wa gesi asilia.

CPA Kasore ameishukuru Serikali ya Korea kusini kupitia Wanasayansi na Wahandisi wasio na Mipaka (SEWB) pamoja na Wizara ya Elimu kuwezesha ujenzi wa mradi huo wa BIOGAS.

Aidha Mkurugenzi wa SEWB, Wiin Soo amesema mradi huo ni matokeo ya mazungumzo kati ya ofisi yake na taasisi ya Tume ya Sayansi Teknolojia (COSTECH), ambayo iliomba msaada wa kusaidiwa kujengewa mtambo huo wa mfano ikiwa ni agizo la Mheshimiwa Rais Samia. 

Posted by MROKI On Thursday, February 13, 2025 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo