MAKUSANYO ya maduhuli ya Serikali kupitia Sekta ya Madini katika Mkoa wa Mbeya yatokanayo na mrabaha, tozo na ada mbalimbali, kwa mwaka wa fedha ulioanza Julai 2024/ 2025 jumla ya Shilingi Bilioni 2.3 zilikusanywa ikiwa ni sawa na asilimia 63 ya lengo la mwaka. Makusanyo hayo ni sawa na asilimia 108 ya lengo la kipindi cha miezi saba (Julai, 2024 mpaka Januari, 2025).
Akizungumza kwa niaba ya Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Mbeya, Mhandisi Migodi, William Kajumla amesema Mkoa wa Mbeya ulipangiwa kukusanya Shilingi Bilioni 3.7.
Amesema, mapato makubwa katika Mkoa wa Mbeya yanatokana na madini ya viwandani, dhahabu na madini ujenzi, pamoja na mapato katika miradi mbalimbali ya barabara.
“Tunategemea mapato kutoka kwenye kiwanda kinachozalisha hewa ya ukaa cha TOL Gas Rungwe, na Kiwanda cha Saruji ‘Mbeya Cement’ kwa madini ya viwandani lakini pia biashara ya dhahabu na machimbo madogo madogo ya madini ujenzi,”amesisitiza.
Aidha, Mhandisi Kajumla ametoa wito kwa watanzania kuchangamkia fursa za uwekezaji zilizopo katika Mkoa wa Mbeya hususan sekta ya madini ujenzi, makaa ya mawe Ngana Kyela na Rungwe na fursa za uwekezaji kwenye uchimbaji na uchenjuaji wa dhahabu kwenye maeneo ya Mabadaga, Msesule na Madibira Wilayani Mbarali na Lwanjiro, Ileya, Ishinda na Chikula Wilayani Mbeya.
0 comments:
Post a Comment