Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
CHEMBA ya Wafanyabiashara wenye viwanda na kilimo (TCCIA) imekutana na watendaji wake wa mikoa yote pamoja na mambo mengine wamejadili namna bora ya kujiimarisha kiutendaji sambamba na kuboreshwaji huduma ya upatikanaji wa vyeti vya uasili (certificate of origin) kidigitali.
Akizungumza kwenye kikao kazi jijini Dar es Salaam jana, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TCCIA, Bi. Mwanahamisi Hussein, alisema chemba imejipanga kuhakikisha kuwa huduma zinazotolewa zinakuwa bora na ufanisi kwa wanachama na watanzania wote kwa kutoa vyeti vya uasili wa bidhaa kwa njia ya kidigitali kwa manufaa ya nchi.
“Tumekubaliana kuboresha matumizi ya TEHAMA ndani ya taasisi yetu (TCCIA) ikiwemo mifumo ya ndani na ile ambayo tunayoitumia kuhudumia jamii ya wafanyabiashara ikiwemo mfumo wa utoaji vyeti vya uasili,” alisema Bi. Hussein.
Alisema uwepo wa teknolojia hiyo umerasimisha zoezi la utoaji vyeti vya uasili wa bidhaa liwe la kidigitali sambamba na mifumo yote ya utoaji wa huduma ya chemba hiyo kuingia kwenye mifumo ya kidigitali ili kuchochea ukuaji wa biashara kwa maslahi mapana ya taifa.
Aidha, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji huyo, alibainisha kuwa miongoni mwa vipaumbele vya chemba kwa sasa ni pamoja na kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo ndani ya nchi sambamba na kuhamasisha matumizi ya teknolojia na kukidhi mahitaji ya soko duniani.
“Ninamshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa namna anavyotupambania sekta binafsi kwa kuweka mazingira rafiki na wezeshi ya ufanyaji biashara na hivyo kuvutia uwekezaji hapa nchini,”alisema Bi. Hussein.
Aliongeza kuwa TCCIA ni taasisi ambayo ina ofisi mikoa yote ambapo kwa sasa inakwenda kuuwisha ushiriki wao kwenye mabaraza ya biashara kuanzia ngazi ya wilaya hadi mikoa ili kufikisha huduma kwa wanachama wake na wafanyabiashara wote kiurahisi.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji wa Chemba hiyo mkoani Tanga, Bw. Charles Hozza alisema mkutano huu umewajengea uwezo watendaji wote wa mikoa na makao makuu pamoja na kufahamu majukumu ya TCCIA kwa kuzingatia utoaji wa huduma bora kwa wanachama.
‘Kupitia kikao kazi hiki tumeweza tumebadilishana uzoefu na maarifa ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya taasisi na hasa katika utoaji wa huduma mbalimbali kwa wanachama wote,”alisema Bw. Hozza.
Naye Afisa Mtendaji wa TCCIA mkoani Kilimajaro, Bw. Boniface Mariki alisema kupitia kikao hicho alisema wameweza kujadili namna bora itakayowawezesha kupata wanachama wapya na kuwafanya wawe wakudumu,
“Nitoe rai kwa wafanyabiashara ambao bado hawajajiunga na chemba wachukue hatua kujiunga sasa kwani wanapishana na fursa nyingi ikiwemo kupata taarifa za masoko ya ndani na nje kuwatengenezea masoko ya kimataifa,” alisema Bw.Mariki.










0 comments:
Post a Comment