October 08, 2023

TCCIA yajipanga kiutendaji sasa kutoa vyeti vya uasili kijiditali

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Chemba ya Wafanyabiashara wenye Viwanda na Kilimo (TCCIA) Bi. Mwanahamisi Hussein, akizungumza na viongozi wa mikoa  wa chemba hiyo (hawapo pichani)  kwenye kikao kazi kilicholenga kujadili namna bora  ya  utendaji kazi sambamba na   uboreshwaji wa huduma ya upatikanaji  wa vyeti vya uasili kwa njia ya kidigitali kilichofanyika  jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.
Meneja   maendeleo ya wanachama kutoka  Chemba ya Wafanyabiashara wenye Viwanda na Kilimo (TCCIA)  Bw. Kelvin Ogodo   akielezea namna chemba hiyo ilivyojipanga kikamilifu katika hutoaji  huduma  kwa wanachama wake kwenye kikao kazi kilichowakutanisha viongozi wa mikoa  wa chemba hiyo jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Chemba ya Wafanyabiashara wenye Viwanda na Kilimo (TCCIA) Bi. Mwanahamisi Hussein, akiwa kwenye picha ya pamoja na  na viongozi wa mikoa  wa chemba hiyo punde mara baada ya kumalizika kwa kikao kazi kilichofanyika jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.
*****************

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

CHEMBA ya Wafanyabiashara wenye viwanda na kilimo (TCCIA) imekutana na  watendaji wake wa mikoa yote pamoja na mambo mengine wamejadili namna bora  ya  kujiimarisha kiutendaji sambamba na   kuboreshwaji huduma ya upatikanaji  wa vyeti vya uasili (certificate of origin) kidigitali.

Akizungumza kwenye kikao kazi jijini Dar es Salaam jana, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TCCIA, Bi. Mwanahamisi Hussein, alisema chemba imejipanga kuhakikisha kuwa  huduma zinazotolewa zinakuwa bora na ufanisi kwa  wanachama  na watanzania wote  kwa kutoa vyeti vya uasili wa bidhaa  kwa njia  ya kidigitali kwa manufaa ya nchi.

“Tumekubaliana kuboresha matumizi ya TEHAMA ndani ya taasisi yetu (TCCIA) ikiwemo mifumo ya ndani na ile ambayo tunayoitumia kuhudumia jamii ya wafanyabiashara ikiwemo mfumo wa utoaji vyeti vya uasili,” alisema Bi. Hussein.

Alisema uwepo wa teknolojia hiyo umerasimisha zoezi la utoaji vyeti vya uasili wa bidhaa liwe la kidigitali sambamba na mifumo yote ya utoaji wa huduma ya chemba hiyo   kuingia kwenye mifumo ya kidigitali ili kuchochea ukuaji wa biashara kwa maslahi mapana ya taifa.

Aidha, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji huyo, alibainisha kuwa miongoni mwa vipaumbele vya chemba kwa sasa ni pamoja na kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo ndani ya nchi sambamba na kuhamasisha matumizi ya teknolojia na kukidhi mahitaji ya soko duniani.

 “Ninamshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa namna anavyotupambania  sekta binafsi kwa kuweka  mazingira rafiki na wezeshi ya ufanyaji biashara na hivyo kuvutia uwekezaji hapa  nchini,”alisema Bi. Hussein.

Aliongeza kuwa TCCIA ni taasisi ambayo ina ofisi mikoa yote ambapo kwa sasa inakwenda kuuwisha ushiriki wao kwenye mabaraza ya biashara   kuanzia ngazi ya wilaya hadi mikoa ili kufikisha huduma kwa wanachama wake na wafanyabiashara wote kiurahisi.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji wa Chemba hiyo mkoani  Tanga,  Bw. Charles Hozza alisema mkutano huu umewajengea uwezo watendaji wote wa mikoa na makao makuu pamoja na kufahamu majukumu ya TCCIA kwa kuzingatia utoaji wa huduma bora kwa wanachama.

‘Kupitia kikao kazi hiki tumeweza tumebadilishana uzoefu na maarifa ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya taasisi na hasa katika utoaji wa huduma mbalimbali kwa wanachama wote,”alisema Bw. Hozza.

Naye Afisa Mtendaji wa TCCIA mkoani  Kilimajaro, Bw. Boniface Mariki alisema kupitia kikao hicho alisema wameweza kujadili namna bora itakayowawezesha kupata wanachama wapya na kuwafanya wawe wakudumu,

“Nitoe rai kwa wafanyabiashara ambao bado hawajajiunga na chemba wachukue hatua kujiunga sasa kwani wanapishana na fursa nyingi ikiwemo kupata taarifa za masoko ya ndani na nje  kuwatengenezea masoko ya kimataifa,” alisema Bw.Mariki.

No comments:

Post a Comment