Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akizungumza kwa njia ya simu na Kansela wa Ujerumani Mhe. Angela Merkel Ikulu Jijini Dar es salaam leo Sept 01,2021.
**********
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia
Suluhu Hassan, leo tarehe 01 Septemba, 2021 amefanya mazungumzo kwa njia ya
simu na Kansela wa Ujerumani Mhe. Angela Merkel.
Katika mazungumzo hayo, Mhe. Merkel amempongeza Mhe.
Rais Samia kwa kushika hatamu ya Urais nchini Tanzania na kumpa pole kufuatia
kifo cha aliyekuwa Rais wa Awamu ya tano Hayati Dkt. John Pombe Magufuli.
Mhe. Merkel amempongeza Mhe. Rais Samia kwa jitihada
zake za kupambana na UVIKO 19 na kuahidi kuunga mkono jitahada hizo kwa kutoa
msaada wa chanjo za kukabiliana na ugonjwa huo.
Aidha, Mhe. Merkel amesema mwezi Oktoba mwaka huu, Serikali
yake itaanzisha majadiliano na Serikali ya Tanzania kuhusu mpango mpya wa
ushirikiano wa maendeleo kwa mwaka 2021 hadi mwaka 2024.
Pia, Mhe. Merkel amempongeza Mhe. Rais Samia kwa
jitihada zake za kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini ambapo
ameahidi kuwashawishi wafanyabiashara wa Ujerumani na watalii kutembelea na
kuwekeza nchini Tanzania.
Kwa upande wake Mhe. Rais Samia amemshukuru Mhe.
Merkel kwa ushirikiano wake na Tanzania katika nyanja mbalimbali za maendeleo.
Mhe. Rais Samia amempongeza Mhe. Merkel kwa kumaliza
kipindi chake cha uongozi akiwa ni kiongozi wa kisiasa mwanamke aliyeongoza
muda mrefu ndani ya Chama chake cha Christian
Democratic Union (CDU) na ndani ya Jumuiya ya Ulaya.







0 comments:
Post a Comment