September 02, 2021

RAIS SAMIA AFANYA MAZUNGUMZO NA KANSELA WA UJERUMANI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akizungumza kwa njia ya simu na Kansela wa Ujerumani Mhe. Angela Merkel Ikulu Jijini Dar es salaam leo Sept 01,2021.
**********

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, leo tarehe 01 Septemba, 2021 amefanya mazungumzo kwa njia ya simu na Kansela wa Ujerumani Mhe. Angela Merkel.

Katika mazungumzo hayo, Mhe. Merkel amempongeza Mhe. Rais Samia kwa kushika hatamu ya Urais nchini Tanzania na kumpa pole kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Awamu ya tano Hayati Dkt. John Pombe Magufuli.

Mhe. Merkel amempongeza Mhe. Rais Samia kwa jitihada zake za kupambana na UVIKO 19 na kuahidi kuunga mkono jitahada hizo kwa kutoa msaada wa chanjo za kukabiliana na ugonjwa huo.

Aidha, Mhe. Merkel amesema mwezi Oktoba mwaka huu, Serikali yake itaanzisha majadiliano na Serikali ya Tanzania kuhusu mpango mpya wa ushirikiano wa maendeleo kwa mwaka 2021 hadi mwaka 2024.

Pia, Mhe. Merkel amempongeza Mhe. Rais Samia kwa jitihada zake za kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini ambapo ameahidi kuwashawishi wafanyabiashara wa Ujerumani na watalii kutembelea na kuwekeza nchini Tanzania.

Kwa upande wake Mhe. Rais Samia amemshukuru Mhe. Merkel kwa ushirikiano wake na Tanzania katika nyanja mbalimbali za maendeleo.

Mhe. Rais Samia amempongeza Mhe. Merkel kwa kumaliza kipindi chake cha uongozi akiwa ni kiongozi wa kisiasa mwanamke aliyeongoza muda mrefu ndani ya Chama chake cha Christian Democratic Union (CDU) na ndani ya  Jumuiya ya Ulaya.

No comments:

Post a Comment