September 21, 2016

RAIS MAGUFULI ATUMA SALAMU ZA RAMBIRAMBI VIFO VYA WATU 13 MWANZA

Rais Dkt. John Pombe Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Bw. John Mongella kufuatia vifo vya watu 13 vilivyosababishwa na ajali ya barabarani iliyotokana na basi la abiria la Kampuni ya Super Shem kuligonga basi dogo la abiria (Daladala) katika kijiji cha Mwamaya kilichopo katika Kata ya Hungumalwa, Wilaya ya Kwimba Mkoani Mwanza.

Ajali hiyo imetokea leo tarehe 21 Septemba, 2016 Majira ya saa 12:15 Asubuhi baada ya basi hilo dogo lililokuwa likitoka Kijiji cha Shirima kwenda Nyegezi Mjini Mwanza kuingia ghafla barabara kuu na kisha kugongwa na basi la Kampuni ya Super Shem lililokuwa likitoka Mkoani Mbeya kwenda Mwanza.

Katika ajali hiyo watu wote 13 waliopoteza maisha na majeruhi 15 waliolazwa hospitali walikuwa abiria wa basi dogo lililogongwa.

Rais Magufuli ameelezea kupokea taarifa za ajali hiyo kwa mshituko mkubwa hasa ikizingatiwa kuwa imetokea ikiwa ni siku moja tu tangu Watanzania wengine 12 wapoteze maisha katika ajali ya basi la Kampuni ya New Force iliyotokea katika kijiji cha Lilombwi, Kata ya Kifanya, Tarafa ya Igominyi Mkoani Njombe.

"Nimesikitishwa sana na vifo vingine vya watanzania wenzetu waliopoteza maisha katika ajali huko Mwanza, nakuomba Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Bw. John Mongella unifikishie salamu za pole kwa familia zote zilizopoteza ndugu, jamaa na marafiki katika ajali hii.

"Nawaombea wote waliotangulia mbele za haki wapumzishwe mahali pema na pia wote walioguswa na msiba wawe na moyo wa subira, uvumilivu na ustahimilivu katika kipindi kigumu cha majonzi ya kuondokewa na jamaa zao" Amesisitiza Rais Magufuli.

Rais Magufuli pia amewaombea majeruhi wote wa ajali hii wapone haraka  ili waungane na familia zao na kuendelea na shughuli za ujenzi wa Taifa.

No comments:

Post a Comment