Rais Dkt. John Pombe Magufuli amemtumia salamu za rambirambi
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Bw. John Mongella kufuatia vifo vya watu 13
vilivyosababishwa na ajali ya barabarani iliyotokana na basi la abiria la
Kampuni ya Super Shem kuligonga basi dogo la abiria (Daladala) katika kijiji cha Mwamaya kilichopo katika Kata ya
Hungumalwa, Wilaya ya Kwimba Mkoani Mwanza.
Ajali hiyo
imetokea leo tarehe 21 Septemba, 2016 Majira ya saa 12:15 Asubuhi baada ya basi
hilo dogo lililokuwa likitoka Kijiji cha Shirima kwenda Nyegezi Mjini Mwanza
kuingia ghafla barabara kuu na kisha kugongwa na basi la Kampuni ya Super Shem
lililokuwa likitoka Mkoani Mbeya kwenda Mwanza.
Katika ajali hiyo
watu wote 13 waliopoteza maisha na majeruhi 15 waliolazwa hospitali walikuwa
abiria wa basi dogo lililogongwa.
Rais Magufuli
ameelezea kupokea taarifa za ajali hiyo kwa mshituko mkubwa hasa ikizingatiwa
kuwa imetokea ikiwa ni siku moja tu tangu Watanzania wengine 12 wapoteze maisha
katika ajali ya basi la Kampuni ya New Force iliyotokea katika kijiji cha
Lilombwi, Kata ya Kifanya, Tarafa ya Igominyi Mkoani Njombe.
"Nimesikitishwa
sana na vifo vingine vya watanzania wenzetu waliopoteza maisha katika ajali
huko Mwanza, nakuomba Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Bw. John Mongella unifikishie
salamu za pole kwa familia zote zilizopoteza ndugu, jamaa na marafiki katika
ajali hii.
"Nawaombea
wote waliotangulia mbele za haki wapumzishwe mahali pema na pia wote walioguswa
na msiba wawe na moyo wa subira, uvumilivu na ustahimilivu katika kipindi
kigumu cha majonzi ya kuondokewa na jamaa zao"
Amesisitiza Rais Magufuli.
Rais Magufuli pia
amewaombea majeruhi wote wa ajali hii wapone haraka ili waungane na familia zao na kuendelea na
shughuli za ujenzi wa Taifa.
0 comments:
Post a Comment