Nafasi Ya Matangazo

March 24, 2012

Chama Cha Mapinduzi kinatarajia kupokea Ujumbe  wa Wafanyabiashara Maarufu kutoka Chama rafiki cha ANC (African National Congress) cha Afrika ya Kusini. Ujumbe huo utawasili nchini tarehe 25/03/2012 na kurejea Afrika Kusini tarehe 29/03/2012.
 
Itakumbukwa kuwa katika maamuzi ya kufanya mageuzi ndani ya Chama yanayoendelea, Chama Cha Mapinduzi kiliamua kuongeza juhudi katika kukifanya Chama kipunguze au kumaliza kabisa utegemezi wa ruzuku katika kuendesha mambo yake.  Hivyo basi, ziara hii ni sehemu ya utekelezaji wa maamuzi hayo.
 Malengo ya ziara hii:-

(i)      Kutafuta fursa mbalimbali za uwekezaji ambazo zitasaidia kudumisha na kuendeleza uhusiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya ANC na CCM.

(ii)     Kubadilishana uzoefu kati ya Makampuni ya ANC na yale ya CCM na kujifunza kutokana na mafanikio waliyoyapata katika eneo la kiuchumi na kibiashara.

 (iii)   Kuonana na Viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali hapa nchini.

(iv)    Kushiriki kongamano la kibiashara litakaloandaliwa na Tanzania Chamber of Commerce, Industries and Agriculture (TCCIA) litakalofanyika Dar es Salaam tarehe 27/03/2012.

(v)     Kutembelea Kambi za Mazimbu Morogoro. Kambi hizi za kihistoria zilitumika kuandaa Wapigania Uhuru wa Chama Cha ANC wakati wa harakati za Ukombozi.
  
Manufaa ya ziara hii kwa CCM.

Pamoja na mambo mengine, Chama Cha Mapinduzi kinatarajia kutumia ziara hii kwa mambo yafuatayo:-

(i)      Chama kitajifunza na kuongeza ujuzi katika mbinu na mikakati ya kuondokana na utegemezi wa ruzuku katika uendeshaji wa shughuli zake.

(ii)     Chama kitatumia fursa hii kubainisha fursa mbalimbali za kiuchumi na kibiashara zilizopo katika Chama zinazofaa kwa shughuli za uwekezaji wa miradi mikubwa na kuzitangaza.

(iii)    Watendaji Wakuu wa Makampuni ya Chama wote wameelekezwa kushiriki kikamilifu, hatua ambayo itawasaidia kujifunza na kupata uzoefu kutokana na mafanikio makubwa ya Makampuni ya ANC katika kusimamia na kuendesha shughuli za kiuchumi na kibiashara.

(iv)    Wataalam mbalimbali wa Chama pamoja na Jumuiya zake watashiriki pia katika kongamano la kibiashara la tarehe 27/03/2012 kwa madhumuni ya kujifunza na kupata uzoefu katika uanzishaji, usimamizi na uendeshaji wa vitega uchumi vya Chama.

Ni matarajio ya Chama Cha Mapinduzi kuwa kutokana na uzoefu mkubwa na wa muda mrefu walio nao wenzetu wa Chama Cha ANC katika kuanzisha, kusimamia na kuendesha vitega uchumi; Chama Cha Mapinduzi kitapata fursa nzuri ya kujifunza mambo mengi hususan katika eneo la uwekezaji wa ubia na matumizi bora ya raslimali za Chama.

Kupitia uzoefu wao tunatarajia Chama kitapiga hatua katika jitihada zake za kupunguza utegemezi mkubwa wa fedha za ruzuku zinazotolewa na Serikali kwa Vyama Vya Siasa katika shughuli za uendeshaji na zile za Kisiasa.

Imetolewa na:
Nape Moses Nnauye,
KATIBU WA HALMASHAURI KUU YA TAIFA
 ITIKADI NA UENEZI
24/03/2012
Posted by MROKI On Saturday, March 24, 2012 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo