Na Mwandishi Maalumu – Dar es Salaam
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge ameibuka mshindi wa Tuzo ya Mkurugenzi Mtendaji Bora wa Mwaka 2025 iliyotolewa na kampuni ya Eastern Star Consulting Group kwa ushirikiano na CEO Roundtable South Africa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge ameibuka mshindi wa Tuzo ya Mkurugenzi Mtendaji Bora wa Mwaka 2025 iliyotolewa na kampuni ya Eastern Star Consulting Group kwa ushirikiano na CEO Roundtable South Africa.
Tuzo hiyo imetolewa hivi karibuni katika Ukumbi wa SuperDome jijini Dar es Salaam, wakati wa hafla maalumu ya kuwatambua viongozi 100 bora na mahiri barani Afrika wanaotoa mchango mkubwa katika maendeleo ya jamii.
Kwa mujibu wa waandaaji, tuzo hizo hutolewa kwa watendaji wanaodhihirisha ubunifu, uwajibikaji na matokeo chanya katika utendaji wao wa kila siku.
Dkt. Kisenge ametambuliwa kwa uongozi wake thabiti unaoweka mbele maslahi ya wananchi, hususan katika kuboresha huduma za tiba ya moyo nchini—jukumu ambalo limeifanya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kuwa kitovu muhimu cha matibabu ya moyo katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Kupatikana kwa Dkt. Kisenge katika orodha ya viongozi 100 bora Afrika ni ishara ya kutambuliwa kimataifa kwa jitihada zake za kusimamia rasilimali, kuboresha miundombinu ya tiba na kuikuza taasisi ya JKCI katika ngazi ya kimataifa.
Chini ya uongozi wake, JKCI imepanua wigo wa huduma za uchunguzi na upasuaji wa moyo, huku idadi ya wagonjwa wanaopatiwa matibabu ndani ya nchi ikiongezeka kwa kasi. Huduma mpya za kitabibu zimeanzishwa, wataalamu wa ndani wamejengewa uwezo kupitia mafunzo ya kisasa na taasisi imeendelea kutekeleza miradi ya utafiti inayolenga kupunguza mzigo wa magonjwa ya moyo nchini.
Baadhi ya wagonjwa wanaohudumiwa na JKCI wamepongeza ushindi huo wakisema ni uthibitisho wa ubora wa huduma na uwajibikaji wa uongozi wa taasisi hiyo.
“Nimekuwa nikitibiwa hapa kwa miezi kadhaa na nimeona jinsi huduma zilivyo bora na za haraka. Kila mfanyakazi anaonekana kujituma na kuwajali wagonjwa. Bila shaka tuzo hii anastahili kabisa kuipata Mkurugenzi wao,” alisema Asha Bakari mmoja wa wagonjwa.
Joseph Mushi anayehudumiwa na taasisi hiyo kwa muda mrefu alisema tuzo hiyo ni fahari sio tu kwa JKCI bali pia kwa wananchi wanaonufaika na huduma zake.
“Zamani tulisikia watu wakisafiri kwenda nje ya nchi kutibiwa, lakini sasa huduma bora zinapatikana hapa hapa nchini. Uongozi wa Dkt. Kisenge umeleta mageuzi makubwa,” alisema.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na washiriki kutoka nchi mbalimbali ikiwemo Tanzania, Kenya, Uganda, Zambia, Malawi na Afrika Kusini ambapo viongozi waliotoa mchango mkubwa katika sekta zao wametambuliwa rasmi.






0 comments:
Post a Comment