Mhe. Rais Jakaya Mrisho Kikwete ametoa shukurani kwa wananchi wote kwa kufanikisha mazungumzo kati yake na wao, usiku wa jana, Jumatano, Septemba 9, 2009, kwa njia ya vyombo vya utangazaji vya televisheni na redio.
Aidha, Mhe. Rais Kikwete amewashukuru wananchi wote waliopata nafasi za kumuuliza maswali, kutoa ushauri wao, hoja zao, kero zao ama kwa njia ya simu za moja kwa moja, ama kupitia njia ya barua pepe ama ujumbe mfupi kwa njia ya simu, SMS.
Mhe. Rais vile vile amevishukuru vyombo vya habari nchini kwa kuandika na kutangaza vizuri tukio hilo kabla ya kufanyika, wakati likifanyika na baada ya kuwa yamemalizika mazungumzo hayo.
Amesema Mhe. Rais Kikwete: “Nimefurahi na nimefarijika sana kwa kupata nafasi ya kuzungumza moja kwa moja na wananchi kwa namna ya kujibu maswali yao, kusikiliza ushauri wao, kupata hoja zao na maoni yao kuhusu mustakabali wa nchi yetu, Serikali yetu, na maendeleo yetu.”
Mhe. Rais amesema kuwa amefurahi kuwa wananchi wamejitokeza kwa wingi kushiriki kwa namna moja ama nyingine katika mazungumzo hayo. Mamia kwa mamia ya barua pepe na sms yalipokelewa kwa ajili ya mjadiliano hayo kati ya Mhe. Rais na wananchi.
Amefafanua Mhe. Rais “Kila mmoja wetu ameshiriki kwa namna yake. Wengine kwa kuuliza maswali ya moja kwa moja, wengine kwa kutoa ushauri na hoja zao kwa njia ya e-mail na sms, wengine kwa kusikiliza mazungumzo kwenye redio, kuyafuatilia mazungumzo kwenye televisheni, kusoma kwenye magazeti na wengine kwa kutuhabarisha kuhusu mazungumzo hayo. Sote ni washiriki. Na nawashukuruni wote.”
Mhe. Rais amesisitiza kuwa Serikali yake imesikia maswali, maoni, hoja na ushauri, na kwamba inayachukuliwa yote kwa makini mkubwa na inapanga kuona jinsi gani itayatekeleza kwa kutilia maanani Ilani ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2005, na raslimali za Bajeti ya Serikali.
Aidha, Mhe. Rais Kikwete amerudia kauli yake kwenye mazungumzo hayo kuwa barua pepe zote pamoja na sms ambazo zilielekezwa kwake, lakini hoja za sms hizo hazikuweza kufafanuliwa kwa sababu ya ufinyu wa muda, zinatafutiwa nafasi ya kujibiwa kwa namna moja ama nyingine.
Vile vile Mhe. Rais amerudia tena kusema kuwa mazungumzo ya jana usiku yalikuwa moja ya njia za kuboresha mawasiliano ya moja kwa moja kati yake na wananchi, na kuwa njia nyingine, zitatangazwa kwa wakati mwafaka.
Kwa sababu ya kukamilika kwa tukio hilo la mazungumzo kati ya wananchi na Mhe. Rais, upokeaji maswali, maoni, hoja na ushauri kwa njia ya barua pepe na sms utasimama kuanzia saa 12, jioni ya leo, Alhamisi, Septemba 10, 2009.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu,
DAR ES SALAAM.
10 Septemba, 2009
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu,
DAR ES SALAAM.
10 Septemba, 2009
0 comments:
Post a Comment