Nafasi Ya Matangazo

March 16, 2024







Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde leo Machi 16, 2024 kwa nyakati tofauti  ameongoza timu za mpira wa miguu  za Tume ya Madini Makao Makuu na Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kwenye michezo ya bonanza ya Tume ya Madini iliyofanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari ya John Merlin jijini Dodoma.

 Michezo mbalimbali iliyofanyika katika bonanza hilo  ni pamoja na riadha, kuvuta kamba, mpira wa miguu, kukimbiza kuku n.k.

Viongozi wa Tume ya Madini walioshiriki katika bonanza hilo ni pamoja na  Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula, Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Eng. Yahya Samamba, Wakurugenzi, Mameneja na Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa.

Akizungumza kwenye bonanza hilo mara baada ya kumalizika kwa michezo mbalimbali, Waziri Mavunde amesema kuwa michezo inaimarisha umoja na kuitaka Tume ya Madini kuendelea kuboresha mabonanza mengine.

Sambamba na kuwapongeza washindi wa michezo mbalimbali na kugawa vikombe, amesema kuwa kama njia mojawapo ya kuimarisha umoja katika Sekta ya Madini Wizara ina mpango wa kuandaa bonanza kubwa litakaloshirikisha Wizara ya Madini na Taasisi zake na wadau wa madini nchini.

Aidha, amepongeza kazi kubwa inayofanywa na Tume ya Madini kwenye usimamizi wa Sekta ya Madini na kuongeza kuwa Wizara ya Madini itaendelea kutoa ushirikiano na kutatua changamoto zote kwenye utendaji kazi.

Awali wakati akizungumza kwenye bonanza hilo, Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula sambamba na kumpongeza Waziri Mavunde kwa ushiriki wa bonanza hilo amesema kuwa uongozi wa Tume umekuwa ukifanya ziara kwenye ofisi za maafisa madini wakazi wa mikoa na kutatua changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa vitendea kazi na kuhamasisha umoja ili kuboresha utendaji kazi.

Katika hatua nyingine, Profesa Kikula amepongeza kazi nzuri inayofanywa na Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa hasa kwenye ukusanyaji wa maduhuli na kuongeza kuwa Tume ya Madini itaendelea kuboresha mazingira ya kazi ikiwa ni pamoja na maboresho ya ofisi na masoko ya madini.

Wakati huohuo, Waziri Mavunde amekabidhiwa medani ya heshima kwa kutambua mchango wake mkubwa kwenye Usimamizi wa Sekta ya Madini na ushiriki wa bonanza ambapo amekabidhiwa na Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula.
Posted by MROKI On Saturday, March 16, 2024 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo